JK: Nikisamehe wafungwa wanaongezeka 3,000 - LEKULE

Breaking

28 Jun 2015

JK: Nikisamehe wafungwa wanaongezeka 3,000

Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete, ameelezea kushangazwa na ongezeko la uhalifu nchini kwamba kila anapotoa msamaha kwa wafungwa 4,000 katika sherehe za Muungano, lakini inapofika siku ya Uhuru, Desemba 9, anapewa taarifa kuna ongezeko la wafungwa 3,000.

Rais Kikwete, aliyasema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya ngazi ya juu ya uongozi wa askari magereza, yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Alisema: “Kila tunapofanya sherehe mbalimbali za kitaifa, najitahidi kutafuta sababu za kuwapunguza…lakini mambo yanakuwa tofauti,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na mamia ya walioudhuria halfa hiyo.

Aliongeza kuwa “magereza 126, yaliyopo hivi sasa, hayatoshelezi kukidhi mahitaji ya kukabiliana na wimbi hilo la msongamano wa wafungwa kutokana na kasi ya uhalifu kuongezeka.

Alisema kutokana na hali ya misongamano ikitokea ikafanyika sensa ya kimataifa juu ya wafungwa magerezani, Tanzania inakuwa ya mwisho katika kukabiliana na ongezeko la wafungwa kwenye magereza.

“Hivi sasa kuna haja ya kurekebisha na kujenga magereza mapya, ili kukabiliana na changamoto hiyo sanjari na kuboreshwa huduma za wafungwa, kwani nao ni binadamu.Hivyo kuwataka askari wa jeshi hilo kufuata taratibu na kutenda haki kwa wafungwa.

“Tendeni haki kwa wafungwa hawa ili kuondoa malalamiko na maneno toka kwa ndugu zao, kwani wapo gerezani kwa ajili ya kujifunza kutokana na makosa yao,” alisema Rais Kikwete.

Pia, aliliagiza jeshi hilo kuandaa mpango mkakati kama wanavyofanya polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili kujua namna za kukabilina na changamoto zinazowakabili.

“Mpango wenu ukikamilika msipite njia ndefu… nileteeni mimi moja kwa moja nijiue namna ya kuufanyia kazi, kabla ya kuondoka madarakani,” alisema Rais Kikwete.

Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja, alisema jumla ya askari 104 walihitimu na kupewa vyeti, kati yao 10 wanatoka katika vyuo vya mafunzo Zanzibar.

Alisema mafunzo yana lengo la kuwaanda wanafunzi hao kuwa askari bora katika jeshi hili, na kozi ilitolewa kwa miezi minne , huku wakifundishwa masomo ya utawala wa magereza, haki za binadamu, afya ya jamii na utawala wa fedha.

“Mbali na kusoma darasani pia, walifanya mitihani yao kwa vitendo,” alisema Kamishna Minja.

No comments: