Dar es Salaam.
“Ni vigumu kumudu kazi na familia kwa wakati wote kutokana na
ukweli kwamba mwanamke anakabiliana na majukumu mengi ikiwamo ya kazini,
kuhudumia familia na wakati huohuo kuangalia mume, lakini hatuna budi
kukabiliana na changamoto hizi ili kuwa na familia bora.”
Ndivyo
anavyoanza kusema Hilda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Idara ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Mwenyewe
anasema kilichomwezesha kufika hapo ni juhudi zake za kupenda
kujiendeleza na kusoma hasa ukizingatia fani hiyo aliipenda tangu akiwa
mdogo.
Hilda ambaye ni mama wa watoto wawili, anasema
dhamira ya kuwa mwanasheria ilichagizwa na tamthilia aliyowahi
kuiangalia ya ‘Inspector Dereck’na ambaye katika tamthilia hiyo
alionekana akizungukazunguka mahakamani akiwa amevaa suti yake nyeusi
yenye kumpendeza.
“Ukweli ni kwamba nilikua nikivutiwa
sana na mavazi ya wanasheria wakiwa mahakamani na hii ndiyo ilinifanya
nisome kwa bidii kwa kuamini kuwa ipo siku ndoto yangu itatimia na
kufikia malengo yangu,” anasema Hilda (34).
Kwa mujibu
wa Hilda, alitamani siku moja kuwa mwanasheria ili kuwahudumia watu
wenye matatizo mbalimbali ikiwamo unyayasaji wa kijinsia dhidi ya
wanawake na watoto, migogoro ya kifamilia na ardhi, kutoa haki pamoja na
kutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaohitaji.
Hilda
ambaye kwa sasa ni mwendesha mashtaka wa Serikali katika Wilaya ya
Ilala, anasema safari yake hadi kufikia hapo haikuwa rahisi kwani
alipitia changamoto mbalimbali lakini hakukata tamaa kufikia malengo
yake.
Muda wa kazi na familia:
“Huku
mtoto anahitaji uangalie kazi yake aliyofanya shuleni, huku mume
anakuhitaji umbembeleze, wakati huo huo unawaza kesi mahakamani, hii ni
changamoto inayopaswa kukubaliana nayo cha msingi ni kuhakikisha kila
kitu kinafanywa kwa wakati wake.”
Anasema kinachotakiwa
kwa wanawake ni kupangilia muda wa kazi na muda wa majukumu ya nyumbani
na hali hiyo itasaidia kuwa na familia yenye furaha na siyo kila wakati
kumuachia mfanyakazi wa nyumbani kwa kisingizio cha kazi.
Hata
hivyo, Hilda anasemea hapendi kuona wanaume wananyanyasa wake zao huku
akiwataka wanawake wajishughulishe katika biashara za ujasilimali ili
kujenga familia bora.
Anasema hali hiyo inasababisha
wanawake wengi kukata tamaa hivyo hutumia muda wake wa ziada kutoa
msaada wa kisheria pamoja na kuwapa matumaini wale ambao wanamigogoro.
“Nachukia
kuona watoto wakiteseka mitaani na kuvunjika kwa familia kwa hali hii
huwaathiri zaidi watoto na kuwapotezea ndoto zao za baadaye, hivyo
nawashauri wa wanawake wenzangu kumshirikisha Mungu ili kuzinususru.”
anasema Hilda na kuongeza kuwa kesi nyingi za wanandoa huwaathiri sana
watoto wao. Mwanasheria huyo ambaye shahada yake ya kwanza ya sheria
aliyoichukua mwaka 2001 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Anapokuwa nyumbani anafanya nini?
Hilda
anasema anapenda kutengeneza bustani ya maua kwani inafanya nyumba iwe
na mwonekano wa kuvutia. Anasema sambamba na kujihusha na masuala ya
bustani akiwa nyumbani pia ni hupenda kupika, kusoma vitabu, kuangalia
kazi za shule za watoto wake na kuangalia luninga ili kujua vitu
vinavyojiri ulimwenguni.
No comments:
Post a Comment