Watoto 92 Wanaishi na Virusi Vya Ukimwi Bunda - LEKULE

Breaking

22 Jun 2015

Watoto 92 Wanaishi na Virusi Vya Ukimwi Bunda

IMEELEZWA kuwa katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, kuna watoto wanaofikia 92 wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
 
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Bunda, Caroline Wanzagi.
 
Wanzagi alisema kuwa watoto hao wanaendelea kupata huduma ya matibabu na misaada mbalimbali kutoka katika mashirika, taasisi na serikalini.
 
Alisema kuwa watoto hao wamepata maambukizi hayo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuyapata kutoka kwa mama zao wenye maambukizi, unyanyasaji wa kijinsia ukiwamo ubakaji na ajira hatarishi.
 
Alisema kuwa ili kupunguza idadi ya maambukizi ya VVU kwa watoto kutoka kwa mama mwenye maambukizi au maambukizi yanayoweza kutokea kwa watoto kutokana na unyanyasaji, ubakaji na ajira hatarishi, ni muhimu kuelimisha jamii juu ya changamoto hiyo, ili kuzuia maambukizi hayo.
 
Aliongeza kuwa pia ili kukabiliana na changamoto hiyo ni muhimu wazazi wote yaani mama mwenye ujauzito na baba wahudhurie huduma za klini, ili kumsaidia mtoto aliyeko tumboni kuzaliwa bila maambukizi ya VVU.
 
Alisema kuwa hali hiyo itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU, kwa kuwa wazazi wote watawajibika katika afya zao na afya ya mtoto, ikiwa ni pamoja na mtoto kupata huduma ya option B kwa mama ndani ya masaa 72 kabla ya uchungu.
 
“Hii itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU kwa kuwa wazazi wote watawajibika katika afya zao na afya ya mtoto, ikiwa pia na mama kupata huduma ya ndani ya masaa 72 kabla ya uchungu,” alisema.
 
Alisema kuwa baba na mama kuhudhuria klini itasaidia baba kufanya maandalizi ya kumwezesha mama kujifungulia kwenye kituo cha afya au hospitalini na hivyo kumkinga mtoto asipate maambukizi ya VVU, ikiwa ni pamoja na kuondoa usiri wa matumizi ya ARV.

No comments: