Dar/Mbeya. Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakieleza
hofu ya Uchaguzi Mkuu kuahirishwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imesitisha mchakato wa kuandikisha wapigakura mkoani Mbeya uliopangwa
kufanyika kuanzia Mei 5 hadi itakapotangazwa tena.
Tayari
kazi hiyo inaendelea kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa
ambako kazi hiyo pia ilianza kwa kusuasua, na NEC ilitarajiwa kuongeza
kasi ya uandikishaji kwa kuingia mikoa ya Dodoma, Katavi na Mbeya ambako
mpango huo umesitishwa kwa muda usiojulikana.
Akizungumza
na gazeti hili jana, kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Lazaro
Samweli alisema walipewa taarifa za kusitisha uandikishaji hadi hapo
watapotaarifiwa tena licha ya Tume hiyo kupeleka vifaa vya BVR.
Mwezi
uliopita, Nec ilitangaza kwamba ingeanza kazi hiyo ya kuboresha Daftari
la Wapigakura mkoani hapa Mei 5, jambo ambalo lilisababisha uongozi wa
jiji utangaze nafasi za kazi ya kuandikisha kwa wenye ujuzi wa kompyuta.
“Kabla
ya Mei 4, ofisa kutoka Tume ya Uchaguzi alikuja akatuambia tusimamishe
mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia hadi hapo tutakapotaarifiwa,
lakini vifaa tulishavipokea, hivyo tunawasubiri wao watakavyotuelekeza
taratibu zao kwa mara nyingine tena,” alisema Dk Samweli.
Alisema
walipokea mashine 86 za BVR kutoka NEC na kwamba mashine 15 kati ya
hizo ni kwa ajili ya mafunzo ya waandikishaji na 71 zinazosalia zitakuwa
maalumu kwa kazi yenyewe ya kuandikishia.
Viongozi wa
vyama vya upinzani wamekuwa wakituhumu kuwa kusuasua huko kwa kazi ya
kuboresha Daftari la Wapigakura ni mpango wa kutaka Serikali ya Awamu ya
Nne iongezewa muda kwa kuwa haijajiandaa kukabidhi madaraka.
Wanajenga
hoja hizo kwa kueleza kuwa hadi sasa Serikali haijatoa zabuni ya
ununuzi wa vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, wakati haitakuwa rahisi
kukamilisha uandikishaji wapigakura mapema baada ya kazi hiyo kuchukua
muda mrefu mkoani Njombe na uchache wa vifaa.
Mwenyekiti
wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hakuwa na taarifa za kusitishwa kwa
uandikishaji mkoani Mbeya, lakini akaongeza kuwa wananchi wanatakiwa
kuwa wavumilivu kwani uandikishaji utafanyika kama ulilovyopangwa.
“Unajua
sikuwa na taarifa hizo kwa sababu nilikuwa katika kikao na wenyeviti
wenzangu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC). Kama kweli limesitishwa, itakuwa ni mchakato mdogo wa maandalizi
haujakamilika. Ila niwatoe hofu wakazi wa mkoa huo uandikishaji
utafanyika kama ulivyopangwa,” alisema Jaji Lubuva.
“Unaweza
kuwa na vifaa lakini kukawa na mambo madogo madogo yanayokwamisha na
ndicho kilichotokea Mbeya japokuwa sina taarifa kamili za kusitisha
mchakato huu,” alisisitiza Jaji Lubuva.
No comments:
Post a Comment