Dar es Salaam. Hali ya jiji la Dar es
Salaam jana ilizidi kuwa mbaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
na kuwaweka wakazi kwenye hali ngumu zaidi baada ya kukumbwa na matukio
mengine makubwa yaliyoathiri jiji na sehemu nyingine kote nchini tangu
kuanza kwa mwaka.
Mvua hizo kubwa zinazolingana na zile
zilizonyesha miaka mitatu iliyopita na kusababisha usumbufu mkubwa,
jana zilisababisha nyumba kadhaa kuanguka, madaraja kukatika, barabara
kufungwa, ikiwapo ya Morogoro, usafiri kuwa mgumu kutokana na misururu
mirefu ya magari na Jeshi la Polisi kulazimika kutoa tamko la kushauri
wananchi kutoka mapema maofisini ili kuwahi majumbani.
Matukio
hayo yametokea siku chache baada ya kusitishwa kwa mgomo wa pili wa
madereva uliosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri karibu nchi nzima.
Madereva waliamua kufanya mgomo huo kupinga masharti mapya ya kupata
leseni yaliyotolewa na Serikali ikiwa ni mkakati uliobuniwa kukabiliana
na ajali ambazo tangu Januari mwaka huu zimeua zaidi ya watu 900.
Mwaka
2015 pia umeanza kwa mgomo wa nchi nzima wa wafanyabiashara, kuibuka
upya kwa mauaji ya albino, tishio la ugaidi lililoambatana na mauaji ya
polisi na kugundulika kwa vituo vya mafunzo ya kigaidi kwa watoto
wadogo, kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya shilingi, kuvurugika kwa
mchakato wa katiba na mvua ya mawe iliyoua watu kadhaa mkoani Shinyanga.
Kwa
muda wa siku mbili, mvua zimenyesha mfululizo na kusababisha mafuriko
kwenye sehemu kadhaa za Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha
biashara na shughuli za Serikali, likiwa na takriban watu milioni 4.4
kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Pamoja
na mvua hizo kunyesha kwa wingi jijini Dar es Salaam, athari zake
zinategemewa kugusa mikoa mingine yote kutokana na umuhimu wa jiji
kiuchumi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema jana kuwa daraja la Mwanamtoti lililopo eneo la
Mbagala Kuu limeng’olewa na mafuriko hayo.
Kamanda Kova
alisema Barabara ya Morogoro imefungwa eneo la kati ya Magomeni na Fire
kutokana na Mto Msimbazi kufurika na kusababisha maji kupita juu ya
daraja.
Alisema nyumba za watu wanaoishi Magomeni
Mikumi zimejaa maji na hivyo Jeshi la Polisi limetoa amri kwa watu wote
kuondoka eneo hilo.
Kova alisema barabara nyingine
iliyofungwa ni ya Kinyerezi ambako maji yalikuwa yakiongezeka na
kutishia kulisomba daraja linalounganisha Kinyerezi na Majumba Sita.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema daraja lililopo eneo
la Mwanamtoti eneo la Mbagala Kuu limeng’olewa na mafuriko na
kusababisha kukatika kwa mawasiliano.
“Nimewaagiza
vijana wangu watembelee sehemu mbalimbali ili kuangalia maeneo ambayo
yameathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam,”
alisema Satta.
Wakati huohuo, meya wa Manispaa ya
Temeke, Maabad Hoja alisema Barabara za Kimbiji, Mpemba Mnazi
zimekatika kutokana na mvua hizo na kuvuruga mawasiliano.
Hoja
alisema halmashauri hiyo italazimika kuchukua hatua za haraka hivyo
itaundwa kamati ili kuangalia jinsi gani ya kutatua tatizo hilo.
“Hatua
ya kwanza, tunawaagiza watendaji wa kata watuletee taarifa zilizopo
kwenye maeneo yao kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema Hoja.
Hadi
sasa tathmini halisi ya hasara iliyopatikana haijawekwa bayana, lakini
wakazi wa jijini hapa waliozungumza na gazeti hili wameeleza jinsi
walivyoathirika na mvua hizo za siku mbili pamoja na mgomo wa madereva
uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Jumatatu.
“Hata leo,
tulikuwa na kipindi lakini kutokana na mvua zinazoendelea, mhadhiri
ametutangazia kusitisha darasa baada ya wanafunzi wengi kueleza kuwa
huko waliko foleni ni ndefu tofauti na siku za kawaida,” alisema Athile
Mputa, mwanafunzi wa shahada ya pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
ambaye pia alikosa vipindi wiki hii kutokana na mgomo wa madereva.
“Hali
inaniongezea mzigo wa masomo ambayo nitalazimika kuyatafutia muda
mwingine ili kukamilisha mtalaa,” aliongeza Mputa ambaye ana anahudhuria
masomo ya jioni UDSM.
Mvua zinazoendelea zimewaathiri
wafanyakazi ambao ofisi zao zipo katikati ya mji. Hali hiyo
ilithibitishwa na Elibariki Mushi anayefanyakazi katika tawi la benki
moja lilipo katikati ya mji.
