Kada achukua fomu, atembea hadi stendi - LEKULE

Breaking

28 Jun 2015

Kada achukua fomu, atembea hadi stendi

Mikoani.
Antony Chalamila (66) amekuwa mgombe wa 41 kuchukua fomu ya kuomba kupitishwa na CCM kuwania urais, lakini kivutio kilikuwa ni jinsi alivyochapa mguu kutoka ofisi za chama hicho hadi stendi ya mabasi kurudi mkoani Morogoro.
Wakati kada huyo akijitokeza tano kabla ya muda wa kuchukua na kurejesha fomu kuisha, makada wengine wawili walirejesha fomu, huku Balozi Amina Salum Ali akilalamikia kukithiri kwa rushwa katika mchakato. 
Chalamila, ambaye aliongozana na msaidizi wake Benjamin Ruvunduka kwenda kuchukua fomu ofisi za makao makuu ya CCM, hakuwa na usafiri wowote wakati wa kuondoka na hivyo kutembea umbali wa takriban kilomita 1.2 kwenda kituo cha mabasi kurejea mkoani kwake Morogoro.
“Naelekea Morogoro hivi sasa wananisubiri huko,” alisema Chalamila alipokuwa akiondoka maeneo ya ofisi hizo huku akisema anashangazwa na kitendo cha waandishi wa habari kumuuliza sababu za kutotoa taarifa za tukio lake.
Chalamila alifika ofisi hizo saa 4:15 asubuhi, akiwa amevalia shati la kijani na suruali nyeusi huku akiwa ameshikilia kifimbo cheusi mithili ya kile cha Hayati Mwalimu Nyerere.
Tofauti na wengine, Chalamila alikuwa akizungumza mithili ya  Mwalimu Nyerere kwa kuzungusha midomo na kuitembeza mikono usoni akiwa na kifimbo hicho ambacho alisema alikinunua Rufiji.
Chalamila aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaomba nafasi hiyo kwa sababu yeye ni mwanachama wa CCM na miongoni mwa haki zake kikatiba ni kuchagua na kuchaguliwa.

Alisema bila ubinadamu huwezi kuongoza.
Alipoulizwa iwapo muda wa siku tano kuanzia jana utatosha wa kutafuta wadhamini, Chalamila alisema unamtosha na kwamba atatumia teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta kupata wadhamini na maeneo mengine atatembea.
“Siku zilizobaki siyo chache wala nyingi sana. Sasa hivi vijana tunajifunza IT (teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta). Nitatumia IT na vilevile nitatembea,”alisema.
“Suala la kwanini nimekuwa wa mwisho, si tatizo kwa sababu aliyetangulia anaweza kuwa wa mwisho na wa mwisho akawa wa kwanza,”alisema kada huyo huku akikicheza kifimbo chake.

Chalamila ni nani?
Chalamila alizaliwa Oktoba 15 mwaka 1949 na kusoma Shule ya Msingi Kigurunyembe na baadaye kujiendeleza kama mtahiniwa binafsi hadi kidato cha sita.
Baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu Chang’ombe jijini Dar es Salaam ambapo alitunukiwa stashada ya masomo ya uhasibu na biashara. Aliwahi kufundisha Shule ya Sekondari ya Iliboro mkoani Arusha na Sekondari ya Morogoro .
Kwa sasa Chalamila ni meneja mkuu wa Chama cha Ushirika cha Kilimo na Masoko cha Morogoro na Mvomero na ana shahada ya Elimu aliyoipata Chuo Kikuu Huria (OUT).

Wanachama wanaomba rushwa
Awali, Balozi Amina Salum Ali alirejesha fomu zake jana lakini akaungana na makada wengine kulalamikia rushwa ndani ya CCM akisema kuwa alikumbana na matatizo kutokana na wanachama kumuomba fedha ili wamdhamini. Aliwatuhumu makada wengine wanaowania urais kuwa wamekuwa wakitumia fedha nyingi katika mpango huo wakati kuna wananchi wanashindwa kupata hata mlo mmoja wa chakula kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.
“Kuna mkoa mmoja baadhi ya wadhamini walitaka kupigana kwa sababu hawakupewa fedha zao za kusaini fomu…Wakati haya yanatokea ya matumizi makubwa ya fedha, kuna watu hata milo miwili ni tabu kwao,” alisema.
Balozi Amina alisema wana-CCM wengine wamediriki hata kutamka kuwa hawatapiga kura bila kupewa fedha, jambo ambalo linaharibu utu na heshima ya mwanadamu.
“Chama ni mapenzi, chama maana yake ni  kujenga misingi, chama ni kujitolea, unataka uongozi ndani ya chama ujitolee. Sisi tumejitolea miaka chungu mzima sio sasa hivi. Kwa hiyo kweli ni (rushwa) tishio,”alisema.
Katika hatua nyingine, Jaji Augustino  Ramadhani, amesema hatakubali kuungwa mkono na mgombea wa chama chake mwenye tabia za  wizi.
Akizungumza baada ya kurudisha fomu mjini Dodoma jana, Jaji Ramadhani alisema: “Atakayenifuata kuomba kuungana na mimi nitamwangalia kwanza. Kama ana tabia za wizi, siwezi kukubali kuungwa mkono naye lakini kama anatabia njema nitakubali.”
“Sijaungana na mtu yeyote, hakuna mtu aliyenifuata wala mimi niliyemfuata. Nilipokuja kuomba kuchukua fomu nilikuja pekee yangu, nikisindikizwa na hawa wote ambao nimerudi nao leo (jana),” alisema.

Membe
Mjini Sumbawanga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe amesema kwamba katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mtu anayemnyima usingizi ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Membe alisema kuwa iwapo Pinda asingechukua fomu ya urais, angekuwa anafurahia ushindi tu.
Akizungumza kwenye ukumbi wa CCM Sabasaba, Membe alisema kuwa Waziri Pinda ni mtu mchapakazi, asiye mbinafsi, mwadilifu, mvumilivu sana mwenye hekima na busara ya hali juu, mwanasheria aliyebobea na ndiye mwalimu wake ambaye alimfundisha kazi.
“Wengine wote hawanitishi nitawagonga, nitawagonga, lakini nikifika kwa Pinda itabidi nipumue kwanza. Kwa hiyo mimi na Pinda ni pacha nikishindwa mimi nitamuunga mkono,” alisema Membe ambaye pia aliwahi kusema atamuunga mkono Profesa Mark Mwandosya.
Awali, katibu uenezi wa chama hicho mkoani hapa, Clement Bakali alisema Membe amepata wadhamini 855.

Nyalandu
Mjini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye anaomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, amesema hizi ni zama za vijana kutawala.
Akizungumza na mamia ya wakazi kwenye viwanja vya ofisi ya CCM ya Wilaya ya Arusha, Nyalandu alisema: “Nimetembea mikoa yote, nimeona shauku ya vijana na hii ni fursa yao kushiriki kulijenga Taifa hili na kwa kutumia rasilimali zilizopo,” alisema.

No comments: