JESHI
la Magereza nchini limeshauriwa kuhakikisha wanaruhusu wafungwa
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa
kielektroniki (BVR), unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hatua hiyo ni kuwawezesha kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi katika uchaguzi ujao.
Rai
hiyo ilitolewa jana na Mratibu wa marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, Noel Nnko wakati walipotembelea Gereza la Wilaya ya Same
na kutoa misaada mbalimbali kwa wafungwa ikiwemo utoaji wa elimu ya
kujiandikisha.
Nnko
alisema licha ya kutolewa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa
kujiandikisha katika daftari la wapiga kura makundi mbalimbali katika
jamii yamekuwa yakisahaulika ikiwemo wafungwa waliopo magerezani katika
maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
kutokana na hali hiyo ni vema viongozi wa Jeshi la Magereza nchi
wakatupia macho suala hilo kwa kuhakikisha wafungwa wanaoruhusiwa
kujiandikisha katika daftari hilo wanapata haki hiyo kwa mujibu wa
sheria.
“Tumepitia
sheria tumejiridhisha kuwa wafungwa wasioruhusiwa kujiandikisha katika
daftari la wapiga kura na kupiga kura ni wafungwa waliohukumiwa vifungo
vya maisha na kifo.
“Hivyo
natoa rai yangu kwa viongozi wa magereza kutenda haki kwa wafungwa
wengine kwani kundi hili limekuwa halipewi kipaumbele katika masuala
mbalimbali ya kijamii,” alisema Nnko.
Katika
hatua nyingine, Nnko aliwataka wafungwa hao kuacha tabia ya kushabikia
viongozi wa kisiasa bali kujiandikisha katika daftari hilo hatua ambayo
itawawezesha kupata viongozi bora kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Pamoja
na kwamba kila mtu ana haki ya kumshabikia mgombea yeyote mnawajibu wa
kuhakikisha mnaacha kuonyesha hisia zenu ili mchague kiongozi ambaye
anaweza kutatua changamoto zinazokabili taifa kwa sasa,” alisema Nnko
Nao
baadhi ya wafungwa katika gereza hilo, wameitaka NEC kusimamia zoezi la
uchaguzi mkuu kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria jambo ambalo
litasaidia kuliweka taifa katika hali ya utulivu na amani.
Walisema
hali ya utulivu na amani katika kipindi cha uchaguzi ipo mikononi mwa
tume hiyo hivyo ni vema ikatenda haki kwa wagombea hali ambayo itaepusha
vurugu na mapigano ambayo yanaweza kutokea kutokana na upungufu ambao
unaweza kujitokeza katika zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment