Akina Mama Waandamana Kudai miili ya Waliouawa na Askari Kwa Kupigwa Risasi Mkoani Simiyu - LEKULE

Breaking

16 Jun 2015

Akina Mama Waandamana Kudai miili ya Waliouawa na Askari Kwa Kupigwa Risasi Mkoani Simiyu

KINAMAMA kutoka Kata ya Bukundi Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, wameandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Erasto Sima, kushinikiza wapewe miili ya vijana wao wawili waliouawa na askari Mei 29, mwaka huu.
 
Vijana hao Gineu Gidahasi na Gitienga Gidahasi ambao ni ndugu wa familia moja wanadaiwa kupigwa risasi na askari wa Kampuni ya ulinzi ya Mwiba Holding kwa madai ya kuingiza mifugo eneo pori la makao ambalo kampuni hiyo imewekeza.
 
Kinamama hao walifika katika ofisi ya Mkuu huyo wa wilaya saa mbili juzi asubuhi  ambapo walilalamikia kitendo cha vijana wao kuuawa na kisha miili yao kutoonekana na kumwomba Sima kuagiza kupatiwa miili hiyo ili waweze kuifanyia mazishi na iwapo itashindikana watakwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kuomba msaada huo.

“Tumechoka na manyanyaso kutoka kwa mwekezaji huyu, kilichotuleta hapa tunahitaji tupatiwe miili ya vijana wetu tukaifanyie mazishi kwa heshima zote za kabila letu na iwapo utashindwa kufanya hivyo basi tutakwenda Ikulu tumuombe Rais Kikwete atusaidie,” alisema Udamulela Gitasori  mkazi wa kijiji cha Lukale.

Walisema hadi sasa zaidi ya vijana sita wameuawa tangu mwaka 2013 kwa madai ya kuingiza mifugo katika eneo la pori hilo ambalo linapakana na vijiji vya Mwabagimu, Lukale na Bukundi na hivyo wamekuwa wakiishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema), aliitupia lawama serikali kwa kushindwa kulipatia ufumbuzi suala la wafugaji kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa mwekezaji huyo licha ya kupatiwa taarifa na hivyo alimwomba Sima kusitisha shughuli zinazofanywa na Mwiba hadi hapo miili hiyo itakapopatikana.


Akijibu malalamiko hayo kwa kifupi Sima alisema serikali wilayani humo imeshaanza kulishughulikia suala hilo na tayari wote waliohusika na mauaji hayo wameshakamatwa.

No comments: