Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameikosoa Serikali ya chama chake kwamba imekuwa siyo sikivu kwa matatizo ya wananchi na kuwa wabunge wa chama hicho wanapitisha sheria ambazo zinakuwa mzigo kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameikosoa Serikali ya chama chake kwamba imekuwa siyo sikivu kwa matatizo ya wananchi na kuwa wabunge wa chama hicho wanapitisha sheria ambazo zinakuwa mzigo kwa wananchi.
Akihutubia
katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake, jijini Mwanza jana, Kinana
alisema atafanya kikao cha kwanza na wabunge wa CCM baada ya uchaguzi
ili kuwaeleza majukumu yao ya msingi ikiwamo kuiwajibisha Serikali.
Alisema
wabunge wa CCM wamekuwa wakiunga mkono kila jambo linaloletwa bungeni
bila kutathmini matokeo ya sheria hizo kwa wananchi wanaowawakilisha.
Alisema lazima ifike wakati wabunge wa CCM wabadilike na kuwatumikia wananchi wao.
“Nitakutana
na wabunge wa CCM na kuwaambia kwamba sheria walizozipitisha
haziwasaidii wananchi… lazima chama kiwe na nguvu ya kuielekeza au
kuiwajibisha Serikali yake,” alisema Kinana huku akishangiliwa na
wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Katibu Mkuu huyo
alisema kuna haja ya kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wa chama na
mojawapo ni kuchagua mtu mwingine wa kuongoza wabunge wa CCM bungeni
badala ya Waziri Mkuu kama ilivyo sasa.
Alisema Waziri
Mkuu ataachwa atekeleze jukumu lake la kuiongoza Serikali bungeni,
lakini kuwe pia na kiongozi wa wabunge wa CCM bungeni. Alisema mfumo huo
utakipa chama nguvu zaidi ya kuisimamia Serikali yake.
“Wamekaa
wabunge tena na kupitisha sheria ya kila gari kuwa na kizimamoto, nani
alisema gari langu lina mpango wa kuungua?” alihoji kiongozi huku na
kusema sheria nyingine zinatakiwa kufutwa kwa sababu hazimsaidii
mwananchi.
Aliishangaa Serikali ya CCM kwa kushindwa
kufuta baadhi ya sheria ambazo zimebainika kuleta usumbufu kwa wananchi
na kusisitiza kuwa lazima ifike wakati Serikali ifanye tathmini ya
sheria zake na kuzifuta ambazo hazifai kwa sasa.
“Nimekuwa
waziri na kiongozi serikalini kwa muda mrefu, lakini sijawahi kuona
Serikali ikifuta sheria. Wamekuwa wakiongeza sheria mpya kila siku. Hivi
karibuni Serikali imepeleka miswada mingine 11 na yote imepitishwa. Kwa
namna hiyo tunambebesha mwananchi mzigo mkubwa,” alisema.
Kinana
aliitaka Serikali kuwashirikisha wananchi wakati wa kutunga sheria ili
kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Kuhusu ahadi za Rais
Kinana
alisema Serikali imefanya mambo mengi katika kuliletea Taifa maendeleo
kwa kutekeleza kikamilifu Ilani ya CCM ya mwaka 2010 na ahadi nyingine
zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za urais.
Alisema
wakati Serikali ikiingia madarakani mwaka 2005, kulikuwa na wanafunzi
wa elimu ya juu 48,000 tu, lakini sasa wanafikia 200,000. Aliongeza kuwa
zaidi ya vijiji 1,000 vimeunganishwa na umeme.
“Katika
kipindi cha miezi 26 ambayo tulikuwa tunatekeleza maazimio ya mkutano
mkuu wa mwaka 2012, nimejifunza mambo mengi. Nimeyajua matatizo ya
wananchi kwa karibu zaidi, lazima Serikali iwe sikivu,” alisema Kinana.
Akimkaribisha
Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwataka
Watanzania wasimame imara kukataa senti tanotano kutoka kwa wanaotaka
kununua uongozi ambao baadaye wanataka kurudisha fedha zao.
“Ndiyo
maana tunakumbana na ‘skendo’ kibao, kesho Escrow, keshokutwa Richmond,
vyote hivi dawa yake moja, lazima tuzuie wanaotaka kununua uongozi… na
kama hiki ndicho wanachokitaka, safari hii tutazuia wanaotaka kununua
uongozi.
“Hatuwezi kuzunguka nchi nzima kusafisha chama
halafu, wachache wanakaa chini wanasema nitanunua hawa, halafu sita
nitakuachia… watashika adabu mwaka huu na hii itakuwa fundisho.
“Niko
tayari kuliongoza jeshi la vijana kukataa biashara ya kununua uongozi
na matumizi mabaya ya fedha kwenye uchaguzi… haya ndiyo yanayoharibu
maadili ya nchi hii kwamba mtu anaamua yake na mwaka huu Mungu
atawalaani,” alisema Nape.
Nape aliwatahadharisha
wananchi kuepuka siasa za ushabiki kwani wakati wao (wananchi)
wakiathirika, watu wachache ndiyo wanaonufaika. Alisema CCM imejipanga
kuja kivingine katika jitihada za kuwatumikia wananchi.
“Chama
cha Mapinduzi hakiuzi uongozi. Natoa wito kwa wale wote wanaofikiri
kuwa wanaweza kufanya hivyo watambue mapema kwamba haiwezekani,”
alisema.
Akimpongeza Kinana kwa juhudi zake za
kukiimarisha chama kwa kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi, Nape
alisema ziara za katibu mkuu huyo zimetumia miezi 26 na siku 18 katika
mikoa 31 nchini.
alisema katika ziara hizo, ametembea
umbali wa kilomita 193,574 huku akizindua miradi 2,671 na kuingiza
wanachama wapya 208,432 na kati yao, 38,934 walitoka Chadema.
Katika
mkutano huo, Nape alimtambulisha mwimbaji mpya ambaye atarithi mikoba
ya marehemu John Komba kuongoza bendi ya TOT katika uhamasishaji wa
chama.
Alimtaja mrithi huyo kuwa ni Twalib Neka na kusema kuwa ameshakamilisha albamu yake ya kwanza akiwa na bendi hiyo.
No comments:
Post a Comment