“Jana (juzi) nilitoka
ofisini saa 1:30 jioni lakini nilifika nyumbani kwangu (Tabata-Segerea)
saa 7:00 usiku. Nilikuwa nimechoka hata hivyo sikupata muda wa kulala
vya kutosha kwani niliwahi kuamka na kwenda ofisini saa 12:00 alfajiri.
Hata hivyo, nilifika saa 6:00 mchana. Hata kazi nashindwa kufanya, hasa
nikifikiria foleni ya kurudi tena nyumbani… sijui nitoke saa ngapi ili
niwahi,” alisema.
Licha ya hao, wafanyabiashara pia
wamepoteza kipato na kuyumba kiuchumi kwa muda. Wengine wamelazimika
kukopa ili kuendesha familia baada ya kutofanya mauzo yoyote kwa wiki
nzima.
Jackline Champanda, ambaye anafanya biashara ya
maji maeneo ya Mbagala, anasema kuwa hali hii ni mbaya kwake tangu aanze
biashara hiyo kwani amepoteza mapato kiasi cha kushindwa kuihudumia
familia yake.
“Sikujua kama kutakuwa na mgomo wa
madereva hivyo nilipoteza Sh20,000 nauli ya kwenda na kurudi kwa
Jumatatu pekee. Hata siku iliyofuata, asubuhi ilikuwa hivyo. Lakini
pamoja na hilo bado biashara siyo nzuri hata kidogo… watu hawanunui maji
wala juisi kama inavyokuwa siku zote,” alisema.
Jackline
anayeishi Ubungo, alifafanua kuwa hali hiyo imemkuta ikiwa ni siku
chache baada ya kununua mzigo mkubwa kwa ajili ya duka lake hivyo hali
inayoendelea kuwa janga kwake.
Wapo wanafunzi waliokosa
masomo pia kutokana na mvua zinazoendelea. Chacha Marigo, mkazi wa
Chanika, alisema kuwa watoto wake hawakwenda shule jana baada ya kukosa
usafiri.
“Niliondoka nyumbani saa 12:00 alfajiri na
niliwaacha wanangu wawili kituoni ambako basi la shule huwapitia kila
siku. Lakini nilipopiga simu shuleni baadaye ili kujua kinachoendelea
mkuu wa usafiri alinijulisha kuwa gari halikupita katika mzunguko leo
(jana). Watoto walirudi nyumbani,” alisema Marigo.
Mwalimu
wa Shule ya Sekondari Loyola, Pontain Kashangashi aliliambia Mwananchi
kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha shule imelazimika
‘kulegeza’ baadhi ya masharti ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na
masomo.
Kashangashi alisema kuwa siku mbili mfululizo
baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakifika shuleni bila ya sare za shule huku
wengine wakichelewa kufika kutokana na mvua hizo ambazo pia
zimesababisha kukosekana na kwa usafiri hasa wa kuingia katikati ya
jiji.
Alieleza kuwa ratiba ya shule inawataka wanafunzi
kufika shuleni saa 12:30 asubuhi lakini kutokana na mvua wengi wamekuwa
wakichelewa wakiwamo baadhi ya walimu. “Wanatembea kwenye mvua kwa muda
mrefu, wanakuja nguo zimeloana hasa viatu ndio vinaharibika sana.
Tumeamua hata masomo ya jioni tuyaondoe ili wanafunzi waondoke mapema,”
alisema Kashangashi.
Victoria Kishimbo, mkazi wa
Kijichi, alisema kuwa tangu mgomo wa mara ya pili wa madereva na mvua
zinazoendelea kunyesha zimemuathiri kwa kiasi kikubwa kwa kuwa amekuwa
akichelewa kwenda hospitali kumpelekea chakula dada yake aliyelazwa
katika Hospitali ya Temeke.
“Ule mgomo ulinichelewesha
kupeleka chakula kwa mgonjwa, yaani nilikaa kituoni hadi muda wa kuona
wagonjwa ukaisha. Nilipofika hospitali nilimkuta amesubiri hadi
amechoka, kibaya zaidi chakula chenyewe kilikuwa kimepoa,” alisema
Victoria.
Alisema baada ya kusikia mgomo umekwisha
alijua hali ingekuwa nzuri, lakini kinyume chake usafiri wa daladala
umekosekana kutokana na mvua zinazoendelea Dar es Salaam. “Mvua zinaanza
kunyesha tangu saa 11:00 asubuhi, ukienda kituoni hakuna usafiri magari
mengi yamekwama kwenye foleni. Sijui hali hii nayo itaisha lini,”
alisema.
Wakati wakazi hao wa jijini Dar es Salaam
wakitafakari matukio hayo makubwa yaliyotokea wiki hii, hali haijawa
nzuri nchini tangu mwaka 2015 uanze kutokana na matukio mengi kulikumba
Taifa, baadhi yakiwa yanatishia amani na usalama wa nchi.
No comments:
Post a Comment