CHILE YAANZA KWA SHANGWE COPA AMERICA - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

CHILE YAANZA KWA SHANGWE COPA AMERICA

Fainali za mataifa ya kusini mwa Amerika kusini (Copa America) zimeanza rasmi huko nchini Chile usiku wa kuamkia hii leo kwa kushuhudia mpambano wa ufunguzi kati ya wenyeji dhidi ya Ecuador.

Mpambano huo uliounguruma kwenye dimba la Nacional, ulimalizika kwa shangwe upande wa wenyeji, timu ya taifa ya Chile kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri yaliyofungwa na Arturo Vidal kwa njia ya penati pamoja na Eduardo Vargas katika dakika ya 67 na 84.

Pamoja na ushindi huo kwa wenyeji, mambo hayakuwa rahisi kwao, kufuatia kikosi cha Ecuador kuonyesha upinzani wa kweli huku safu ya ulinzi ya timu ya taifa ya Chile ikionekana kusumbuliwa na mshambuliaji wa klabu ya West Ham Utd, Enner Valencia.

Valencia mara kadhaa alionyesha dhamira ya kutaka kuisaidia Ecuador kupata bao kabla ya wenyeji Chile kujipatia goli la kuongoza, baada ya mpira wa kichwa alioupiga kugonga mwamba wa juu katika lango la La Roja.

Michuano hiyo itaendelea tena usiku wa kuamkia kesho kwa mchezo wa mwingine wa kundi la kwanza ambapo timu ya taifa ya Mexico itapambana na kikosi cha Bolivia kwenye uwanja wa Sausalito, uliopo mjini Viña del Mar.

Katika michuano hiyo ya Copa Amerika kundi la pili lina timu za Argentina, Paraguay, Jamaica pamoja na mabingwa watetezi Uruguay.


Kundi la tatu lina timu za Brazil, Colombia, Peru pamoja na Venezuela.

No comments: