MWANAMKE AZIKWA, ARUNDIKIWA VYOMBO JUU YA KABURI LAKE - LEKULE

Breaking

14 Jul 2015

MWANAMKE AZIKWA, ARUNDIKIWA VYOMBO JUU YA KABURI LAKE

Wahenga walisema ukisitajabu ya Musa utaona ya Farao, hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wananchi wa mji wa Bariadi mkoani Shinyanga waliofurika katika kaburi la marehemu, Jesca Onesmo (28), ambaye alifariki kisha kuwekewa samani na vyombo vyake mbalimbali juu ya kaburi lake.

Ilikuwa asubuhi ya saa mbili, Julai 7, mwaka huu ambapo baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Marambo, Bariadi waliokuwa wamepata msiba walipokwenda eneo la Makaburi ya Kidinda kwa ajili ya kutafuta mahali pa kuchimba kaburi, walipofika eneo hilo walipigwa na butwaa baada ya kuona  kaburi moja likiwa limewekewa vitu juu, hali ambayo ilitafsiriwa kuwa amezikwa navyo.
Uwazi baada ya kupewa habari hiyo lilifika katika eneo hilo na kukuta samani za ndani, godoro na vyombo mbalimbali vikiwa vimerundikwa juu ya kaburi hilo na baada ya uchunguzi ikajulikana kuwa ni kaburi la Jesca.
Mwananchi mmoja ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema: “Kwa kweli hili ( la kurundikwa vyombo vyake juu ya kaburi) limetushangaza sana na ni la kwanza kutokea hapa Bariadi, hata sisi hatujui sababu lakini labda ni ushirikina.”
Baada ya tukio hilo polisi waliarifiwa ambapo walifika makaburini na kuamua kuvipakia vyombo hivyo kwenye gari la polisi na kuvipeleka kituoni na baada ya kufika huko walivifanyia upekuzi na kugundua vitu mbalimbali.
Habari za kipolisi zinasema walikuta pochi ya marehemu ambayo ndani yake ilikuwa na shilingi 13,000 pamoja na simu ndogo lakini pia walifanikiwa kukuta cheti cha hospitali kilichoonesha marehemu alikuwa mgonjwa na alikuwa anatumia dawa kila siku.
Aidha, walipata pia daftari la mchango wa kifo ambalo lilionesha kuwa alichangiwa na walipata jina na namba za simu ya dada yake (jina linahifadhiwa) ambaye inadaiwa kuwa ndiye aliyehusika kumzika ingawa baada ya kumpigia simu hakupokea na walipomfuatilia walikuta ametoroka na familia yake, hadi sasa haijafahamika alipo.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo kutangazwa na vyombo vya habari baadhi ya wananchi walidai kuwa marehemu alikuwa anaishi na mume wake huko wilayani Kahama na hawakujua nini kilitokea hadi kuzikwa na kurundikiwa vyombo juu ya kaburi lake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP  Gemini Mushy amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
“Tukio hilo lipo lakini tunaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo chake na sababu ya kumzika na vyombo vyake,” alisema kamanda huyo.

No comments: