MASLAHI: Goran aishangaa Simba kumtosa - LEKULE

Breaking

18 May 2015

MASLAHI: Goran aishangaa Simba kumtosa

Dar es Salaam.
Kocha Goran Kopunovic amesema kiasi cha dola 20,000 pekee ndiyo kimemyima ajira ya kuendelea kuifundisha Simba kwa ajili ya msimu ujao.
Akizungumza na gazeti hili kutoka kwao Belgrade, Serbia  jana asubuhi,  Kopunovic alisema pande zote mbili zimeshindwa kukubaliana na sasa kila mtu anaweza kuangalia mustakabali wake sehemu nyingine.

Kopunovic ambaye aliikuta Simba ikiwa katika nafasi ya nane katika Ligi Kuu Bara na kuiacha katika nafasi ya tatu alisema baada ya ofa yake ya awali ambayo alitaka Wekundu hao wampatie kiasi cha dola 50,000 (Sh 100milioni) na mshahara wa dola 14,000 ( Sh28 mil) alilazimika kushusha kwa mara mbili kuwaridhisha viongozi hao jambo ambalo limeshindikana.

Alisema ofa ya mwisho ambayo alilazimika kuwapa Simba kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe aliitaka kumpatia dola 45000 (Sh90 Ml) kama ada ya kuongeza mkataba, huku pia akishusha mshahara wake mpaka dola 6500 (Sh 13milioni) ili asaini mkataba wa miaka miwili.
“Ukiangalia tofauti yangu ni ndogo ni kama dola 20,000 tu kwa sababu wao walitaka wanipe dola 25,000 kama kiasi cha kusaini mkataba mpya na mshahara wa dola 6,000, kama imeshindikana nawatakia kila la kheri wachezaji na hata mashabiki wa timu bado nitabaki mtu wa Simba,” alisema Goran.

“Nafikiri kila kitu kimeshindikana mimi siyo kocha ghali hapana, lakini najiamini kwamba ni kocha mzuri ambaye naweza kuipa mafanikio timu yoyote, lakini nina mahitaji yangu ukiangalia walitaka nisaini mkataba wa miaka miwili,”alisema Kopunovic.

Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Hanspoppe alisema klabu hiyo kwa sasa haina kiasi hicho cha fedha na wameamua kutompa mkataba mpya kocha huyo, wameanza kutafuta kocha mpya ambaye atakuja kusaidiana na Seleman Matola.

“Tumempa ofa yetu, akasema anaenda kuongea na familia yake kwanza, tulimtaka hadi Ijumaa (Mei 15) awe ametupa jibu, lakini akatuambia kwamba hawezi kuchukua kiasi hicho, tumeshindwa na sasa tunatafuta kocha mwingine,” alisema Hanspoppe.

Tayari Simba inahusishwa na kumtaka kocha Mbelgiji, Piet Demol anayetarajiwa kutua Dar es Salaam wiki hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuifundisha timu hiyo.

Hata hivyo, Demol hajawahi kufundisha klabu yoyote ya Afrika zaidi ya kuwa mkurungezi wa ufundi katika shule ya kukuzia vipaji ya Kumasi, Ghana pamoja na kuwa mshauri wa klabu ya Asante Kototo.

Katika hatua nyingine; wachezaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Nassoro Masoud ‘Chollo’ na Awadh Juma wanaamini bado timu hiyo inamuhitaji kocha Kopunovic  kwa msimu ujao.

“Simba tunapaswa kutulia kipindi hiki, tujipange kwa ajili ya ubingwa msimu ujao, sioni sababu ya kuachana na Goran, ni kocha mzuri na kiwango chake kimeonekana kwa kipindi hiki kifupi alichotufundisha,” alisema Awadh Juma na kuongeza.

“Kila mdau wa Simba anatambua Goran aliikuta timu katika hali gani, tangu amekuja kiwango kimeonekana na tunacheza kitimu.”

Okwi alisema ujio wa Goran umeifanya timu kumaliza ligi katika nafasi ya tatu, kubaki au kuachana naye nawaachia uongozi waamue.

Wakati Chollo alisema hataki kuingilia masuala ya uongozi, lakini bado anaamini uwepo wa kocha Goran unahitajika.

“Mimi kama mchezaji nauachia uongozi ufanye kazi yake, siwezi kuyaingilia masuala yao, lakini Goran bado ana nafasi Simba,” alisema Chollo.


No comments: