Serikali Kushusha Ushuru wa Mafuta leo? - LEKULE

Breaking

22 Jun 2015

Serikali Kushusha Ushuru wa Mafuta leo?

SERIKALI leo inatazamiwa kujibu hoja mbalimbali zilizoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/16.
 
Mbali na Wizara ya Fedha ambayo itakuwa na mengi ya kufafanua au kurekebisha kutokana na mapendezo yake mbalimbali yaliyomo kwenye Bajeti, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Dk Mary Nagu, naye atakuwa na ‘kibarua’ cha kujibu hoja za wabunge kutokana na taarifa yake ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa katika mwaka ujao wa fedha alioiwasilisha bungeni siku ambayo Bajeti ilisomwa, Juni 11, mwaka huu.
 
Moja ya hoja inayotarajiwa kutolewa ufafanuzi au kufanyiwa marekebisho na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya pamoja na manaibu wake, Adamu Malima na Mwigulu Nchemba kabla ya Bejeti ya Serikali kupitishwa kwa kupigiwa kura, ni ongezeko la tozo ya nishati ya mafuta.
 
Katika bajeti ijayo, Serikali inapendekeza kuongeza tozo ya mafuta ya dizeli kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita; petroli kutoka Sh 50 hadi Sh 100 kwa lita na mafuta ya taa kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 150. Kuhusu mafuta ya taa ilielezwa kwamba ongezeko hilo litasaidia pia kuondoa uchakachuaji.
 
Tozo hiyo ambayo fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kupelekwa kwenye Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) iliwagawa wabunge katika makundi mawili; moja likiipinga na lingine likiiunga mkono.
 
Wale wanaopinga wanasema itaongeza mzigo kwa wananchi kwa kuwa nishati hizo zinapoguswa zina athari nyingi za kuendelea lakini wale wanaounga mkono tozo hiyo wanasema ni ndogo kulinganisha na umuhimu wake na kwamba maendeleo hayawezi kuja bila kuyatolea jasho.
 
 Suala la nyongeza pensheni nalo linatarajiwa kutolewa ufafanuzi wa Wizara.
 
Serikali katika mwaka ujao wa fedha inapendekeza kiwango cha pensheni kupanda kutoka Sh 50,000 za sasa hadi Sh 85,000. Hata hivyo, wabunge wengi walitaka kiwango hicho kiongezeke hadi kufikia Sh 100,000 au zaidi huku wachache wakisema hizo zilizopendekezwa zinatosha.
 
Wizara hiyo ya Fedha pia itajaribu kujibu hoja kwamba bado kuna vyanzo vya mapato vingi kama uvuvi kwenye bahari kuu ambako tumeshindwa kwenda na kwamba kwenye migodi na utalii tungeweza kupata mapato mengi zaidi kuliko ilivyo sasa.
 
Wizara hiyo pia itajaribu kueleza namna itakavyodhibiti matumizi katika mwaka ujao wa fedha kwani baadhi ya wabunge walilalamikia kukosekana kwa nidhamu ya pesa kwenye taasisi nyingi za umma huku hatua za kuwawajibisha watuhumiwa zikiwa legelege.
 
Mbali na mikakati iliyopo katika kuimarisha Shilingi, serikali itatakiwa pia kujibu namna takavyoshughulikia madeni yake kama vile makandarasi, mifuko ya hifadhi ya jamii hadi wakulima wanaoidai serikali takribani Sh bilioni 22.
 
Waziri Nagu naye atatakiwa kujibu hoja kwamba ingawa uchumi unaonekana kukua kwa asilimia 7 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kati nchi 20 duniani zenye mwelekeo mzuri wa uchumi, hali hiyo haijitafsiri vyema katika mifuko ya wananchi.
 
Wizara ya Viwanda nayo, kati ya hoja kadhaa zilizoelekezwa huko, italazimika kueleza ni jinsi gani imejizatiti katika kuimarisha viwanda nchini na kuhamasisha wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zenye uhitaji mkubwa nchini kama pikipiki na bajaji na hivyo kukuza uchumi na kutengeneza ajira zaidi.
 
Baadhi ya wabunge walikuwa na hoja kwamba ni wakati sasa wa kuimarisha na kujenga viwanda nchini, ili tusiendelee kuwa nchi ya kuagiza kila kitu hadi madodoki, hali ambayo inatufanya tuhitaji sana matumizi ya dola na hivyo kuyumbisha thamani ya Shilingi yetu.
 
Wizara ya Kilimo nayo itatakiwa kujibu hoja zilizoelekezwa kwake, hususani namna itakavyojipanga kuhakikisha Tanzania inakuza kilimo chake ikiwa ni pamoja na kuuza mchele katika nchi jirani ikiwemo Kenya ambayo inapeleka pesa zake za kigeni Pakistan ili kupata zaidi ya kilo laki mbili za mchele kila mwaka.
 
Wakati karibu kila wizara iliguswa na mjadala, Ofisi ya Waziri Mkuu pia itatakiwa kujibu namna itakavyosimamia ulipaji wa fidia kwa halmashauri zilizopata ‘maafa’ kama ile ya Masasi iliyochomwa moto na wahuni pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha katika halmashauri mbalimbali nchini utakaokuwa unakwenda kwa wakati.
 
Wakati akiahirisha Bunge Ijumaa iliyopita, Sipika Anne Makinda alivitaka vyama vyote vya siasa kuhakikisha wabunge wao wanakuwepo leo ili kusikia majibu ya serikali.
 
 Wiki iliyopita wakati wa majadiliano ya Bajeti ya Serikali na Hali ya Uchumi kulikuwa na mahudhurio yasiyoridhisha ya wabunge na mawaziri.

No comments: