Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi inapenda kutoa taarifa kuwa hadi jana tarehe 03 Mei, 2015 raia wa Burundi
waliongia nchini kuomba hifadhi walikuwa 1,852.
Raia hawa wa Burundi waliingia nchini kupitia vijiji mbalimbali vya mkoa
wa Kigoma. Vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Kigaye, Sekeoya na
Kakonko. Vingine ni Kosovo, Kagunga na
Kibuye, huku wengine wakiwa wamepitia katika Kituo cha Uhamiaji cha Manyovu
kilichopo mkoani Kigoma.
Baada ya kufanyiwa mahojiano
ya kina katika kituo maalumu kilichopo mjini Kigoma, 1,252 kati yao
wamehamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu
Mkoani Kigoma na mahojiano yanaendelea kwa waliobaki na wanaoendelea kuwasili.
Shughuli ya kuwahoji na
kuwahamishia katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu inafanywa na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa
linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), pamoja na wadau wengine.
Aidha Serikali za vijiji
zinasaidia kuwapokea na baada ya kufanyiwa ukaguzi, hatimaye wanasafirishwa
hadi mjini Kigoma.
Pamoja na ujio wa raia hawa
wa Burundi, hali ya ulinzi na usalama katika maeneo wanapoingilia ni shwari na
hadi sasa hakuna matukio yoyote ya uhalifu yalitolewa taarifa. Vyombo vya
ulinzi na usalama vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vilivyopo katika maeneo
hayo vinaendelea na kazi zake kama kawaida.
Hata hivyo raia wanaoishi
katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi mkoani Kigoma wametakiwa kutoa
taarifa kwa Serikali za Vijiji vyao kuhusu wageni wanaofika katika maeneo yao,
badala ya kuwahifadhi kiholela majumbani mwao, na kuwa watakaobainika kukiuka
maagizo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.
Raia hawa wa Burundi ambao
wamekuwa wakiingia nchini wakiwa katika vikundi vidogovidogo wataendelea
kupokelewa kufuatana na taratibu na sheria zinazotawala upokeaji wa waomba
hifadhi.
Imetolewa na:
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI
WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
04 MEI, 2015
No comments:
Post a Comment