Mapendekezo ya CAG yanapuuzwa - LEKULE

Breaking

21 May 2015

Mapendekezo ya CAG yanapuuzwa

Dar es Salaam. Ushauri unaotolewa mara kwa mara kwa Serikali, taasisi zake na mashirika ya umma umekuwa ukipuuzwa na kusababisha Serikali kuendelea kupoteza fedha nyingi kwa njia ya ufisadi huku Deni la Taifa likizidi kukua, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti ya CAG imeweka bayana ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha na ripoti hiyo maalum inaonyesha kuwa uovu huo umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa uchanganuzi wa Mwananchi, Sh600 bilioni zilizofanyiwa ufisadi, zingeweza kusaidia kupunguza nakisi kwenye bajeti ya Serikali kwa kuelekezwa kwenye wizara tatu ambazo ni Ofisi ya Rais, iliyopangiwa Sh587 bilioni, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh68.8 bilioni) na Ofisi ya Makamu wa Rais (Sh112 bilioni).
Pia, fedha hizo zingeweza kujenga vyumba 8,000 vya madarasa kwa gharama ya Sh75 milioni kila kimoja au kuwezesha vijana zaidi ya mara 12 ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, au kujenga kilomita 600 za barabara kwa kiwango cha lami.
Ukaguzi huo maalumu ulifanywa ili kuangalia kama rasilimali zilizotengwa zimetumika kwa ufanisi kwa kuzingatia kiwango cha fedha kilichowekezwa, tija na ufanisi kama ilivyotarajiwa na kupitishwa na Bunge kwenye maeneo kadhaa, inaeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapendekezo ya CAG yalitolewa katika ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi za miaka ya nyuma kwenye maeneo ya usimamizi wa udhibiti wa athari za mafuriko kwa Serikali, mikoa na serikali za mitaa uliofanyika kwa kutumia mafuriko yaliyowahi kutokea Babati (2007).
Vilevile, mapendekezo hayo yalilenga katika kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma ya afya ya msingi, ukaguzi uliofanyika kwenye vituo vya afya (2009); programu za ukaguzi wa shule za sekondari nchini (2009) na usimamizi wa udhibiti wa taka ngumu nchini na usimamizi wa ujenzi wa barabara (2010).
Sehemu nyingi za matokeo ya uchunguzi kwenye ripoti hiyo zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ulifanywa chini ya asilimia 50.
Mapendekezo hayo yalikuwa kwenye utunzaji wa kumbukumbu za miradi na kuwapo mfumo wa ufuatiliaji, miradi kuchelewa kumalizika na kuongeza gharama, ukusanyaji mapato, utoaji wa fedha kwa taasisi za Serikali kama Bohari ya Madawa ili kusaidia kupunguza ongezeko la Deni la Taifa, halmashauri kuwa na mifumo bora ya utoaji kandarasi, mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wakaguzi wa elimu wa shule za sekondari na ugawaji na usimamizi wa dawa na vifaa tiba.
Wizara ya Ujenzi, ambayo mwaka jana iliidhinishiwa Sh1.22 trilioni, inaelezwa kutofanya tathmini ya kutosha kabla ya kuanza miradi ya ujenzi wa barabara na kusababisha ichukue muda mrefu kukamilika kutokana na makandarasi kusubiri kuondolewa kwa nyaya za simu, mabomba ya maji na miundombinu ya umeme.
Pia, wizara husababisha ongezeko la gharama za miradi kutokana na kuwapo na tofauti kubwa ya makadirio ya awali na gharama halisi. “Ufuatiliaji uliofanywa kwenye utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa umebaini kuwa kumekuwa na pungufu kwenye ufanisi wa udhibiti wa bajeti ambao ungeweza kusaidia kuzuia ongezeko la gharama kati ya bajeti ya mwanzo na bajeti iliyofanyiwa marekebisho kwenye miradi ya Ujenzi wa barabara nchini,” inasema ripoti hiyo.
Katika ukaguzi huo CAG anaonyesha jinsi kulivyokosekana ushahidi wa kuondolewa kwa mali zinazopita nchini kuelekea nchini jirani na kubakizwa na kisha kuingizwa sokoni, hivyo Serikali kukosa makusanyo ya kodi ya Sh835 bilioni.
“Mapitio ya mfumo wa kutunzia taarifa (Asycuda) kwa mwaka 2013/14 umeshindwa kuthibitisha uondoaji wa mizigo 1,316 iliyoingizwa nchini kwa muda kutoka nchi mbalimbali kinyume na sheria ya kusimamia ushuru wa forodha wa Afrika Mashariki,” inaeleza.
Zitto asema haikubaliki
Mbunge wa zamani Kigoma Kaskazini, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema: “Kiasi ambacho hakikulipwa yaani Sh800 bilioni ni sawa na asilimia 10 ya makusanyo yote ya kodi za ndani.”
Alisema wakati fedha hizo zinapotea, Serikali inakosa fedha na hivyo kushindwa kuendesha miradi mingine.
“Fedha iliyokwepwa Idara ya Forodha peke yake inalipa madeni yote ya makandarasi wa barabara wanaoidai Tanroads. Fedha hii ingelipa madeni yote ya mfuko wa PSPF wanayoidai Serikali. Fedha hizi zingeweza kulipia miradi miwili mikubwa nchini ya mashine za kielekroniki (BVR) na vitambulisho vya Taifa ambayo inasuasua kutokana na ukata,” alisema.
Ripoti hiyo inabainisha ufisadi wa kufanya malipo bila ya viambatanisho kwenye wizara, idara za Serikali na balozi, hali kadhalika matumizi nje ya bajeti.
Ripoti ya CAG inaonyesha Deni la Taifa katika kipindi cha hadi kufikia Juni 30, 2014 lilikuwa Sh26,487.4 bilioni, deni la ndani likiwa na thamani ya Sh7,144.5 bilioni na deni la nje ni Sh19,342.9 bilioni. Deni hilo linaendelea kukua kila mwaka na kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Machi, 2015, limefikia Dola 14,697.7 milioni, ambazo ni sawa na Sh29.5, wakati deni la ndani limefikia Sh7,509 bilioni.

No comments: