Dodoma/Dar.
Muswada wa Haki ya Kupata Habari uliokuwa usomwe, kwa mara ya pili Jumamosi wiki hii, uko kwenye hatihati baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kukubali uondolewe na kurudishwa kwa wadau kwa ajili ya kuujadili kabla ya kurudishwa tena bungeni na kusomwa.
Muswada wa Haki ya Kupata Habari uliokuwa usomwe, kwa mara ya pili Jumamosi wiki hii, uko kwenye hatihati baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kukubali uondolewe na kurudishwa kwa wadau kwa ajili ya kuujadili kabla ya kurudishwa tena bungeni na kusomwa.
Katibu Mtendaji
wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema jana kuwa
baada ya kikao na Kamati ya Bunge, wamekubaliana kuwa muswada huo
uliokuwa usomwe kwa mara ya pili unatakiwa kupata baraka za wadau.
“Kamati
ya Bunge ilituita, lakini tuliwaambia yetu. Muswada ni mbovu,
haujashirikisha maoni ya wadau na mambo mengi hayaendani na lengo la
muswada,” alisema Mukajanga.
“Tuliwaambia muswada
unakuja kwa mara ya pili, lakini ni bomu, na tumeiomba Kamati ya Bunge
kumwambia Spika kuwa, kwa sasa, hakuna muda wa kuujadili, tupate muda wa
kuujadili zaidi, ufanyiwe kazi kikamilifu,” alisisitiza.
Hata
hivyo, Mukajanga alisema kuwa Kamati itamshauri Spika kuwa kuna haja ya
kuujadili pamoja na kutoa muda zaidi wa kuufanyia kazi na hakuna sababu
ya kuukimbiza kupitishwa.
Kwa upande wake Deus Kibamba
alisema muswada huo utabana uhuru wa upatikanaji wa habari na kwamba
kuruhusu kupitishwa kwa muswada huo, kutaviweka vyombo vya habari na
waandishi wa habari katika wakati mgumu kutokana na sheria na kilichomo
kwenye muswada wenyewe.
Alipoulizwa Katibu wa Bunge, Dk
Thomas Kashililah kuhusu makubaliano kati ya MCT na Kamati ya Bunge ya
Jamii, alisema wanasubiri taarifa kwa kuwa lazima mwenyekiti wa kamati
amweleze Spika sababu za kuurudisha kwa wadau ndipo atoe uamuzi. “Kamati
haina mamlaka ya kurudisha muswada kwa wadau,”alisema Dk Kashililah.
Moat waisihi Serikali
Wakati
MCT pamoja na wadau wa habari wakikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Maendeleo ya Jamii, jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha
wamiliki wa vyombo vya habari ambao wameiomba Serikali kuuondoa bungeni
muswada huo hadi hapo watakaposhirikishwa, kwani ukipitishwa kuwa sheria
utawanyima wananchi haki ya kupata habari.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald
Mengi aliwaambia waandishi wa habari, baada ya kikao hicho kwamba,
muswada huo ukipitishwa kuwa sheria, utavinyima uhuru wa usambazaji
habari vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi, kitendo ambacho ni
kinyume na Katiba ya nchi. “Ibara ya 5 ya Katiba inasema kila mtu ana
haki ya kupata taarifa zilizopo chini ya mamlaka na kwamba kila mwenye
taarifa atatoa kwa umma taarifa ambayo iko chini ya mamlaka yake,”
alisema Mengi.
Alisema cha kushangaza katika ibara ya
18 ya muswada huo, kuna taarifa nyingi ambazo haziruhusiwi kutolewa
zikielezwa kuwa ni kwa maslahi ya Taifa na anayekiuka na kuziandika
habari hizo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atafungwa jela
miaka isiyopungua mitano.
“Huo ni mkanganyiko
usioeleweka na kwa maoni yangu Serikali inajaribu kuzima uhuru wa
kukusanya na kusambaza habari kwa wananchi; waandishi wengi watafungwa
kama muswada huo utapitishwa kuwa sheria,” alisema Mengi.
“Kuna haraka gani kupitisha sheria inayobana uhuru wa vyombo vya habari? Tunajiuliza Serikali inataka kuficha nini?” alihoji.
Naye,
Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz anayemikiki vyombo vya habari vya
New Habari (2006) Ltd, alisema muswada huo ni mbaya na utazaa sheria
mbaya, hivyo ameiomba Serikali kuuondoa kwani unahitaji kuangaliwa upya
na wadau ili wapate fursa ya kutoa maoni yao.
“Muswada
huu utaturudisha nyuma kama taifa, hivyo hakuna haja ya kujadili kifungu
kimoja kimoja kwani vingi vina athari kwa wadau wa wahabari na
wananchi. Tunaomba Serikali iuondoe bungeni muswada huu,”alisihi.
Mkutano
huo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication
Ltd (MCL), Francis Nanai na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa
Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
Akitoa ufafanuzi wa
muswada huo, Mwanasheria kutoka Kampuni ya Maleta and Ndumbalo Advocate,
Dk Damas Ndumbalo alisema katika muswada huo kuna mambo mengi yanatajwa
kama yenye maslahi kwa Taifa ambayo hayatatakiwa kutolewa kama taarifa.
Miongoni
mwa taarifa ambazo zina maslahi kwa Taifa ambazo hazitakiwi kuripotiwa
ni yoyote itakayoathiri uendeshaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa
(TBC). Kwa mujibu wa Dk Ndumbalo, muswada huo ukiwa sheria, utakuwa
kikwazo kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao.
Akifafanua
zaidi, Dk Ndumbalo alisema kifungu cha 11 na 12 cha muswada huo kinatoa
muda wa siku 30 mamlaka husika kukupa taarifa ulizoomba. “Siku zote
thelathini unasubiri taarifa uliyoomba, sasa hiyo itakuwa bado
habari?”alihoji.
No comments:
Post a Comment