SERIKALI
za Tanzania na Uganda zimepiga marufuku watu kujenga nyumba katika
mipaka inayozitenganisha nchi hizo ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya
lazima.
Agizo
hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki mkoani Kagera na wakuu wa wilaya za
Misenyi kutoka Tanzania pamoja na wakuu wa Wilaya za Rakai na Isingiro
za nchini Uganda.
Wakuu
hao wa wilaya walitoa maagizo hayo baada ya kukutana kwenye mkutano wa
ujirani mwema uliofanyika eneo la Mutukula, Tanzania.
Katika
mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Fadhili Nkurlu, ambaye alikuwa
mwenyeji wa mkutano huo, alisema ajenda kuu katika mkutano wao ilikuwa
ni kujadili jinsi ya kutatua kero mbalimbali, zikiwamo mfereji
uliochimbwa katikati ya mpaka wa kimataifa katika eneo la Mutukula.
“Mfereji
huo humwaga maji machafu kutoka upande wa Uganda na kuishia katika
makazi ya Watanzania na unasababisha uharibifu wa mali na miundombinu
mbalimbali.
“Katika
suala hilo, tulikubaliana kuwa, suala hilo lirudishwe kwa wataalamu wa
ardhi wa nchi husika ili walitazame kwa makini na kutoa ushauri na
mapendekezo yatakayotatua kero hiyo.
“Wataalamu
hao tumewapa muda wa siku 30 kuanzia Mei 7 mwaka huu ili wakamilishe
jambo hili na kupeleka ripoti kwetu ili ufumbuzi upatikane.
“Wataalamu
hao watazunguka mpaka mzima kuanzia jiwe namba 27 hadi 41 ili kubaini
matatizo madogo madogo yanayosababishwa na jamii au yanayoikumba jamii
iliyoko mipakani ili tuyafanyie kazi na kuendeleza amani iliyopo,” alisema Nkurlu.
Kwa
upande wa Mkuu wa Wilaya ya Rakai, Mubiru Charles na Mkuu wa Wilaya ya
Isingiro, Muhangi Herbert, walisema kwa nyakati tofauti kwamba
wanasubiri ripoti itakayoletwa na wataalamu hao wa ardhi ili kuona
makosa yamefanyika wapi na yatafutiwe ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment