Wahandisi, Tanroads waanza kulifanyia tathmini jiji la Dar - LEKULE

Breaking

10 May 2015

Wahandisi, Tanroads waanza kulifanyia tathmini jiji la Dar


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ameteua timu ya wahandisi kutoka Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na kujua gharama stahiki kulirudisha jiji katika hali yake.
Akizungumza jijini jana, Sadiki alisema kuwa baada ya kufanya tathmini hiyo, itatoa mwanga ni kiasi gani kinahitajika ili kurudisha miundombinu iliyoharibika katika hali yake ya kawaida.
“Siwezi nikasema leo (jana) kuwa miundombinu iliyoharibikia itafanyiwa matengenezo kwa kiasi hiki au kile, subirini. Nimeitisha wahandisi na wanaendelea na kazi,” alisema Sadiki na kuongeza kuwa;
“ Hiki kitu siyo cha kukurupuka kina taratibu na sheria zake inabidi zifuatwe, hayo yote yakishakamilika wananchi wa mkoa huu watafahamishwa lini ukarabati unaanza na kwa kiasi gani, kwani hapa hakuna siri,”.
Akizungumza na gazeti hili juzi ofisini kwake, mkuu huyo wa mkoa alisema mvua zimelivuruga jiji na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Sadiki aliyasema hayo baada ya kumalizika kikao cha kutathmini mafuriko hayo kilichohusisha wakuu wa wilaya za mkoa huo, Ilala, Kinondoni na Temeke, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa na Kitengo cha Maafa Mkoa.
Sadiki aliliambia gazeti hili kuwa, jiji haliko kwenye hali nzuri kwani barabara zaidi ya 20 zimeharibiwa, madaraja kadhaa, makaravati yamesombwa na maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika baadhi ya maeneo.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua hizo ni pamoja na Keko, Chang’ombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Africana, Msasani Bonde la Mpunga, Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko na Basihaya.
Waathirika waweka ngumu
Licha ya kuathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizoonyesha mfululizo kwa siku kadhaa, wakazi wa maeneo yaliyopatwa na adha hiyo wamesisitiza kuwa hawatahama katika makazi yao kwa sababu mafuriko yamewafuata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili walidai kuwa wameishi maeneo hayo kwa miaka mingi, wakipata huduma zote, ikiwamo maji, umeme lakini hakukuwa na adha hiyo, huku wakiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutafuta jinsi ya kuwasaidia.
Wakazi wa Magomeni Madaba ambako nyumba zilijaa maji na kuonekana paa juzi na jana, kwa nyakati tofauti walisema kuwa huu ni mwaka wa nne wanaingiliwa na maji na miaka minne iliyopita, walipewa namba kwa ajili ya kupewa viwanja lakini hadi leo hawajapewa.
Mussa Mkinga aliliambia gazeti hili kuwa amejenga eneo hilo tangu mwaka 1989, akiwa na kazi, hivi sasa ameshastaafu anapoambiwa kuhama lazima kuwe na mazingira ya kumuwezesha kufanya hivyo.
“Ninyi wenyewe mmewatafuta wataalamu wameweka wazi kuwa katika njia za maji kumejengwa majumba, wenye fedha wameziba, hakuna wa kuwauliza sisi wanyonge ndiyo tunaathirika, sina mpango wa kuhama, nilipewa namba siikumbuki ni ngapi huu mwaka wa nne sijapewa hicho kiwanja sasa nitahamia wapi, ”alisema Mkinga.

Magomeni Mkwajuni
Mkazi wa eneo la Magomeni Mkwajuni tangu miaka ya 80, Rehema Bakari alisema kuwa maji yalikuwa yanaingia lakini siyo kama yalivyoingia kipindi cha mvua hizi, kwani yamesomba kila kitu huku yakimuacha na nguo moja aliyovaa.
Alisema angekuwa na uwezo angeondoka kwani hata vitu kidogo vilivyobaki anavyovitoa vinanuka kinyesi, kutokana na eneo hilo kuzongwa na vyoo vilivyozibuliwa kipindi cha mvua hivyo vinyesi kusambaa kila kona.
Wakazi wa Magomeni Sunna wameliambia gazeti hili kuwa wao wanaomba uhai, kwani hata huko Mabwepande walikopewa viwanja wanashindwa kuviendeleza kutokana na ukata.
Zuwena Kika alisema kuwa ameachiwa na mumewe watoto watano baada ya kufariki dunia, amepewa kiwanja Mabwepande alipopata mafuriko miaka minne iliyopita, lakini hana uwezo wa kukiendeleza kiwanja hicho, alipewa mifuko ya saruji isiyokuwa na kitu kingine ambayo haikuwa msaada.
Bonde la Kigogo
Kelvin Otea mkazi wa Bonde la Kigogo alisema kuwa amejenga hana pa kwenda na hata maji yalivyojaa ndani ya nyumba yake alilala kwenye eneo ambalo lilikuwa na unafuu.
“Sina pa kwenda mama, nihamie wapi, hao wanaosema nihame wanipe mahali pa kuishi na wanitengenezee mazingira ya kuishi huko, tofauti na hapo nitakuwa muongo,” alisema Otea.
Hali halisi katika baadhi ya maeneo
Maeneo mengi tofauti na juzi, yamekauka na familia nyingi zilikuwa zikionekana kupambana na tope pamoja na kufua nguzo zilizokuwa zimetapakaa udongo.
Wahenga walisema ‘kufa kufaana’, kutokana na mafuriko hayo na maji kujaa ndani ya nyumba nyingi hivyo, baadhi ya vijana kupata ajira ya kusafisha nyumba hizo.
Vijana hao walikutwa wakisafisha masofa, magodoro, vitanda, makabati na kutoa matope yaliyorundikana ndani ya nyumba hizo baada ya maji kutoka.
“Ndiyo tunapiga kazi, tumepatana na mwenye nyumba atatulipa kidogodogo, ”alisema kijana mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa hiyo siyo kazi yake (kuzungumza na waandishi).

No comments: