Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira amesema kama chama chake, CCM, kitampa fursa
ya kuwania wadhifa wa urais, atasimama kwenye mstari wa uadilifu na
ufanisi ili kulinda heshima ya cheo hicho.
Akizungumza
na Mwananchi baada ya kupokea tani 7,492 za mbolea kutoka kwa watu wa
Japan jana Dar es Salaam, Wasira alisema pamoja na kwamba CCM bado
haijapuliza kipenga cha kuwania nafasi hiyo, lakini kikimteua basi ana
uhakika wa kuwashinda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). “Nina nguvu
kwenye chama changu...mimi ni mwadilifu, sina makundi yoyote. Nina
hakika nitakuwa rais bora,” alisema.
Wasira, ambaye ni Mbunge wa Bunda alisema wadhifa wa urais hauangalii umri, sura au fedha bali uwezo wa kuongoza na uadilifu.
Alisema
umri mkubwa siyo kigezo cha kuwa rais bora, kwani hata rais wa sasa wa
Nigeria ana miaka 72. Akifafanua, alisema kama angekuwa na afya dhaifu
au kukosa akili timamu, basi hicho kingeweza kuwa kigezo cha kuukosa
urais. “Mimi siyo mbunge dhaifu na simhofii yeyote kisiasa. Nina hakika
na usafi wangu kiakili, kimwili na uwezo wa kuongoza,” alisema.
Katika
kujiweka kwenye mstari wa kukubalika, mbunge huyo aliukosoa uchambuzi
wa mchambuzi Julius Mtatiro katika gazeti hili uliomtaja kama mmoja wa
viongozi wenye kauli za ‘kidikteta’.
Alisema,
“Inapotokea nikasema ukweli, basi nisituhumiwe kuwa ni dikteta. Penye
ukweli unatajwa ukweli, penye uongo, ukweli huwekwa bayana.
“Mtatiro anadai mimi nimewahi kutoa kauli za vitisho, hilo siyo kweli bali mimi ni msema kweli na huo ndiyo utawala bora.”
Kuhusu
jimbo lake kuwaniwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa CCM, Esther Bulaya,
Wasira alisema, “Sina hofu juu ya mbunge huyo, kwanza siyo saizi yangu.
Hata nisipogombea (Esther) hatashinda, namruhusu agombee nina uhakika
hawezi kushinda.”
No comments:
Post a Comment