Pinda aainisha mafanikio ya Serikali ya JK kwa miaka 10 - LEKULE

Breaking

13 May 2015

Pinda aainisha mafanikio ya Serikali ya JK kwa miaka 10


Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana aliwasilisha Bajeti ya lala salama ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2015/16, huku akieleza mafanikio katika sekta mbalimbali yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Nne tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005.

Bajeti hiyo iliwasilishwa katika mkutano wa 20 wa Bunge la 10 ambao ndiyo wa mwisho kwa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya Bunge kuvunjwa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akitumia saa 2.30 kusoma hotuba hiyo ya kurasa 105, Pinda alisema katika mwaka 2015/16, ofisi yake imepanga kutumia Sh5.8 trilioni ambazo matumizi yake yatafafanuliwa katika bajeti za wizara zilizopo chini ya ofisi yake.

Pinda alitumia fursa hiyo kuzungumzia pamoja na mambo mengine, mafanikio katika usafirishaji wa reli, bila kugusia harufu ya ufisadi katika ununuzi wa mabehewa katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) uliosababisha vigogo wake watano kusimamishwa kazi.

Mafanikio ya Serikali

Pinda alisema tangu 2005 hadi 2014, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kwamba Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani 74,274 milioni na kutoa ajira 869,635.

Alisema katika kipindi cha miaka 10, Serikali iliwawezesha wananchi kubaini fursa za kiuchumi kupitia mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira ulioanzishwa mwaka 2006, kutoa mikopo ya masharti nafuu ya Sh50 bilioni iliyotolewa kwa wajasiriamali 74,790.

 “Katika mwaka 2015/16, Serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, vyama vya kuweka akiba na kukopa ili waweze kukopesheka,” alisema. Kuhusu ajira, alisema vijana walioajiriwa katika sekta ya umma ni 188,087 na walioajiriwa katika sekta binafsi ni milioni moja wakati vijana milioni 15 wamejiajiri katika shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara ndogondogo.

Alisema viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka huu.
Kuhusu uchumi, Waziri Mkuu alisema umekua kutoka asilimia 4.7 mwaka 2006 hadi asilimia saba mwaka 2014 na hivyo kuongeza pato la Mtanzania kutoka Sh360,865 mwaka 2005 hadi Sh1.7 milioni mwaka 2014.

“Uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 341,109 mwaka 2006 hadi tani 375,158 mwaka 2015. Tani 43,354 za mazao ya uvuvi na tani 42,100 za samaki hai wa mapambo ziliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa Sh7.5 bilioni. Viwanda vya kuchakata samaki vimeongezeka kutoka 25 hadi 48,” alisema Pinda. Pia, alizungumzia pia sekta ya utalii akisema idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi 1,102,026 na kuongeza mapato ya utalii kutoka Dola za Marekani 1,853 milioni hadi Dola 1,983 milioni.


Sekta ya madini

Pinda alisema thamani ya madini yaliyozalishwa nchini na kuuzwa nje iliongezeka kutoka Dola 655.5 mwaka 2005 hadi Dola milioni 1,794 mwaka 2014, huku sekta ya viwanda ikikua kwa wastani wa asilimia 7.7.

Barabara

“Serikali ya awamu ya nne imekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 1,226 na kilomita 1,305 za barabara kuu zimejengwa kwa kiwango cha lami na kilomita 960 kufanyiwa ukarabati. Kilomita 393 za barabara za mikoa zimejengwa kwa kiwango cha lami,” alisema.

Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanza ujenzi wa Bandari ya Mbegani - Bagamoyo itakayokuwa kubwa Afrika Mashariki na Kati sambamba na kujenga, kupanua na kukarabati viwanja vya ndege.

Kuhusu umeme, alisema Serikali imeimarisha miundombinu ya uzalishaji wa umeme nchini kwa kiwango kikubwa na kuongeza uzalishaji kutoka megawati 891 mwaka 2005 hadi 1,226 Machi 2015 na kwamba watumiaji wa umeme wameongezeka kutoka asilimia 13 hadi 36.

Pia, aligusia mafanikio yaliyopatikana katika elimu, ikiwamo ujenzi wa maabara, kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu na kuboresha sekta ya afya chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi wa mwaka 2007 hadi 2017.

Wanawake katika uongozi

Pinda alisema: “Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, idadi ya mawaziri wanawake imeongezeka kutoka sita kati ya mawaziri 25 mwaka 2005 hadi kufikia 10 kati ya mawaziri 30 mwaka 2015.”

 “Wakuu wa mikoa wameongezeka kutoka wawili kati ya 21 mwaka 2005 hadi saba kati ya wakuu wa mikoa 25 mwaka 2015. Wakuu wa wilaya wameongezeka kutoka 20 kati ya wakuu wa wilaya 104 mwaka 2005 hadi wakuu wa wilaya 46 kati ya 133 mwaka 2015.

Alisema majaji wanawake wameongezeka kutoka wanane kati ya 50 mwaka 2005 hadi kufikia 24 kati ya majaji 67 mwaka 2015 na wabunge wanawake wametoka 62 kati ya 288 mwaka 2005 hadi kufikia 127 kati ya 357 mwaka 2015.

Mauaji ya albino

Akizungumzia mauaji ya albino, Pinda aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri na kuelimisha jamii kuondokana na imani potofu za kishirikina kwa kuamini kuwa kupata kiungo cha albino ni kutajirika. “Mpaka sasa watuhumiwa 181 wamekamatwa na kuhojiwa tangu mwaka 2006 na 2015. Kati yao 133 wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi na 13 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa,” alisema Pinda.

Ajali za barabarani

Pinda alisema kuanzia Julai 2014 hadi Machi mwaka huu, kulikuwa na matukio 8,072 ya ajali za barabarani ambayo yalisababisha vifo vya watu 2,883 na kuwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vinafanya utafiti wa kina kuhusu ajali hizo.

No comments: