KIONGOZI
wa Uamsho na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Faridi Hadi Ahmed na
wenzake 22 wanaokabiliwa na tuhuma za ugaidi wamegoma kula gerezani.
Washtakiwa
hao wamegoma kula na wamedai mahakamani kwamba hata waitwe wahaini
hawawezi kugeuza madai yao ya kutaka Zanzibar ipate mamlaka yake kamili.
Hayo
yalidaiwa jana na washtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta, wakati kesi yao ilipokuwa
inatajwa.
Upande
wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali ulidai
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo ukaomba kesi iahirishwe huku
ukisubiri kumbukumbu za mahakama kwa ajili ya kukata rufaa.
Mshtakiwa
Sheikh Farid, alidai chanzo cha kushtakiwa katika kesi hiyo ni madai
yao katika mchakato wa katiba ya kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka
sahihi.
“Sisi
wote ni viongozi wa jumuiya, baada ya yote hayo ndiyo misukosuko
ikaanza kwetu, kesi ya ugaidi ni bandia, madai yetu hatuwezi kuyageuza
hata watuite wahaini.
“Tulifanyiwa
mambo mengi ya ukatili, sisi tunadai heshima ya nchi yetu, tulitamka
wazi hatutaki Muungano tunataka Rais wetu apewe heshima yake kama Rais
wa Zanzibar,” alidai.
Alidai
hawana ajenda ya siri, walifanya mihadhara zaidi ya 200 na walitakiwa
kushtakiwa Zanzibar kwa hiyo kutengeneza mazingira hayo ni kutaka
kuwadhulumu haki zao.
Sheikh Faridi alidai Serikali iliyopo madarakani imezeeka na ni kikongwe.
Mshtakiwa huyo na wenzake 22 waliomba siku saba kesi yao isikilizwe na endapo zitaisha hatua watakayochukua itaonekana.
Alisema
hawawezi kukubali kudhulumiwa huku wakikaa kimya. Walimtaka Kamishna
wa Zanzibar ajieleze kwa nini aliamua kuwaleta Tanzania Bara kuwashtaki.
Hakimu
Rutta alisema ni haki kwa waliopo gerezani kutembelewa, waliogoma kula
waambiwe wale kwa sababu rai yake ni kutaka wafike mahakamani na
wanafuatilia kwa karibu.
Baada ya Hakimu kusema hayo kesi iliahirishwa hadi Mei 25 mwaka huu.
Mshtakiwa Salum Ally aliomba wapigwe risasi kichwani wamalizwe kwa sababu wamechoka.
Washtakiwa hao wanadaiwa kula njama kufanya ugaidi, kuwawezesha watu kufanya ugaidi na kuwahifadhi magaidi.
Uhalifu huo unadaiwa ulifanyika sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment