Karagwe. Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Karagwe
imebatilisha ushindi wa wenyeviti 36 wa vitongoji, Kata ya Kiruruma kwa
tiketi ya CCM, baada ya kuridhika kuwa mwenendo wa uchaguzi haukuwa huru
na haki.
Hatua hiyo imetokana na kesi iliyofunguliwa
na wagombea 36 wa Chadema waliopinga kuenguliwa kuwania nafasi za
uenyekiti wa vitongoji katika kata hiyo.
Akisoma hukumu
hiyo jana, Hakimu Victor Bigambo alisema kwa kuzingatia ushahidi
uliotolewa, Mahakama imeridhika pasi na shaka kuwa utaratibu uliotumika
kuwatangaza washindi hao wa CCM haukufuata kanuni na sheria zilizokuwa
zinaongoza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka jana.
Katika
uchaguzi huo, wagombea wote Chadema katika kata hiyo, walienguliwa
baada ya kuwekewa pingamizi la kutumia muhuri wa Katibu wa Chadema kwa
madai kuwa haukuonyesha jina la tawi.
Hakimu Bigambo
alisema kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni, uchaguzi huo ni batili
hivyo nafasi hizo zitangazwe upya na kumwagiza msimamizi wa uchaguzi
Wilaya ya Karagwe kuitisha uchaguzi kuzijaza. Pia, alisema walalamikiwa
wanatakiwa kulipa gharama za uendeshaji kesi hiyo.
Wanachama
hao Chadema walikuwa wakitetewa na Wakili Revocutus Mathayo ambaye
aliieleza Mahakama hiyo kuwa kutokana na kuenguliwa, wateja wake
walipata madhara makubwa ikiwamo ya kisaikolojia na kutoweka kwa amani
kwenye jamii.
Wakili Mathayo alidai kuwa kutokana na
kutowasilisha vielelezo vya kuthibitisha ushindi wa waliotangazwa kutoka
CCM, ni dhahiri kuwa kanuni na sheria zilikiukwa kuwapata washindi hao.
Kesi hiyo hiyo ni miongoni mwa nyingine kadhaa zilizofunguliwa baada ya
uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo mbalimbali nchini kwa
ukiukaji wa taratibu.
Katika maeneo hayo mamia ya
wagombea wa CCM walipita bila kupingwa kutokana na kilichoelezwa kuwa
wenzao wa Chadema walikosa sifa kwa kukosea kujaza fomu au kuidhinishwa
na maofisa wa chama wasioruhusiwa kikanuni.
No comments:
Post a Comment