Bunge linapochemka ndio raha yetu- Lissu - LEKULE

Breaking

28 Jun 2015

Bunge linapochemka ndio raha yetu- Lissu

Dodoma.
Bunge la 10, ambalo linamaliza kazi yake Julai 8 kabla ya kuvunjwa siku moja baadaye, lilikuwa na mengi, lakini mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anasema kilichowafurahisha wapinzani ni wakati chombo hicho kinapochemka kutokana na hoja zao.
Mwananchi ilifanya mahojiano na Lissu, ambaye ni msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani, ambaye alizungumzia nyakati ambazo wapinzani walifurahia sana na masuala mengine.

Swali: Bunge la 10 linamaliza muda wake, unaweza ukalielezea vipi?

Lissu: Ninaweza kuliangalia kwa mitazamo tofauti, kwanza nikianza na Bunge la mwaka 1964-1965, ni Bunge la kuijenga Tanganyika kutoka katika Bunge la Kikoloni, 1965-1970, lilikuwa Bunge la Azimio la Arusha.
Bunge la 1970-1975, halikuwa na kazi kubwa, lilikuwa katika maandalizi ya kutengeneza Katiba ya Tanzania. Mwaka 1975-1980 lilikuwa Bunge lililotengeneza Katiba ya sasa pamoja na kumlea mwana aliyezaliwa, CCM. Mwaka 1980-1985 lilikuwa Bunge la mageuzi na mabadiliko ya Katiba hasa katika masuala ya haki za binadamu na Muungano.
Hapa sasa ndipo ilipoonekana kuwa Tanzania na Zanzibar ni moja kwa sababu mtikisiko wake ulimweka pembeni Rais Aboud Jumbe mwaka 1984. Mwaka 1985-1990 lilikuwa Bunge la vuguvugu la mageuzi na Bunge la 1990-1995 lilikuwa Bunge la kwanza la vyama vingi.
Mwaka 1995-2000 hakukuwa na mabadiliko sawa na Bunge la 2000-2005. Mwaka 2005-2010 lilianza kuwa Bunge la wapinzani kutokana na kuibuliwa kashfa za Epa, Buzwagi, Richmond. Hapa sasa sauti zetu ndipo ziliposikika.
Bunge la 10 naliangalia kwa mtazamo miwili, hapa sasa wapinzani ndipo walipotumia kila aina ya nguvu kujitokeza mbele kupaza sauti na naamini tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na hii sauti ndiyo itakayotupa ushindi mwaka huu. Jambo la pili, Bunge hili limeshindwa kutengeneza Katiba, Kura ya Maoni na ni Bunge lililopata joto jingi kutoka kwa wapinzani, ndani na nje ya Bunge.

Swali: Unaposema nje ya Bunge unamaanisha nini?

Lissu: Nikisema nje ya Bunge namaanisha, Watanzania walikuwa wanalifuatilia kwa karibu sana kupitia televisheni, sasa ndani ni joto na nje watu walikuwa na joto. Kila mtu alitengeneza ufahamu wa Bunge na ilitupa nguvu kuwa Watanzania sasa wana ufahamu.

Swali: Kitu gani hasa kiliwafanya sauti zenu zisikike kipindi hiki cha karibuni ikiwa ni takribani miaka 20 tangu kuanza kwa vuguvugu la mageuzi hadi mageuzi yenyewe mwaka 1992.

Lissu: Unajua tulianza kwa kusuasua sana, hatukusikika. Wakati Rais anakuja kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Novemba 18, 2010, tulisusia pale na hapo ndipo tukatengeneza ufahamu mkubwa kwa Watanzania na wakaanza kutuelewa kwa nguvu na zaidi, hoja ilikuwa kumsusia Rais.
Sasa, mjadala na hoja ulibadilika, ikawa upinzani kumsusia Rais, ilisikika sauti ya Rais na upinzani ulisikika na tulifanye vile kutengeneza ‘awareness’.

Swali: Unadhani mlifanikiwa kwa kiasi gani?

Lissu: Tulifanikiwa sana. Hapa naweza kusema sauti ya upinzani ilisikika, tulikuwa hatujui tufanye nini tusikike.

Swali: Ukiacha hiyo ya Rais, mara kwa mara mmekuwa pia mkisusia vikao na kutoka nje, hii nayo mlikuwa na dhamira kama hiyo? Na kususia unadhani kuna mafanikio au kubomoa?

Lissu: Tulikuwa na dhamira kama hiyo. Unajua unapodai haki kuna njia nyingi za kutengeneza mazingira usikike; kususia, kufanya maandamano na hiyo huleta changamoto kwa upande mwingine.
Sasa, nikupe mfano mmoja ambao naweza kusema tumefanikiwa. Tuliposusia Bunge Maalumu la Katiba, wenzetu walidhani sasa ndiyo nafasi ya kupitisha mambo yao, lakini wapi, si hii Katiba, hadi leo hakuna kinachoendelea.
Tulikuwa na nafasi yetu kama upinzani, lakini hawakutusikiliza, wakaanza kupigisha kura watu wasiokuwapo, waliokwenda Hija ili muradi yatimie, lakini mwisho wa siku hadi leo ni vurugu, nasema upinzani kwa hapa tumefanikiwa.

Swali: Kwa nini msidai haki na mkawasilisha malalamiko ama hoja zenu kwa kafuata utaratibu?

Lissu: Utapigwa bao. Wewe ukifuata njia hizo hakuna wa kukusikiliza.

Swali: Nini mmejifunza katika Bunge la 10 hasa mwenendo mzima wa Bunge?

Lissu: Unajua wapinzani hatukujengewa mazingira, tulichokiona, kama Serikali ikiwajengea mazingira wapinzani, kila waziri kivuli akawa na ofisi, tungeinyoosha Serikali. Unajua hali inavyokuwa ukimwagiwa maji ya baridi unapokuwa usingizini, sasa ndivyo ilivyo katika upinzani kwa watawala.
Pamoja na kwamba mawaziri vivuli hawana ofisi, tumefanya kazi na tunachotaka sisi, si kuivuruga Serikali, tunachotaka sisi si kuishambulia tu Serikali hata tunapowabeza, ni kwamba tunawataka kuongeza kasi ya uwajibikaji na kama kasi inawashinda watuachie.
Mmeona hapa, katika Bunge la 10 mawaziri wameng’oka katika kashfa mbalimbali, wameng’oka kwa tuhuma mbalimbali na nasema Bunge lenye nguvu, linazalisha Serikali yenye nguvu na Bunge lenye upinzani wenye nguvu, linazalisha Bunge lenye nguvu.
Mwenendo mzima ni mzuri, lakini sasa, hii kasoro iondolewe Bunge lijalo. Mawaziri vivuli wapewe ofisi wafanye kazi zao. Wakiwa na wageni wanawapeleka kantini, kweli? Hii si sawa.

Swali: Unadhani kama wapinzani, mmeichangamsha Serikali kwa kiasi gani?

Lissu: Zamani ilikuwa tofauti kidogo. Tuliwapiga sana bao, kwenye kanuni na vitu vingine, wapinzani walikuwa wakisoma sana, walikuwa wakifuatilia sana mambo na kuleta bungeni kutengeneza hoja, wenzetu walikuwa hawana hulka ya kusoma kwa baadhi yao, sasa siku hizi wanatufuatilia kweli. Wanasoma hotuba zetu tena kwa umakini sana na ‘wanachallenge’ hata sisi inatupa joto kwamba tutengeneze kitu ambacho ukikiwasilisha kweli kimewagusa.

Swali: Hoja zenu zinafanikiwa vipi kwa wingi wa wabunge wa CCM na idadi yenu?

Lissu: Hapo sasa ndiyo shida. Unajua wenzetu wako wengi na sisi hatuzidi 100 ukiacha hao akina Cheyo (John) na Mrema (Augustine), sasa inapokuja suala la kutoa uamuzi, wanatushinda kwa kuwa wao ndiyo wengi na hoja zetu zinabakia kufa kifo cha kawaida, ila moto tunawawashia wa kutosha.
Tungekuwa wengi, ingekuwa nzuri, na bunge lijalo, ninatamani liwe na uwiano sawa wa wabunge wa CCM na upinzani ili kuleta usawa kuliko hali ya sasa.

Swali: Kitu gani kibaya na kitu gani kizuri ambacho hamuwezi kukisahau katika Bunge hili?

Lissu: Hii naweza kusema ‘bad moment’ ya upinzani ni pale Spika alipoonyesha upendeleo kwa Serikali. Ilikuwa inatuumiza. Wakati mwingine hata kutoa hoja kunaminywa, kumekuwa na miongozo mingi hadi leo haijatolewa majibu, sasa hapo ndipo upinzani ilikuwa ikituchanganya.
Sasa, Spika ajaye asimamie misingi ya kanuni na sheria, awe anajua sheria na kuondoa hali hiyo. Spika ajaye pia ajipange na moto wa upinzani ambao ninadhani mwakani utakuwa mkubwa.
‘Best moment’ ya upinzani ni pale tulipowasha moto bungeni. Aisee, upinzani unapoibana Serikali kwa hoja, akaingilia Mwanasheria Mkuu, akaingilia Mnadhimu wa Serikali, Spika, huku wapinzani wakiendelea kutoa hoja mfululizo, pale huwa tunafurahi sana, kama mimi pamoja na kwamba ninashiriki kutoa hoja na najua kabisa tumewashika, ule ugomvi pale huwa naufurahia sana. Pale sasa upinzani tunaamini tumechukua pointi.

Swali: Umesema unatamani kuona Bunge lijalo liwe na uwiano sawa, mnatamani wabunge wa namna gani?

Lissu: Natamani kuona Bunge la uwiano sawa wapinzani na CCM, hili ni la msingi na wabunge hasa wa upinzani natamani kuona wenye mitazamo migumu kama ya Lissu, (John) Mnyika, (Mch Peter) Msigwa, (Halima) Mdee, Mkosamali, (David) Kafulila wabunge wa namna hii watachangamsha sana Bunge.

Swali: Wabunge gani wa CCM mnawakubali?

Lissu: Kwa pale, wabunge wa CCM ambao tunawakubali wanaposimama ni Kangi Lugola (Mwibara) ni mwenye misimamo, James Lembeli (Kahama), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Luhaga Mpina (Kisesa), Ester Bulaya (CCM). Ni wabunge wanaotaka kuona hili na hili linatokea na wanawashangaa wenzao wanatoka nje ya mstari kwa nini. Hawa tunawakubali sana.

No comments: