Chadema Wazuiwa Kuhudhuria Mikutano ya CCM - LEKULE

Breaking

12 May 2015

Chadema Wazuiwa Kuhudhuria Mikutano ya CCM

HAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, kimewapiga marufuku wanachama wake wasihudhurie mikutano ya hadhara ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Wito huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Wilaya ya Momba, Ayubu Sikagonamo, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Sogea.
 
Sikagonamo alitoa agizo hilo baada ya wanachama wa chama chake kudaiwa kupigwa na wanachama wa CCM hivi karibuni.
 
“Ili kuondokana na vurugu zinazoweza kuepukika, wanachama wetu mnatakiwa kutohudhuria mikutano inayoitishwa na CCM, hata kama wamewafuata katika maeneo mnayofanyia kazi zenu.
 
“Yeyote atakayekwenda katika mikutano ya CCM na kupigwa na wanachama wa CCM, hatutashughulika naye kwa sababu atakuwa amejitakia mwenyewe.
 
“Wananchi wote kwa muda huu tunaoelekea kwenye uchaguzi mkuu, kila mmoja awe tayari kukiunga mkono chama chake na siyo kuwashabikia wengine,” alisema Sikagonamo.
 
Pia aliwataka wafuasi wa chama hicho wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kuwa na sifa za kuwachagua wagombea wa Chadema na wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
Naye Katibu wa BAVICHA, Wilaya ya Momba, Hoseah Kibwana, alilitaka Jeshi la Polisi kutokitetea chama chochote cha siasa kwa kuwa hilo siyo jukumu lake.
 
Aliwataka wagombea wa CCM wanaotaka kugombea ubunge katika Jimbo la Mbozi Magharibi linaloongozwa na Chadema, wasiendelee kupoteza muda kwa kuwa hawatashinda.

No comments: