MAKAMU
Mwenyekiti wa marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, Angel George, amesema mipango imekamilika ya
kwenda kuchangia damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es
Salaam.
George
alitoa taarifa hiyo jana jijini hapa, baada ya kusoma taarifa kwenye
vyombo vya habari ikieleza kwamba, Hospitali ya Taifa Muhimbili
inakabiliwa na uhaba wa damu.
“Hii
taarifa tumeiona, tayari tumewasiliana na marafiki wa Lowassa waitwao
Friends of Lowassa nchi nzima na naamini tukimaliza kikao leo, safari ya
kwenda kuchangia damu kule Muhimbili ili kuokoa maisha ya Watanzania
wenzetu itakuwa tayari.
“Kwa
hiyo naomba nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania wenzetu wanaojali na
kuthamini maisha ya Watanzania wote, wajitokeze ili kufanikisha
uchangiaji wa damu,” alisema George.
“Sisi
ambao ni marafiki wa Lowassa, tumeamua kufanya shughuli hizo za
kuisaidia jamii ili kumuunga mkono na kumhamasisha Lowassa anayetarajiwa
kutangaza nia hivi karibuni ya kuwania urais kupitia CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
“Hii
ndiyo hamasa yetu kwake sisi marafiki zake na tumeamua kuisaidia jamii
kwa kuchangia damu ili kuitanguliza jamii mbele. Lakini hata kwake ni
hamasa kwamba akifanikiwa kuingia Ikulu, jamii iwe ya kwanza,” alisema.
Kupitia
vyombo vya habari juzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa
Wateja cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema
hospitali hiyo imekumbwa na uhaba wa damu hatua ambayo imelazimu kuomba
msaada wa dharura serikalini na kwa watu binafsi.
Alisema
uongozi wa hospitali hiyo umewaomba Watanzania, mashirika ya umma,
kampuni na watu binafsi, kujitokeza kwa wingi ili kuchangia damu kwa
ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopelekwa hospitalini hapo.
“Kwa
siku Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huhitaji wastani wa chupa za damu
70 hadi 100 na hii inachangiwa na ongezeko la mahitaji ya damu ambayo
hutumika zaidi kwa wagonjwa wa dharura, wajawazito, wagonjwa
waliofanyiwa upasuaji, watoto na wagonjwa wa saratani,” alisema
Aligaesha.
No comments:
Post a Comment