MAMBO 5 YALIYOMPONZA… LOWASSA - LEKULE

Breaking

14 Jul 2015

MAMBO 5 YALIYOMPONZA… LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani na aliyekuwa mtangaza nia ya kugombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, Edward Lowassa akipokea fomu zilizosainiwa na wadhamini wake.
TAYARI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtangaza Waziri wa Ujenzi, John Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea urais mwaka huu huku Samia Suluhu Hassan akiwa mgombea mwenza, lakini bado jina la mgombea aliyekatwa, Edward Lowassa linazungumzika, safari hii yakibainishwa mambo matano yanayoolezwa ndiyo yalichangia kukatwa kwake.

Akizungumza na Uwazi juzi mjini hapa kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya CCM-Taifa (Nec) alisema nguvu ya Lowasaa kichama ilikuwa kubwa lakini mambo hayo matano ndiyo yalisababisha akashindwa kufikia hata hatua ya Tano Bora.
…Akisaini katika kitabu cha wageni kwnye moja ya ofisi za CCM mikoani.

“Sisi kama wajumbe, tunajua mengi. Lowassa alikuwa mgombea mwenye nguvu, alikuwa na watu ndani ya Nec, lakini sasa Kamati Kuu (CC) ilimkata kwa vigezo vyake, lakini naamini ndani ya hayo mambo matano ndiyo maana alikatwa.

MAKANISA, MISIKITI YATAJWA

Kwa mujibu wa mjumbe huyo kutoka Mkoa wa Tanga, kitendo cha Lowassa kuchagisha fedha kwa njia ya harambee kwenye misikiti na makanisa akiwa kama mgeni mwalikwa, kulichangia CC ya CCM  kumwona kama alianza kampeni mapema.
“Unajua ndani ya makanisa mengi yanasemwa. Baadhi ya watu ndani ya chama chake walisema alianza kampeni mapema kwa vile kule kuzungumza na waumini kuliweza kumpa nguvu ya kisiasa. Hii nayo ilichangia,” alisema mjumbe huyo.
…Akikusanya fomu za zilizosainiwa na wadhamini.

STAILI YA KUTANGAZA NIA
Mjumbe huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, jambo la pili ambalo lilimtia doa ya kuteuliwa Lowassa ni staili aliyoitumia kutangaza nia.
Alisema: “Unajua CCM inakataza kabisa mtu mwenye kutangaza nia kufanya vitendo vyovyote vyenye dalili ya kampeni. Lowassa alipoyakaribisha yale makundi ya kumshawishi kugombea na kuzungumza na vyombo vya habari pia ilikuwa ni kigingi kwake. Kama itakumbukwa kuwa, kuna wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ilibidi aseme.”

KUFUNGIWA NA KAMATI
“Pia itakumbukwa kuwa, Februari 18, mwaka jana, Kamati Kuu ya CCM iliwafungia makada wake sita kwa kosa la kuanza kampeni mapema jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa chama.
“Lowassa alikuwemo, lakini wengine pia walikuwemo kama Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Januari Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema), na Frederick Sumaye (waziri mkuu msatafu).
“Sasa, walipofunguliwa, Lowassa alionekana kama anaendelea kwa kitendo chake cha kuzungumza na wananchi kwa kupitia kigezo cha makundi kwenda kumshawishi,” alisema mjumbe huyo.

MATAJIRI, WAFANYABIASHARA WAKUBWA
Kitendo cha kudaiwa kuwa na ukaribu na baadhi ya matajiri na wafanyabiashara wakubwa ambao wanatiliwa shaka na baadhi ya wananchi pia kunatajwa kuwa sababu ya CC kuamua kumuweka kando Lowassa.

DOA LA RICHMOND
Licha ya mwenyewe kuwahi kusema mbele ya mkutano mkuu wa Nec wakati fulani kwamba, katika mchakato wa upatikanaji wa tenda ya kufua umeme kwa Kampuni ya Richmond, hakuna alilolifanya bila serikali kuu kujua lakini bado doa lile lililosababisha akajiuzulu uwaziri mkuu limeonekana kuwa kikwazo kwake.

“Ni kweli Lowassa alijiuzulu kwa sababu ya nafasi yake lakini si kwamba alihusika na ufisadi. Lakini nahisi iko haja kwake kuweka bayana kuhusu ule mchakato kwani baadhi ya wanasiasa wenzake wamekuwa wakitumia ishu ile kama jiwe la kumpigia.
“CC iliona kwamba, kama wangempeleka yeye kwenye kinyang’anyiro labda wapinzani wangetumia sakata la Richmond kujizolea kura kwa madai kwamba, Lowassa alijiuzulu kwa sababu hiyo,” alisema mjumbe huyo.

KUTOKA NDANI ZAIDI
Hata hivyo, pia kuna madai kwamba, wajumbe wa CC walimtafakari Lowassa kwa umakini na kugundua kuwa, alitakiwa kukatwa jina mapema kabla ya kuingia kwenye Tabo Bora.
“Kama Kamati Kuu ya CCM ingempitisha Lowassa kwenye Tano Bora, hakuna ambaye angemshinda mbele ya safari kwenye Nec na Mkutano Mkuu. Alikuwa na nguvu kubwa kwa wajumbe. Ndiyo maana wakamdhibiti kule mwanzoni kabisa,” kilisema chanzo kimoja na kuongeza:
“Lakini hata Nec na Mkutano Mkuu walipopelekewa jina la Magufuli walifurahia kwa sababu hana makundi ndiyo maana akazoa hizi kura 2104 na ndiye mgombea aliyepeleka hofu kwenye vyama vya upinzani (Ukawa) kwa sababu hana kashfa.”

KISA CHA KUKATWA MEMBE
Chanzo hicho kilisema kuwa, Bernard Membe ilibidi akatwe ili kutuliza upepo wa kisiasa ndani ya chama.

“Unajua Membe ndiye aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Lowassa. Kuingia kwake kwenye Tano Bora na kuachwa Lowassa kusema kweli kulizua taharuki kubwa. Baadhi ya watu walikusudia kuibua uasi. Ndiyo maana ukawasikia wajumbe wakiimba wana imani na Lowassa wakati mwenyekiti wetu (Jakaya Kikwete) akiingia ukumbini.

“Ilibidi jina la Membe likatwe ili kambi ya Lowassa waone kifo cha wengi ni harusi na upepo mbaya ukatulia ndani ya chama la sivyo mpaka leo (Jumapili) kungekuwa bado Tano Bora iko mikononi mwa wajumbe wa Nec,” kilisema chanzo hicho.

No comments: