MSUVA ANG`ARA TUZO ZA VPL 2014-15 - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

MSUVA ANG`ARA TUZO ZA VPL 2014-15

Mshambuliaji wa Yanga SC, Simon Msuva ameng’ara katika usiku wa tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutwaa kiatu na mpira wa dhahabu.
Katika hafla ya utoaji tuzo za washindi wa Ligi Kuu msimu uliomalizika Mei mwaka huu, iliyofanyika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio, Dar es Salaam, Msuva amebeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu akiwashinda beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC na Mrisho Ngassa waliyekuwa naye Yanga SC kabla ya kutimkia Afrika Kusini.
Kwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu, amepata jumla ya Sh. Milioni 11.4, yaani Sh. Milioni 5.7 kwa kila tuzo aliyotwaa usiku wa leo.  Msuva ambaye yupo na timu ya taifa, Taifa Stars nchini Ethiopia, aliwakilishwa na baba yake Happygod Msuva na mama yake Suzan Msuva.
Baba wa Mzee Happygod Msuva, baba wa mshambuliaji wa Yanga SC, Simon Msuva (katikati) akiinua tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu kwa niaba ya mwanawe. Kulia ni Mama Msuva, Susan na kushoto mgeni Rasmi, Waziri Nkamia
Kipa Shaaban Kado wa Coastal Union ameshinda kipa bora wa msimu na kuwabwaga wenzake Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar kutwaa tuzo hiyo ya kipa bora na kujinyakulia Sh. Milioni 5.7.
Kipa wa zamani wa Yanga SC, Mbwana Makatta amewashinda Mserbia Goran Kopunovic aliyekuwa Simba SC na Mholanzi Hans Van Der Pluijm wa Yanga SC katika tuzo ya kocha bora, baada ya kuinusuru Prisons kushuka daraja na kuzawadiwa Sh. Milioni 8.6.
Israel Nkongo amewashinda Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu katika tuzo ya Mwamuzi Bora na kupata Sh. Milioni 8.6, wakati Mtibwa Sugar imezipiga kumbo  Mgambo JKT na Simba SC katika tuzo ya timu yenye Nidhamu na kuzawadiwa Sh. Milioni 17.2.
Katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alikabidhi hundi ya Sh. Milioni 80.4 kwa kuwa mabingwa, Azam FC Sh. Milioni 40.2 kwa kuwa wa pili, Simba SC Milioni 28.7 kwa kuwa wa tatu na Mbeya City Milioni 22.9 kwa kuwa nne.

Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kevin Twisa aliwapongeza washindi wote na akasema wataendelea kudhamini ligi hiyo waliyoanza kuidhamini mwaka 2002.

No comments: