Dar es Salaam. Siku moja baada ya Ikulu kutangaza
kuwasafisha mawaziri watano na Katibu Mkuu, Eliackim Maswi, wabunge
wamejiweka pembeni na suala hilo wakisema Bunge lilishatimiza wajibu
wake.
Juzi, Ikulu iliwasafisha mawaziri wanne
walioshinikizwa kuachia ngazi na Bunge kutokana na kuhusishwa na sakata
la Operesheni Tokomeza Ujangili na mmoja aliyejiuzulu kutokana na kashfa
ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, pamoja
na katibu mkuu wa wizara.
Waliotangazwa na Ikulu kuwa
safi ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa na Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Wawili hao wanatajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM
ingawa hawajatangaza nia.
Wengine ni aliyekuwa Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo.
Hali
kadhalika, Profesa Sopster Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya escrow, pamoja na katibu mkuu
wa wizara hiyo, Eliackim Maswi aliyesimamishwa kutokana na sakata hilo,
wametangazwa kuwa safi.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri
Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema kitendo
cha Serikali kutangaza kuwa mawaziri hao hawakuhusika katika kutekeleza
makosa yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, kinaonyesha nia ya
kuendeleza tabia ya viongozi kutopenda matatizo yaliyotokea wakiwa
madarakani.
“Kilichofanyika ni kuionyesha dunia kuwa
hakuna kuwajibika, unapopewa jukumu lazima uwajibike. Sijui Taifa hili
linakwenda wapi? Nakosa hata maneno ya kuzungumza,” alisema Msigwa.
Msigwa,
ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii ambayo ni moja ya wizara
nne zilizohusika kwenye operesheni hiyo, alikuwa miongoni mwa wabunge
waliokuwa mstari wa mbele kuchangia wakati Bunge likijadili ripoti ya
kamati iliyochunguza suala hilo na kubaini ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Mbunge
wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema kuwa katika taarifa hakuna
kipya kwani haina tofauti na ile ya Kamati ya Bunge iliyoundwa
kuchunguza suala hilo.
“Ukifuatilia kwa makini taarifa
hiyo, utabaini ndiyo yaleyale yaliyokuwa yakijadiliwa bungeni na wabunge
nikiwamo mimi,” alisema Bulaya.
“Jana (juzi)
nilimsikiliza kwa makini sana (Katibu Mkuu Kiongozi) Balozi Sefue wakati
akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ila kichwani lilinijia
swali moja tu; hivi madai yaliyotolewa na wananchi katika tume
iliyoundwa kuchunguza jambo hili ya kweli au si kweli?” alihoji Bulaya.
“ Lakini Sefue mwenyewe amekiri kwamba madai yaliyotolewa na wananchi mengine yalikuwa yana ukweli ndani yake.”
Aliongeza
kuwa binafsi hayupo tayari kuzungumza habari za mawaziri, kwani hajui
utafiti au uchunguzi wao walipoufanya ila anachoweza kusema Bunge
limefanya kazi yake ipasavyo bila kumpendelea au kuumumiza mtu yoyote.
Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola, ambaye hakuwa amepata habari hizo hadi jana
alipoambiwa, aliungana na Bulaya kuwa Bunge lilitekeleza wajibu wake.
“Huko hatuhusika nako kwani huo ni mhimili mwingine,” alisema Lugola.
Mbunge
wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ambaye anaongoza jimbo lenye
wafugaji wengi, alidai kuwa taarifa hiyo haina jipya kwani ina mambo
yaleyale yaliyojadiliwa na wabunge wakati ripoti ikiwasilishwa bungeni
na kwamba kujiuzulu kwa mawaziri ilikuwa ni kisiasa na hakuna
aliyeonewa.
“Sisi wabunge hatukusema Waziri Kagasheki
kaua mtu, bali watendaji wake ndiyo walikuwa wazembe kwa kutokuwa makini
na kazi zao,” alisema Ole Sendeka.
“Sisi wabunge na
Bunge tumefanya kazi na hata wao wenyewe wamekiri katika ripoti yao na
wamesema kama sisi tulivyoitoa,” alisema Ole Sendeka.
John Shibuda, mbunge wa Maswa Magharibi, alihoji kama kuwajibika ni kukubali kufanya kosa.
“Kwani
(Rais wa Awamu ya Pili) Mzee Ali Hassan Mwinyi alipowajibika alikuwa
ameua? Nipo njiani ninakwenda kwenye mkutano wa wafugaji kutoka kanda ya
ziwa. Nitawasikiliza wana maoni gani kuhusu jambo hilo halafu
nitakwambia,” alisema.
Uamuzi wa Ikulu kuwaondolea doa
hilo mawaziri hao wanne umetokana na ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais
Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati
wa utekelezaji wa operesheni hiyo iliyolenga kuondoa ujangili kwenye
hifadhi za Taifa, lakini ikaishia kuua wananchi, kutesa na kupora mali
zao.
Pia, Profesa Muhongo na Maswi wamesafishwa baada
ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya uchunguzi na
kubaini kuwa hawakuhusika kuchota fedha kutoka akaunti hiyo ya escrow
wala kupewa rushwa na kwamba Maswi aliagiza fedha hizo zitolewe kwenye
akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu kwa kufuata ushauri wa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ambaye pia alijiuzulu kutokana na
kashfa hiyo.
Balozi Sefue aliwaambia wanahabari kuwa
tume iliyoundwa na Rais Kikwete ilijiridhisha kuwa mawaziri hao
waliwajibika kisiasa na hawakuhusika moja kwa moja na vitendo hivyo na
hakuna hatua inayostahili kuchukuliwa dhidi yao.
Rais
Kikwete aliunda tume hiyo Mei mosi mwaka jana kuchunguza malalamiko
yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Operesheni
hiyo ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utali kwa lengo la kupambana
na ujangili na ilitekelezwa kwa ushirikiano na wizara za Ulinzi, Mambo
ya Ndani na Kilimo na Mifugo.
No comments:
Post a Comment