Misikiti, makanisa, shule sasa kukatiwa bima za majanga - LEKULE

Breaking

10 May 2015

Misikiti, makanisa, shule sasa kukatiwa bima za majanga


Dar es Salaam. Serikali imeanza mchakato wa kutengeneza sera mpya ya bima na kupitia sera hiyo, majengo yote makubwa, zikiwamo shule za bweni, misikiti na makanisa yatatakiwa kukatiwa bima, ili litakapojitokeza janga lolote waathirika waweze kulipwa.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima, Israel Kamuzora wakati wa kikao cha wadau kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho cha wadau wa masuala ya bima, kililenga kupata maoni yao kuhusu sera hiyo mpya inayopendekezwa.
Kamishna wa Bima, Kamuzora alisema sera hiyo inalenga kupanua sekta ya bima nchini ili iweze kuchangia kikamilifu uchumi wa nchi.
Alisema kufikia Oktoba mwaka huu, wanatarajia kupeleka sera hiyo katika mamlaka husika ili ipitishwe.
“Sera hii ya bima inayopendekezwa, imelenga katika kuifanya sekta ya bima kuchangia kikamilifu uchumi wa nchi,” alisema Kamuzora.

Pia, alitumia nafasi hiyo kuelezea vipengele vinavyotaka misikiti, makanisa, shule na majengo mengine makubwa kuwa na bima za majengo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, ambaye kwa sasa ni mdau wa masuala ya bima, alisema ni vyema sera hiyo ikapelekwa kwa wadau wengine muhimu ili waweke mchango wao pia.

Aliwataja wadau hao muhimu kama Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Kwa miaka mingi tumekuwa na sera nzuri, lakini zimekuwa zinajikita katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini tumekuwa na udhaifu kuangalia masuala ya kiusalama. Tusifanye makosa hayo katika sera hii ya bima. Tumekuwa waathirika wa uhalifu wa kupangwa pamoja na uhalifu wa kisasa,” alisema.

Kamuzora aliunga mkono mawazo ya Manumba na kwamba atahakikisha vyombo hivyo vya ulinzi na usalama vinapata sera na hiyo na kutoa mawazo yao namna ya kuiboresha.

Aliongeza kuwa kupitia sera hiyo, halmashauri za wilaya na manispaa zitakuwa na jukumu la kuweka sheria ndogondogo zitakazosaidia utekelezaji wa sera hiyo.

No comments: