Watu 15 Wauawa Kwa Mapanga Geita - LEKULE

Breaking

12 May 2015

Watu 15 Wauawa Kwa Mapanga Geita

WATU 15 wameuawa kwa kukatwa mapanga katika matukio tofauti mkoani Geita kwa imani za ushirikina.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema matukio hayo ya mauaji yametokea katika  miezi mine kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu.
 
Konyo alisema  mauaji hayo yametokana na imani potofu za ushirikina na wahusika wakubwa wa matukio hayo ni waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi.
 
“Kwa mwaka huu mpaka hivi sasa  tulikumbwa na matukio 15 ya mauji yaliyotokana na imani za ushirikina ambako katika wilaya tano kulikuwa na wastani wa watu watatu ambao waliuawa, lakini tunashukuru matukio haya tumepungua kwa sababu ya operesheni ya kuwasaka waganga,” alisema Konyo.
 
Wakati huohuo, Kamanda Konyo amethibitisha kuwa mtu mmoja, Lyoba Juma (23), mkazi wa Kijiji cha Milwa Butiama amefariki dunia kwa kugongwa na gari ya Land Cruiser mali ya Mgodi wa GGM iliyokuwa likiendeshwa na Yusuph Hashibeli.
 
Alisema tukio hilo lilitokea  ndani ya mgodi wa dhahabu wa GGM eneo la WD1 wakati  Juma  na vijana wenzake walipokwenda kupora mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu.

Kamanda alisema  walinzi waliokuwa katika doria waliwafukuza na yeye aliteleza katika kifusi na kubiringika mpaka barabarani ndipo tairi za nyuma ya  gari hiyo ilipomkanyaga  kichwani.

No comments: