MBUNGE
wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ametonesha vidonda vya ufisadi
baada ya kuzungumzia ripoti ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue
iliyowasafisha baadhi ya watendaji serikalini waliohusika katika kashfa
ya Escrow.
Serukamba
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu,
alishangazwa na taarifa hiyo kuwasafisha baadhi ya watu waliohusishwa
katika kashfa hiyo na kuwaacha wengine, jambo ambalo alisema ni ubaguzi.
Kauli
hiyo aliitoa bungeni mjini Dodoma jana alipokuwa akichangia Hoja ya
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoiwasilisha bungeni
juzi akiomba Sh trilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Katika
mchango wake, Serukamba alisema ni vizuri Bunge likaitaka Serikali
itangaze kuwa wote waliohusishwa katika kashfa hiyo nao ni wasafi.
Alisema
haoni mantiki kwa Serikali kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Eliackim Maswi na Waziri Profesa Sospeter Muhongo na
kuwaacha wengine waliowajibika pamoja.
Serukamba
alisema kwa kuwa Serikali imewasafisha viongozi hao ni wazi kuwa
muamala uliofanyika wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika
akaunti ya Tegeta Escrow ni halali.
Mbunge
huyo alisema ili kutenda haki kwa watu wote ni vema wanasiasa wengine
waliojiuzulu nyadhifa zao na kuwajibishwa kwa Azimio la Bunge warejeshwe
katika nyadhifa zao.
Waliopoteza
nyadhifa zao kutokana na kashfa ya Escrow ni pamoja na aliyekuwa Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine
ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja.
“Kuhusu
suala la Escrow, juzi Katibu Mkuu Kiongozi alitoa ripoti baada ya
uchunguzi kufanyika ripoti ikasema katibu mkuu wake na waziri wake ni
safi maana yake mwamala ule ni safi.
“Kama
mwamala ule ni safi, katibu ni safi waziri ni safi, Chenge anakuwaje
mchafu? Tibaijuka anakuwaje mchafu? Ngeleja anakuwaje mchafu?
Mliowapeleka mahakamani wanakuwaje wachafu? Haiwezekani tuache hizi ni
style za zamani.
“Bunge
lako linadhalilishwa watu walidanganya watu walileta document (nyaraka)
feki wanatetewa, Tibaijuka tulimhukumu kwa nini? Ina maana kwa
Serikali hii kuna watu ni wazuri na wengine ni wabaya tuambieni. Nataka
waziri mkuu aje atuambie usafi wa hawa watu ni nini.
“Jingine
mheshimiwa spika ni suala la Tokomeza, mmefanya vizuri sana, mheshimiwa
spika tuliomba ripoti ya Tokomeza hawakuleta na kama Serikali mmesema
mawaziri wale ni safi naomba muwarudishe katika wizara zao.
“Kule
Kenya kipindi fulani Waziri wa Fedha alituhumiwa kwamba amekula rushwa
akajiuzulu, Mwai Kibaki (rais mstaafu) akaunda tume ya judicial (tume ya
kimahakama) kama mlivyounda kwenye Tokomeza, ripoti ilipotoka
ilionyesha kuwa Waziri wa Fedha, Amos Kimunya hana kosa lolote, rais
alimteua kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
“Mnapoamua
kuchukua hizi njia za juu za good governance (utawala bora) msiishie
nusu, haiwezekani muishie kwenye nusu, tukiamua kuchunguza na tukabaini
kuwa hawakukosea tunawarudisha kwenye nafasi zao, ndiyo matakwa ya good
governance (utawala bora). Tuache usanii hapa kwenye hili jambo.
“Kuna
watu hapa Maige alituhumiwa kuwa alisafirisha wale wanyama twiga kwenda
nje, muundieni tume ili tuone kweli kama ni yeye ndiye alikwenda
kwenye ndege kuwaingiza pundamilia ili na yeye mumsafishe mbona
mnasafisha watu nusu, hii ni nini?
“Akina
Ngeleja hapa akina Mkulo waundieni tume wote tujue kama walikosea.
Haiwezekani muumize wachache mimi katika hili hapana kama kuna jambo
linaniumiza ni injustice, haiwezikani tuwe na Serikali ya double
standard (ndumilakuwili).
“Walijiuzulu
akina Karamagi (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) hapa akina
Msabaha (aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki), waziri mkuu (Edward
Lowassa). Kwa nini hamkuunda judicial inquiry (tume)?” alisema na kuhoji Serukamba.
Mbunge
huyo alisema inaweza kuwa ndiyo njia nzuri za utawala bora kwa mtu
aliyejiuzulu kuundiwa tume kujua kama kweli alikosea arudishwe katika
nafasi yake.
“Suala
hili la Escrow mheshimiwa spika lazima akina Chenge nao wasafishwe,
vinginevyo mniambie na hawa mliowasafisha ni wachafu. Mnatumia nguvu
nyingi kuwasafisha lakini mnafanyaje nusu? Au wengine mna ajenda nao?
“Hebu
tuambieni kama kuna ajenda, hapa akina Mwambalaswa walivuliwa uenyekiti
wa kamati na wenyewe semeni kwamba hawakukosea kwa nini muishie nusu?
“Hatuwezi
kunyamaza tuache uonevu kwa watu haiwezekani, kuna watu ni wema na
wengine ni wabaya haiwezekani. Hiki si chama tunachokijua wote. Werema
(aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali) aliondoka kwa sababu gani,
maana kama mnasema mwamala ni safi waliosimamia wote ni safi wengine ni
wachafu.
"Kuna watu Ikulu nao walituhumiwa lakini bado wapo ofisini sasa Werema mlimuondolea nini uanasheria wake?” alisema.
Baada
ya kumaliza kuchangia, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka
(CCM) alinyanyuka katika kiti chake na kwenda kumpa mkono Serukamba na
baadaye alitoka ndani.
Kwa upande wake Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalasawa (CCM), alipingana na Serukamba katika dhana ya watu kusafishwa.
Mwambalaswa
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa hiyo, alisema hapingani na uamuzi
wa Bunge.
“Kimsingi
mimi sipingani na azimio la Bunge sihitaji kujitetea wala kusafishwa.
Mimi nilikuwa mjumbe wa bodi ya Tanesco niliwajibika katika siasa kwa
hivyo sihitaji kusafishwa kwa kuwa si mchafu na wala sina matope,” alisema.
No comments:
Post a Comment