HOSPITALI
ya Taifa Muhimbili (MNH) imekumbwa na uhaba wa damu hali ambayo
imeulazimu uongozi wa hospitali hiyo kuomba msaada wa dharura kwa
Serikali na watu binafsi.
Uongozi
huo pia umewaomba Watanzania, mashirika ya umma, makampuni na watu
binafsi kujitokeza kusaidia kuchangia damu kuokoa maisha ya wagonjwa
wanaopelekwa katika hospitali hiyo.
Taarifa
iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa
Wateja, Aminiel Aligaesha, ilieleza kuwa kwa siku hospitali hiyo
huhitaji wastani wa chupa za damu 70 hadi 100 kwa siku.
Alisema
hali hiyo inachangiwa na ongezeko la mahitaji ya damu ambayo hutumika
zaidi hasa kwa wagonjwa wa dharura, kina mama wajawazito, wagonjwa
waliofanyiwa upasuaji, watoto na wagonjwa wa saratani.
“Kila
mgonjwa wa upasuaji wa moyo anahitaji kiasi cha chupa tano mpaka sita
za damu. Matumizi haya yanafanyika kabla, wakati na baada ya kufanyiwa
upasuaji,” alisema Aligaesha.
Alisema
kwa wiki hii wamelazimika kufungua kambi maalumu za Madaktari Bingwa wa
Moyo kutoka nchi mbalimbali ambao wanashirikiana na madaktari wa hapa
nchini kufanya upasuaji wa moyo, kati ya wagonjwa watano hadi sita kwa
siku.
“Wagonjwa
wa moyo pekee huitaji chupa 30 hadi 36 kwa siku. Kambi hizi zimeanza
mapema Aprili mwaka huu na tunatarajia kuwa nazo katika miezi mitatu
ijayo kama njia ya kuwafanya madaktari hawa waendelee kuja na kufanya
upasuaji wa moyo kwa ufanisi ambako damu huhitajika zaidi,” alisema Eligaesha.
Alisema
hospitali hiyo ya taifa hutegemea kupata damu kutoka vyanzo vikuu
viwili ambavyo ni ndani ya hospitali na Mpango wa Taifa wa Damu Salama
(NBTS).
“Makusanyo ya damu kutoka vyanzo vya ndani ni kati ya chupa 20 hadi 40 kwa siku huku matumizi yakiwa chupa 70 hadi 100.
“Mathalani
kuanzia Aprili 17 mwaka huu hatukuweza kupata damu hata chupa moja
kutoka Mpango wa Taifa Damu Salama hali iliyosababisha upungufu mkubwa
wa damu hospitalini hapa ikilinganishwa na mahitaji,” alisema.
No comments:
Post a Comment