RAIS Jakaya Kikwete ameagiza Wakuu wa Mikoa na Maofisa Elimu wote
nchini, kuanza ujenzi wa shule maalumu za kidato cha tano na sita kwa
kila kata na wakishindwa, katika shule za sekondari za kata, wachague
baadhi na kujenga madarasa ya vidato hivyo.
Alitoa agizo hilo jana katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya
Elimu, yaliyoadhimishwa kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma
na kuwakumbusha kuwa kati ya wanafunzi waliofaulu kwenda kidato cha tano
mwaka huu, ni asilimia 75 tu walioendelea na masomo hayo.
“Wakuu wa mikoa na maofisa elimu mliopo hapa naagiza na hili ni kwa
nchi nzima, tuanze utaratibu wa kuwa na shule za kidato cha tano na sita
za kata. Mnaweza kujenga shule mpya, au mchague baadhi ya sekondari za
kata ziwe na kidato cha tano na sita,” alisema Rais Kikwete na kuongeza
kusema si vyema kuwaacha mtaani asilimia 25 wenye sifa ya kuingia kidato
cha tano.
Alisema bila kuchukua hatua hiyo, Tanzania inaweza kurudi katika hali
ya elimu aliyoikuta ambapo wanafunzi wenye sifa ya kuendelea na masomo,
waliachwa kutokana na ufinyu wa nafasi za kuendelea na elimu.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati alipokuwa akiingia madarakani,
alikuta asilimia sita tu ya wanafunzi waliokuwa wamefanya Mtihani wa
Taifa wa Darasa la Saba, ndio waliokuwa wakichaguliwa kuendelea na elimu
ya sekondari.
“Leo kila anayefaulu darasa la saba, anakwenda sekondari… tukisema
leo mwanafunzi amefeli darasa la saba amefeli kweli tofauti na zamani
ambapo walikuwa wakichaguliwa,” alisema Rais Kikwete.
Tanzania ilipotoka
Rais Kikwete alielezea sababu ya Serikali inayomaliza muda wake kuwekeza zaidi katika elimu, kiasi kwamba bajeti ya elimu katika Mwaka wa Fedha unaoisha kuwa kubwa kuliko ya sekta zingine, inayofikia Sh trilioni 3.4 kutoka Sh bilioni 600 iliyokuwepo mwaka 2005.
Rais Kikwete alielezea sababu ya Serikali inayomaliza muda wake kuwekeza zaidi katika elimu, kiasi kwamba bajeti ya elimu katika Mwaka wa Fedha unaoisha kuwa kubwa kuliko ya sekta zingine, inayofikia Sh trilioni 3.4 kutoka Sh bilioni 600 iliyokuwepo mwaka 2005.
Sababu ya kwanza: Rais Kikwete alisema, waliona kuwa kuwekeza katika
elimu ndio kuwekeza katika taifa na Serikali isingechukua uamuzi huo,
Watanzania hawataweza kutawala mazingira yao na kutumia vizuri
rasilimali zao.
Pili alisema alipoingia madarakani, alikuta Tanzania yenye watu wengi
zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko nyuma
ikilinganishwa na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa
wakisoma shule za sekondari na vyuo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka 2005 wanafunzi waliokuwa wakisoma
sekondari ni zaidi ya 500,000, wakati nchini Uganda waliokuwa wakisoma
sekondari walikuwa zaidi ya 700,000 na Kenya zaidi ya 900,000.
Kwa upande wa vyuo vikuu, Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,000 tu wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi 124,000 na Kenya 180,000.
“Kuwa nyuma katika kutoa fursa ya elimu ikilinganishwa na wenzetu
ilikuwa inaweka nchi yetu katika mazingira mabaya katika ushindani wa
soko la ajira la Afrika Mashariki,” alisema Rais Kikwete.
Mbali na mazingira mabaya katika ushindani wa soko la Afrika
Mashariki, Rais Kikwete alisema Watanzania nao walifikia hatua ya kuamua
kupeleka watoto wao kwenda kusoma Kenya na Uganda.
Hatua zilizochukuliwa
Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.
Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.
“Tulihimiza wadau wengine wajenge vyuo vya elimu ya juu na kuamua
mikopo ya elimu ya juu itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vyote,” alisema
Rais Kikwete.
Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma
sekondari na imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma
elimu ya sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi
2,100,000.
Hata hivyo alisema ni rahisi kuipita Kenya kwa hilo pengo la
wanafunzi 300,000, kwa kuwa shule za sekondari zilizopo zina nafasi ya
kuongeza wanafunzi milioni mbili zaidi.
“Hapa lazima tuwafukuzie Wakenya, lazima tuwakute na kuwapita na huu
ni ushindani mzuri kwa kuwa ni ushindani wa maendeleo,” alisema Rais
Kikwete.
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu
vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi
walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
No comments:
Post a Comment