Dodoma. Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya
kudai kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kichovu, kauli ambayo ilizua
mabishano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama.
Akichangia
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2015/16, Lissu alisema Serikali hiyo
imeshindwa karibu kila jambo, ikiwamo uandikishaji wa wananchi katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema uchovu huo pia
umejidhihirisha wazi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza
kwamba mpaka sasa haijapewa fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba, wakati imebaki miezi mitano ufanyike.
Lissu
alivutana na Spika Anne Makinda pale alipotakiwa kukaa chini kumpisha
Mhagama azungumze baada ya kugoma kwa maelezo kuwa waziri huyo
ameingilia wakati akitoa ufafanuzi wa uchovu wa Serikali.
Mvutano
huo ulianza Lissu alipokuwa akisema kuwa mbali na kukwama kwa
uandikishaji katika Daftari la Wapigakura, hata katika upigaji wa kura
za kupitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge Maalumu la Katiba,
marehemu, mahujaji na wagonjwa ni miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo
waliopiga kura.
“Hata Uchaguzi Mkuu mpaka sasa Serikali
haijatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hakuna maandalizi yoyote.
Hatukubali kuona Serikali hii ikijiongezea muda kwa kisingizio hicho,”
alisema Lissu.
Kauli hiyo ilimwinua Mhagama na kueleza
kuwa katika Bunge la Katiba zilipigwa kura halali, huku akifafanua jinsi
Serikali ilivyofanya shughuli nyingi za maendeleo.
“Mheshimiwa
Spika, Lissu analidanganya Bunge. Kauli zake ni za kuudhi namwomba
asiendee kupotosha umma,” alisema Mhagama huku Lissu akisisitiza kauli
yake.
Wakati Mhagama akisimama kuomba utaratibu wa
Spika, Lissu naye alisimama akipinga kitengo cha kukatizwa na waziri
huyo kuchangia, tukio ambalo liliingiliwa na Spika na kuzua majibizano.
“Huyu
ananizuia kwa misingi gani, kafuata utaratibu upi,” alisema Lissu huku
Mgahama naye akiendelea kuzungumza huu akiwa amesimama kabla ya wote
wawili kukatishwa na Spika Makinda aliyewataka wakae chini na kufafanua
kuwa yeye ndiye anayejua utaratibu.
Baada ya kutoa
ufafanuzi huo, Makinda alimpa nafasi Mhagama kuendelea kuzungumza na
alipomaliza alimpa nafasi Lissu ili amalizie kuchangia hotuba hiyo.
Mbowe
Awali,
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliwasilisha
hotuba ya kambi hiyo, akisema hakuna maandalizi yoyote yanayofanywa na
Serikali ambayo yanaashiria wazi kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba
mwaka huu.
Mbowe ambaye pia hakumaliza kusoma hotuba
yake baada ya kukatishwa na Spika wa Bunge, Makinda baada ya kuibuka
ubishi juu ya muda wa uwasilishaji, alisema hayo wakati akitoa maoni ya
kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema
ukweli huo umethibitishwa na NEC kwenye ukurasa wa randama ya Tume hiyo
namba 13 unaosema: “Kwa upande wa maandalizi ya Kura ya Maoni na
Uchaguzi Mkuu, 2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa.”
Alihoji
kama Serikali haijaipatia Tume fedha kwa ajili ya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu, inategemea miujiza gani kuwa ifikapo Oktoba uchaguzi huo
utafanyika.
“Ni lini zabuni zitatangazwa kwa ajili ya
makandarasi mbalimbali ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu na tarehe ya kuwapata hao wazabuni ni lini?” alihoji.
Alisema
wakati Serikali ikishindwa kuipatia NEC fedha kwa ajili ya kufanya
maandalizi ya uchaguzi ili ufanyike katika mazingira ya amani, haki na
utulivu, imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi wake.
“Hii
ni kutokana na ukweli kuwa tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza
zaidi ya magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya maji
ya kuwasha, doria na shughuli za ukaguzi katika mwaka huu wa fedha,”
alisema.
Alisema NEC inadaiwa madeni na makandarasi
ambao walisambaza vifaa kwenye uchaguzi uliopita ambayo yanathibitishwa
kwenye randama ukurasa wa 13, lakini hazikutengwa kwenye bajeti
Kura ya maoni
Mbowe
alisema Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka 2013, iliweka bayana muda
maalumu wa kuchapisha swali la kura ya maoni, kutoa elimu kwa umma na
siku ya kufanyika kwa kura ya maoni na kuwa muda wa kufanya yote hayo
kwa mujibu wa sheria umeshapita.
“Haiwezekani tena kwa
kura ya maoni kufanyika sasa au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya
maoni ya mwaka 2013 kuletwa bungeni.”
No comments:
Post a Comment