LEMA,WENZAKE RUMANDE KWA SAA NNE - LEKULE

Breaking

22 Jun 2015

LEMA,WENZAKE RUMANDE KWA SAA NNE

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na watu wengine 24 juzi walijikuta wakiwekwa mikononi mwa polisi kwa saa nne kutokana na purukushani za uandikishaji wa wapigakura katika mfumo wa BVR.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni kwenye kituo cha uandikishaji kituo cha Osunyai, Kata ya Sombetini ambako watu hao akiwamo mbunge walitiwa mbaroni.
Diwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga alisema mbunge huyo na watu wengine walikamatwa huku wengine 13 wakijeruhiwa katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema juzi kuwa tukio hilo alikuwa amelisikia juujuu lakini hakuwa amepata taarifa zaidi.
Mmoja wa washuhuda wa tukio hilo, Amiri Ally alisema juzi saa 12.20 jioni Lema alifika katika kituo hicho na kuuliza kinachoendelea na kuhamasisha waandikishaji kufanya haraka katika kuandikisha lakini walitokea vijana kadhaa waliodhaniwa ni wanachama wa CCM na kuanza kumzuia mbunge huyo asiingie ndani.
“Kila jioni Lema huwa anazungukia vituo kuangalia maendeleo lakini hakuna jambo linalotokea ila leo (juzi) kuna vijana ambao huwa tunawaona kwenye misafara ya CCM kama walinzi, walianza kumzuia Lema asiingie ndani, walianza kusukumana na wananchi nao waliingilia kati, ndio vurugu zikaanza,” alisema.
“Vurugu zilipopamba moto polisi walikuja na kuwakamata baadhi ya watu na kuondoka nao akiwamo Lema na watu wengine wakaanza kukimbia ovyo,” alisema Amiri.
Mmoja wa watu waliojeruhiwa, Abduli Adam alisema baada ya kuona mbunge anasukumwa hovyo na vijana walioonekana kama ni kutoka kwa walinzi wa CCM aliingilia kati kutaka kumsaidia lakini alichomwa kisu cha kichwa na kuvuja damu nyingi.
“Mimi nilikuwa kwenye foleni nikashangaa kelele upande wa pili kuangalia nikamuona Mbunge Lema katikati, hivyo nikajitosa kumsaidia nikachomwa kisu cha kichwa sijui aliyenichoma na sasa niko njiani naelekea hospitali ya Mkoa Mount Meru kutibiwa,” alisema.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na mwanasheria wa Chadema, mwenyekiti wa Mtaa wa Osunyai, viongozi mbalimbali wa chama na wananchi waliokuwa wanajiandikisha kituoni hapo.
Kukamatwa kwa watu hao kulisababisha shughuli ya uandikishaji kusitishwa kutokana na vurugu kuzuka kwenye kituo hicho saa 12 jioni badala ya saa 2:00 usiku kama ilivyopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumzia tukio hilo, Lema alisema, “Nimeshindwa kuelewa kukamatwa kwangu baada ya kutoa taarifa polisi, inawezekana vipi mlalamikaji akakamatwa na wahalifu wakawa huru.”

No comments: