Hizi ndizo ndoto za waowania urais za kuiondoa nchi kwenye umaskini - LEKULE

Breaking

18 Jun 2015

Hizi ndizo ndoto za waowania urais za kuiondoa nchi kwenye umaskini

Oktoba mwaka huu Watanzania wanatarajia kumpokea rais mpya wa awamu ya tano kwa imani kuwa atakata kiu kubwa ya watu wanaopenda kuona wanawekewa mazingira mazuri ya kuondokana na umaskini.
Uzoefu wa awamu nne zilizopita, umeonyesha kuwa pamoja na vyama vinavyowasimamisha wagombea kwenye kiti cha rais kuwa na sera zao, kila aliyengia alikuwa na aina yake ya mabadiliko katika uchumi nchi.
Anayeingia madarakani katika kipindi hiki, anaweza akawa ana majukumu makubwa zaidi kuliko wengine waliopita maana Watanzania wengi wana mambo mengi ambayo wanahisi yangetatuliwa, nchi itaingia kwa haraka kwenye mafanikio na kuondokana na umaskini uliokithiri.
Hadi sasa, Watanzania zaidi ya 30 wamejitokeza kupitia CCM na CUF, wakiwa na mawazo mbalimbali ya kutatua matatizo ya Watanzania kiuchumi, iwapo watapewa ridhaa ya kukalia kiti cha rais.
Yafuatayo ni sehemu ya maelezo ya baadhi yao ambao katika maelezo yao wanawahakikishia Watanzania watazifanya ndoto zao za maendeleo kuwa kweli.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa anasema akifanikiwa kuingia Ikulu atahakikisha analiondolea taifa sifa mbaya ya kuombaomba na kulifanya kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika. “Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia,” anasema Lowassa.
Anasema anataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira ili kuwawezesha Watanzania kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anasema akipewa ridhaa hiyo, atazishirikisha sekta binafsi na umma katika kuendesha uchumi na kuziwezesha kupata mitaji mikubwa.
Anasema ana mpango wa kuvifufua viwanda na kuboresha kilimo, ili mazao yanayozalishwa yanunuliwe hapahapa nchini.
“Hatutaki tena kusafirisha malighafi nje halafu tunaletewa bidhaa zilezile zilizosindikwa. Haya mapinduzi ya viwanda ni lazima, mara tu nikiingia Ikulu Oktoba mwaka huu,” anasema.
Anasema kasi ya kufanikisha maendeleo ya viwanda itachochewa na uwepo wa gesi asilia iliyovumbuliwa mikoa ya Kusini, itakayopunguza gharama za upatikanaji wa nishati ya umeme.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba anasema atahakikisha anakukuza uchumi kwa kuwa na serikali ya watu waadilifu. Anasema atahakikisha kuwa Serikali inaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. “Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu. Nitaunda serikali ya mawaziri 18, ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake,” anasema Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina anasema anataka nafasi hiyo ya juu nchini ili akasimamia makusanyo ya kodi yatokanayo na rasilimali za taifa yanakuwa mara tatu. Anasema kuwa Tanzania ina uchumi mzuri lakini unaharibiwa na mfumo wa utawala uliopo. “Kwa sasa Taifa linakusanya Sh12 trilioni kwa mwaka, lakini mimi nitahakikisha makusanyo hayo yanaongezeka mara tatu ya hapo. Sasa makusanyo yanashindikana kutokana na kuwapo kwa mianya mingi ambayo inaruhusu wizi wa mali za umma,” anasema. Mpina anasema Tanzania siyo maskini ila umaskini uliopo unasababishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wizi, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu inayofanywa na watu binafsi na serikali.
Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala anaamini kuwa uchumi unajengwa kwa kuyapa umuhimu mambo makubwa matatu; huduma za jamii, elimu na maji. Anasema ataboresha miundombinu ya reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.
“Kazi ya kujenga uchumi na maendeleo ninaamini tunaiweza, tukiamua. Uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo; sema tuna upungufu katika kuchukua hatua za kutenda,” anasema.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira anasema Tanzania inahitaji miundombinu mingi kuanzia vinu vya kufulia umeme hadi mifumo ya usambazaji maji safi na mawasiliano ya simu. “Utawala wangu utaweka kipaumbele cha hali ya juu mpanguo huo ili kuhakikisha uwapo wa miundombinu ya uhakika na gharama nafuu kwa ajili ya wazalishaji na walaji kuendana na ukuaji wa juu unaomfaidisha kila mmoja,” anasema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anasema ili kufanikiwa kiuchumi nchi, inahitaji rasilimali watu, hivyo ameahidi kutumia nguvu katika kufanikisha jambo hilo. Anasema anataka nchi ipige hatua kutoka hapa ilipo iende mbali zaidi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo elimu na afya.

Waziri Nyalandu anaeleza atatumia nguvu kubwa kuwekeza katika rasilimali watu ambayo ni muhimu kama ilivyo kuongeza nguvu za kuwawezesha Watanzania kuwekeza katika jamii.

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba anasema iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu, atawavusha Watanzania kutoka katika hali ya uchumi mdogo uliopo hivi sasa na kuwaingia katika ulio wa kati. “Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili, nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia,” anasema Nchemba.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Entrepreneurship Limited, Boniphace Ndengo anasema Tanzania inaweza kufikia kiwango cha uchumi mzuri utakaoleta ustawi kwa wananchi wengi.

Ndengo anasema alianza biashara ya mghahawa mdogo Mtaa wa Uhuru mjini Musoma, lakini hivi sasa anaitwa mwekezaji hivyo kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo nchini, anakusudia kujenga Tanzania kuwa kituo bora cha kimataifa cha utalii na kuifanya kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Mjumbe wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ally anasema atatokomeza rushwa kwa kuwa ni adui wa uchumi.

Amina anataja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuinua uchumi, kuongeza mapato, kupambana na rushwa, huduma za jamii kuondoa matabaka ya walionacho na wasionacho na kudhibiti mapato ili yaendane na matumizi.

Balozi Ally Karume anasema Tanzania ili iweze kujenga uchumi imara, inahitaji kiongozi mwenye mbinu na uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi kwa vile ndiyo adui wakubwa wa maendeleo yake.

“Uhuru wa kujituma ni muhimu sana kwa kila mtu. Siyo mtu anataka kuuza njugu wewe unamwambia huna leseni. Unamuuliza leseni kwani anataka kuendesha gari? Mtu akitaka kuendesha gari ndiyo mdai leseni, lakini siyo kuuza njugu lazima watu wapewe uhuru wa kujituma,” anasema Balozi Karume.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Enterpreneurship, Boniphace Ndengo anasema adui mkubwa wa taifa ni rushwa na ujinga ambao ‘umezaa’ ufisadi, hivyo atakapoingia madarakani anapiga vita rushwa ili kukuza uchumi.

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal anasema kwa kuwa yeye ni mwanasayansi atatumia taaluma hiyo kuleta maendeleo nchini. “Hakuna uamuzi uliokuwa sahihi zaidi ya uamuzi wa kisayansi. Mimi siku zote uamuzi wangu unafuata utaratibu huo, ndivyo nilivyolelewa na kufunzwa na nitaendelea kuongozwa kisayansi,” anasema.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema: “Nitahakikisha uchumi wa wanyonge unainuka. Kwa hiyo katika mpango wa miaka mingine mitano, tutajikita kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tukifanya hivi umaskini utapungua kwa kiwango kikubwa na ajira zitapatikana.” Monica Mbega anasema akifanikiwa kuwa rais wa Tanzania atafanyia utafiti changamoto za awamu zilizopita na kuhakikisha anazitafutia suluhu ya kudumu.

Monica anasema pia atakabiliana na viashiria vya uvunjifu wa amani ambavyo vinatishia kuvuruga mipango ya maendeleo. Viashiria hivyo anavitaja kuwa ni uhasama, mauaji ya albino, wizi, ubaguzi wa dini na ukabila.

“Tutazungumzia upendo na umoja kuanzia ndani ya familia ndio kitovu kitakachosaidia kujenga amani. Amani itajengwa na upendo misamaha na umoja,” anasema.

Waziri wa Ofisi wa Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya anasema atakuza uchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha kisasa, kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya shughuli za kilimo.

Anasema atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa kujisimamia na kwamba Serikali itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya Watanzania waone matunda ya kukua kwa uchumi. “Serikali itakuwa injini ya kukua Kwa uchumi kwa kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye kazi kwa ufanisi na kulipa kodi nzuri kwa Serikali,’’ anasema.

Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo anasema ataondoa umaskini nchini kwa kutumia uchumi wa gesi. “Nitafuta umaskini kwa kutumia uchumi wa gesi ambao utakuwa unamilikiwa na Watanzania wenyewe. Gesi nimesomea kwa hiyo ninafahamu mambo haya vizuri. “Tena kutokana na juhudi zangu za kuhamasisha vijana wapelekwe nje kusoma masomo ya gesi, nategemea mwakani tutakuwa na wataalamu wengi zaidi watakaoweza kufanya kazi kwenye sekta hii.”

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja anasema atapambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi, ambayo ni umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili. “Maendeleo ya kweli ya nchi yetu hayawezi kuletwa na sekta ya umma peke yake, bali yataletwa kwa kushirikisha kikamilifu sekta binafsi. Ni muhimu rais wa awamu ya tano awe na weledi wa kutosha kuhusu utendaji wa sekta ya umma na binafsi,” anasema.

No comments: