Dk Gharib Bilal amtuma Lowassa - LEKULE

Breaking

13 May 2015

Dk Gharib Bilal amtuma Lowassa

Dar es Salaam. Wakati CCM ikifanya jitihada za kudhibiti makada wake wanaotajwa kuwania urais, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amemtuma waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuendesha moja ya shughuli ambazo chama hicho kinaamini kuwa ni moja ya majukwaa ya kampeni kwa wagombea.

Dk Bilal amemtuma Lowassa, mmoja wa makada wanaotajwa kutaka urais, kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Patandi mkoani Arusha Alhamisi wiki hii, ambako habari zinasema siku mbili baadaye huenda mbunge huyo wa Monduli akatangaza rasmi nia yake ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu kwa tiketi ya CCM.

Taarifa iliyotolewa jana na mwandishi wa habari wa Makamu wa Rais, Boniface Makene inaeleza kuwa Dk Bilal anakabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa na hivyo ametoa ombi maalumu la kuwakilishwa kwenye harambee ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ulioanza mwishoni mwa miaka 90.
“Makamu wa Rais ameona kuwa shughuli hii ya uchangiaji wa ujenzi wa msikiti isisogezwe mbele kumsubiri, bali iendelee kwa kuwa anaamini Lowasa ana uzoefu katika kufaninikisha shughuli za aina hii. Pia mchango wake katika shughuli za harambee katika shughuli ni wa mfano,” inasema taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa mchango wa wanajamii wanaoswali katika msikiti wa Patandi ni mkubwa kwani wamekuwa wakijitoa kwa namna nyingi kujenga mshikamano baina ya jamii zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na wameshiriki kuwasaidia watoto yatima.
Uamuzi huo wa Dk Bilal, ambaye kwa nafasi yake anaingia kwenye vikao vyote vya juu vya chama tawala, vikiwamo vya Zanzibar, utakuwa umetikisa harakati za kudhibiti baadhi ya makada wanaotajwa kuwania urais, hasa kambi ya Lowassa ambayo inasemekana inalalamikia kuchezewa rafu na uongozi wa CCM, ingawa haijabainisha rafu hizo.

Lowassa ni mmoja wa makada sita waliopewa onyo kali na CCM Februari mwaka jana, likiwazuia kujihusisha na uchaguzi kwa zaidi ya miezi 12 baada ya kubainika kuwa walianza kampeni mapema kwa kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili, zikiwamo za harambee na hivyo kutakiwa kuomba kibali kabla ya kushiriki.

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita Lowassa na makada wengine wanaotajwa kuwania urais walialikwa Zanzibar kwenye harambee ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa Magharibi, ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki tangu walipofungiwa na chama hicho mwaka jana.

Wasomi waliotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uteuzi huo walikuwa na maoni tofauti.
“Sina mengi, hakuna atakayeshindwa kuona kuwa wana mu-endorse (wanamuunga mkono) huyo. Yeye (Lowassa) ni miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania urais, kwa hiyo hii ni moja  ya ‘technic’ mbinu,” alisema Profesa Tolly Mbwete ambaye ni mkuu wa Chuo Kikuu Huria.

Alisema uteuzi huo ni miongoni mwa harakati za kumuweka vizuri Lowassa katika uchaguzi ujao.
Lakini mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema iwapo Lowassa amepewa jukumu hilo na Dk Bilal, maana yake ameonekana ana uzoefu na anaifahamu kazi hiyo na aangaliwe kama waziri mkuu mstaafu na si vinginevyo.

Dk Makulilo alisema kuteuliwa kufanya kazi ya harambee hiyo wakati kama huu kunatafsiriwa kama ni kitendo cha kupigiwa chapuo kisiasa katika uchaguzi mkuu.

“Lakini Lowassa ana ujuzi, kwa sababu ni waziri mkuu mstaafu, lakini katika siasa hakuna shida ya kumtumia kiongozi huyo kwa sababu aliwahi kufanya harambee nyingi za kiserikali, kichama na za kwake binafsi,” alisema.

Dk Makulilo alisema kupewa kwa Lowassa kuifanya kazi hiyo kunachanganywa na nafasi yake ya kutaka urais na makundi ndani ya CCM.

Kabla ya kufungiwa, Lowassa alikuwa akipata mialiko mingi ya kushiriki katika harambee za vikundi mbalimbali vya kijamii ikiwa ni pamoja na makanisa, misikiti na vikundi vya wasanii na kufanikisha kupatikana mamilioni ya fedha.

Tangu apewe adhabu hiyo, Lowassa amekuwa kimya na badala yake vikundi vya watu mbalimbali vimekuwa vikienda jimboni kwake Monduli mkoani Arusha na kwenye makazi yake akiwa bungeni mjini Dodoma kumshawishi aingie kwenye mbio za urais.

Lakini wakati vikundi hivyo vikizidi kumiminika, viongozi wa CCM walianza kutoa kauli za kuponda vitendo vya kushawishi makada wa chama hicho kugombea urais, wakisema kuwa ni mchezo wa kuigiza.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa akidai kuwa watu waliokuwa wakienda nyumbani kwa kada wa chama hicho, ambaye hakumtaja jina, kwa lengo la kumshawishi achukue fomu za kuwania urais, walikuwa wanapangwa kwa kuwa mwanachama huyo alishatia nia na ndio maana alianza mapema kampeni zilizosababisha apewe adhabu.

Nape amekuwa akikaririwa mara kwa mara akitoa kauli zinazoonyesha kukinzana na kambi ya mbunge huyo wa Monduli na wakati fulani Lowassa, bila ya kumtaja katibu huyo wa uenezi wa CCM, alisema madai hayo ni ya kipuuzi  na kwamba hawezi kumjibu kwa kuwa akifanya hivyo atampa umaarufu.

Vita ya urais kwa tiketi ya CCM imekuwa na sura tofauti na inazidi kupamba moto kadri siku za kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu zinavyokaribia.

Mapema wiki hii ulienea ujumbe kwenye mitandao unaoonyesha kuwa Lowassa ameguswa na maombi ya wananchi ya kumtaka agombee urais na kwamba amepanga kutangaza rasmi uamuzi wake Jumamosi kwenye hafla itakayofanyika mjini Arusha.

Kambi ya Lowassa ilijitokeza mapema kupinga taarifa hiyo ikisema kuwa haikutumwa na mwandishi wa mbunge huyo wa Monduli, Aboubakar Liongo na kwamba taarifa zinazotolewa na ofisi ya kada huyo huwa hazimuelezei kuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Lowassa anaweza kutangaza rasmi uamuzi wake wa kuingia kwenye mbio hizo Jumamosi kwenye Uwanja wa NMC mjini Arusha baada ya uwanja wa chama chake  wa Sheikh Amri Aneid kufungwa.

Hivi sasa kuna kesi Mahakama Kuu ambako makada wawili wa CCM, John Guninita, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Dar es Salaam, na Hamisi Mgeja, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Shinyanga, wamefungua kesi dhidi ya mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Paul Makonda kwa madai kuwa aliwadharirisha.

Makonda ambaye kwa sasa ni mkuu wa wilaya ya Kinondoni anadaiwa kuwaelezea wawili kuwa ni vibaraka wa Lowassa kutokana na kueleza msimamo wao kwa mbunge huyo wa Monduli.

No comments: