Nape: CCM itashinda tu hata kwa goli la mkono - LEKULE

Breaking

23 Jun 2015

Nape: CCM itashinda tu hata kwa goli la mkono

Sengerema.
CCM imesema kuwa itahakikisha inarudi Ikulu hata “kwa bao la mkono” wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyehunge wilayani hapa.
Neno “bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona kitendo hicho.
“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Nape, aliye kwenye ziara ya katibu mkuu wa CCM, aliwataka wananchi wa Sengerema kusubiri ushindi wa chama hicho na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kuiweka CCM kuanzia udiwani mpaka ubunge kwa nafasi ya urais tayari kuna uhakika.
Katika mkutano huo, Nape alisema ana uhakika CCM itashinda baada ya kushuhudia mwitikio wa Watanzania tangu alipoanza kuongozana na Kinana katika ziara zake za kuizunguka nchi na kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.
Amebainisha kuwa amejifunza na kujiridhisha kuwa chama chake bado kinapendwa miongoni mwa wapigakura waliofikiwa tofauti na vyama vya upinzani.
“Tumefika maeneo mengi ambayo upinzani haujafika. Huko tuna hazina kubwa ya wanachama. Hakuna namna Ukawa wanaweza kuingia Ikulu mwaka huu,” alisisitiza.

Wapinzani waja juu

Kauli hiyo ya Nape ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani waliosema kuwa mtendaji huyo anamaanisha kuwa CCM itaiba kura.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakutaka kabisa kuzungumzia kauli ya Nape zaidi ya kusema watakutana Oktoba.
“Kwa bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana, ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba,” alisema Dk Slaa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.
Naibu mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema kauli ya Nape inamaanisha kuwa CCM itaiba kura kwani kwa kawaida bao la mkono ni bao haramu.
“Kauli hiyo inaonyesha dhahiri kuwa wataiba kura na kwa sababu katiba yetu ni mbovu matokeo yake yatatangazwa kama yalivyo… hiyo ndiyo maana ya bao la mkono,” alisema.
Kambaya alisema hata hivyo CCM isijiaminishe kwa lolote kwani hivi sasa wananchi wamebadilika kimtazamo kutokana na matatizo mengi yanayoiandama nchi kama vile afya, elimu duni na migogoro ya ardhi.
“Lakini CCM wajue kuwa kutatokea machafuko makubwa iwapo wamejipanga kuingia Ikulu kwa njia hiyo ya bao la mkono. Kauli ya Nape ni ya kidikteta na inaonyesha dhahiri kuwa wamejikita kwenye utawala wa mabavu,” alisema.
Kadhalika Kambaya alisema CUF imeshajipanga na kuhakikisha inaziba mianya yoyote ya wizi wa kura kuanzia kwenye Daftari la Wapigakura hadi katika ujanja wa kuwapigisha kura marehemu, askari na wanajeshi kama inavyodaiwa kufanyika Zanzibar.
Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Nape anatoa maneno ya kuvutia kwake kama njia ya kuwakatisha tamaa wapinzani na wanachama, hata hivyo alimuonya kuwa siasa za sasa hazitabiriki kwa njia hiyo.
“Lakini ajue kuwa mambo yanabadilika. Anaweza kushangaa mambo yakawa mengine, sasa hivi wananchi wana mwamko mkubwa na wanabadilika,” alisema.
Alisema CCM haina haja ya kujitapa kwa sasa wakati bado haijapata mgombea kwani huenda wakapata ambaye wananchi hawatamuunga mkono hata kidogo.
“Bado CCM wana makundi jambo ambalo kwao ni udhaifu. Lakini pia lazima wajue kuwa wakati wa mchujo utakapofika, wale watakaokatwa hawatafurahia kuachwa na hapo kuna sababu za wapinzani kushinda,”alisema.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wakati Nape anabishana kwenye majukwaa, NCCR inaendelea kupiga kazi.
“Badala ya kujadili hoja za msingi zenye manufaa kwa wananchi yeye anajadili CCM kupiga bao?” alihoji Mbatia.
Akijibu hoja ya Nape, Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Nancy Mrikaria alisema kauli ya kada huyo imekaa kisiasa na si kiuhalisia kwani ni kawaida kwa chama cha siasa kujiaminisha kuwa kitashika dola.
“Unajua chama chochote hata kiwe kidogo lazima kikiri kuwa kitashika dola ili mradi ilani yao inakubalika na unakubaliwa na wananchi kwa sababu chama chochote nia yake ni kuingia ikulu,” alisema.
Alisema hata vyama vidogo kama TLP hukiri ushindi kwa kusema kuwa vinataka kuingia ikulu kwa sababu chama hakiwezi kukiri mbele ya wananchi kuwa hakitashinda.

Uhujumu BVR

Katika hatua nyingine, mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, akitoa taarifa ya mkoa wake kwa Kinana alisema kuwa amegundua uhujumu unafanywa kwenye mashine za kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Wapigakura.
Alifafanua kuwa mashine hizo za kielektroniki zinazotumika kuandikisha wapigakura (BVR), hazina ubovu wowote na kwamba baada ya kuona kuwa kuna wakati zinagoma kufanya kazi, huwa inakuwa kwa zote na hivyo alichukua hatua ya kufanya uchunguzi ambao umetoa mwanga wa kinachoendelea na kwamba yupo mbioni kuchukua hatua.
“Kuna watu hujitambulisha kama wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi na kuingia ofisi za uandikishaji. Watu hawa sijui wanafanya nini lakini huzifanya mashine zote zisifanye kazi. Wanaingilia mfumo wake,” alisema Mulongo.
“Yupo ofisa mmoja ambaye alichukua likizo na akaonekana sehemu ambako baadaye mashine zilisimama kufanya kazi. Tumewapa tahadhari hiyo pia mkoa wa Mara juu ya hujuma hii ambayo bado hatujajua inafanywa kwa maslahi ya nani.”
Pamoja na changamoto hiyo, alifafanua kuwa zoezi linaendelea vizuri na anatarajia kuwa lengo la kuandikisha watu 1.4 milioni litatimia kama ilivyopangwa.
Kinana anaendelea na ziara yake ya siku 11 mkoani hapa ikiwa ni sehemu ya safari yake ya kuizunguka mikoa ya Kanda ya Ziwa inayojumuisha pia Geita na Kagera.

No comments: