Dar es Salaam.
Ndivyo alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Ndivyo alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa
alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa Dar es Salaam kuendelea na
kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani
ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza kuwa yeye ndiye anayeweza kuleta
mabadiliko hayo.
Mbunge huyo wa Monduli ametoa kauli
hizo kabla ya vikao vya juu vya kufanya uamuzi wa mgombea urais wa CCM
vitakavyoongozwa na Rais Kikwete. Vikao hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari
makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho
kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi mbalimbali, lakini Lowassa,
ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi kuliko makada wengine, ndiye
ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete kwenye hali ngumu.
Tangu
alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha kwanza na wahariri Mei 25
mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli kadhaa katika mikoa
mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza nia ya kugombea
urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu
swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo jina lake litakatwa kwenye
mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza jinsi alivyokitumikia chama
na imani yake.
“Sina mpango wa kuhama chama changu,
sina Plan B. Mimi ni Plan A tu. Tangu nimalize chuo kikuu mwaka 1977,
nimekuwa mwana-CCM. Sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo
nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano Arusha. Maisha yangu yote ni CCM,” alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia
maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 30 wakati
akitiania, Lowassa alielezea tukio la kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya
CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa
habari akiwa pamoja na Kikwete, ambaye pia alichukua fomu hizo.
“Wakati
ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na
baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa
kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa
kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye
hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,” alisema Lowassa na kuongeza
kuwa wakati ule alimuunga mkono Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete
ataniunga mkono.”
Mwaka huo, Kikwete alishindwa na
Benjamin Mkapa ambaye baadaye akawa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu.
Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua fomu na badala yake alimuunga mkono
Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo wa Monduli kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu
wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine kauli hiyo ya
Lowassa kutaka amuunge mkono ndiyo iliyosababisha Rais Kikwete kutupiwa
swali na mwanadiplomasia wa Marekani Juni 9 wakati akizungumza na
Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi katika hoteli ya Chawnie Plaza.
Rais Kikwete alijibu kuwa hana mtu wake na kwamba wote ni wagombea wake,
na kama ni suala la kuchagua, ana kura moja tu kama wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba
wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Huu
ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na
mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema Lowassa kwenye Uwanja wa
Samora mjini Iringa.
Pia aliwaambia wahariri mjini
Dodoma kuwa hawezi kuondoka CCM na kama kuna watu wanadhani hivyo,
waondoke wao. Alikuwa akijibu swali kama atakuwa tayari kuondoka CCM
iwapo ataenguliwa kwenye mchujo wa wagombea urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni
22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema hatarajii
jina lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua mwanasiasa
atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa
mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi kufanya
kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na hakuna mgombea atakayeweza
kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo anayetaka kukata
jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni kosa la kukatwa
jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi jina litarudi
tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa kifupi maswali
ya wanahabari na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi
dhidi yake amtaje jina.
“Kama hawakunitaja
hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme na anitaje. Nachoka na siasa za
tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tu zijengwe hoja.
CCM ikijipanga itashinda
Juni
25, akiwa mjini Babati kutafuta wadhamini, Lowassa alisema iwapo CCM
itajipanga vizuri, ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema
katika uchaguzi.
“Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha magomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu.”
Kwa
kujipanga, Lowassa alikuwa akimaanisha kumteua yeye kugombea urais kwa
tiketi ya CCM, akisema kufanya hivyo kutamaliza uchaguzi mapema.
Alichokisema Dar
Akiwa
Dar es Salaam juzi kusaka wadhamini alirejea kauli ya Mwalimu Nyerere
ya mwaka 1995 kwamba mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM, yatatafutwa
nje ya chama hicho.
Kutokana na kauli hizo ni wazi
kuwa rais Kikwete atakuwa katika mtihani mzito wakati atakapokuwa
akiendesha vikao vya chama hicho vya kupata mgombea urais.
Kwa
mujibu wa ratiba za CCM, kikao kitakachoanza kitakuwa na Usalama na
Maadili kitakachofanyika Julai 8 na kufuatiwa na Kamati Kuu Julai 9
ambayo itawachuja wagombea hao 42 na kubaki watano ambao majina yao
yatawasilishwa Halmashauri Kuu (NEC) Julai 10 kuchuja wagombea hao na
kubaki watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata mmoja. Mkutano
mkuu utafanyika Julai 11 na 12.
Vikao vyote isipokuwa cha Usalama na Maadili vitaongozwa na Rais Kikwete.
Jambo
jingine linaloonekana kukitesa chama hicho katika kupitisha mgombea ni
idadi kubwa ya wana-CCM wanaojitokeza kumdhamini waziri mkuu huyo wa
zamani.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho kila
mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama 30 katika mikoa 15
nchini ili kufikisha idadi ya wadhamini 450, lakini Lowassa amekuwa
akipata wanachama hadi 50,000 wanaotaka kumdhamini katika baadhi ya
mikoa.
Makada, wasomi wazungumzia kauli
Pius
Msekwa alisema chama kikongwe kama CCM hakiwezi kutishika kwa kauli
kama hizo ambazo zinaweza kuwa na tafsiri tofauti kwa wananchi wa
kawaida ambao hawafahamu taratibu za chama wanaoweza kuamini kuna watu
wanaonewa.
Alisema kwa taratibu za chama, mgombea
anatakiwa kueleza sera zake atakachowafanyia wananchi, lakini akiwa
anatoa kauli za vitisho anakuwa kero kwa wanaomsikiliza kwani
haziwasaidii.
“Sidhani kama ni kauli nzuri,
kinachotakiwa wagombea wanadi sera zao na wasubiri kupitishwa na kamati
itakayokaa kwa ajili hiyo badala ya kutamka kauli zisizokuwa na tija
wala faida kwa mwananchi wa kawaida, ”alisema Msekwa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tilya alisema
ameshangazwa na tabia hiyo ya wagombea wa CCM iliyoibuka kabla ya
taratibu za uchaguzi kutangazwa kwani huko nyuma haikuwapo.
Alisema
anachofahamu CCM ina taratibu zake za kupata wagombea kwa kuwachuja,
hivyo kauli hizo zinaonyesha kuingilia mamlaka hizo na wanaozisimamia.
Alisema
ameshangazwa na kinachojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea
wa CCM badala ya kutangaza nia na kuomba wadhamini wao wanafanya kampeni
kabisa utafikiri wameshapitishwa.
“Hii ni hatari kwa
siasa, watu kufanya mambo kwa kutokuzingatia taratibu siyo jambo jema,
nahisi kuna kitu hakipo sawa huko, wanapaswa wajichunguze na kuacha
wahusika wafanye kazi yao badala ya wao kuwa majaji,” alisema Dk Tily.
Mhadhiri
wa UDSM, Dk Benson Bana alisema anayachukulia hayo kama majigambo ya
wanachama kutafuta nguvu na kujiamini na kwamba haoni kama kuna shida,
kwa sababu mwisho wa siku watajulikana nani anabaki na nani anaondoka
katika kinyang’anyiro hicho.
“Ninachoomba kifanyike
hapa ni kamati kufanya kazi yake bila kupindapinda wala kumuogopa mtu,
kwani inaonekana wazi kuna ambao wanajinadi wakiwa na lengo la kutafuta
nafasi huko mbele ya safari ili wasiachwe na atakayeshinda, kutengeneza
historia katika maisha yao, pia wapo wenye nia ya kweli,” alisema Dk
Bana.
No comments:
Post a Comment