CCM ngoma mbichi Dodoma - LEKULE

Breaking

21 May 2015

CCM ngoma mbichi Dodoma

Dodoma. Mambo yanaonekana kuwa mazito kwa CCM ambayo inajiandaa kufanya moja ya mikutano yake muhimu ya vyombo vyake vya juu kabla ya kuanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu baada ya Sekretarieti kukutana hadi usiku wa manane kufanya maandalizi ya vikao hivyo.
Vyombo hivyo vya juu vya CCM, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vitakutana kuanzia kesho kupanga utaratibu wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu, huku vikitakiwa kufanya maamuzi mazito kuhusu makada wanaotaka kuwania urais ambao wamefungiwa pamoja na mawakala ambao wamekuwa wakiendesha kampeni za kutaka wagombea hao waungwe mkono.
Sekretarieti ya chama hicho ilikutana kuanzia juzi hadi usiku wa manane kufanya maandalizi na jana kufuatiwa na Kamati ya Kanuni ambayo inatazama upya kanuni za uchaguzi za chama hicho ambazo zinaweza kuwagusa wagombea wanaoonekana kukiuka taratibu.
Vikao hivyo vinafanya kazi ya kuandaa na kuthibitisha ajenda za vikao vikuu huku ajenda muhimu katika mikutano hiyo ikiwa ni hali ya kisiasa nchini, maandalizi ya uchaguzi mkuu, mchakato wa namna ya kuwapata wagombea wa CCM wa ngazi zote na ratiba ya uchaguzi.
Vikao hivyo pia vitapewa taarifa ya maandalizi ya ilani ya chama na kutoa maoni.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa kikao cha sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kiliketi juzi kuanzia 10:00 jioni hadi sasa 6:00 usiku, lakini hakikumaliza kazi yake, hivyo kitaendelea leo.
“Jana (juzi) walikaa hadi sasa 6:00 usiku na leo (jana) wamepumzika, lakini kesho (leo) wataendelea tena na vikao vya Sekretarieti,” alisema mmoja wa maofisa wa chama hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji.
Habari zaidi kutoka ndani ya ofisi za makao makuu ya CCM, maarufu kama White House zinasema kuwa wajumbe wa Kamati ya Kanuni walikutana jana jioni kuangalia upya kanuni za uchaguzi.
Hata hivyo, chanzo kingine cha habari kilieleleza kuwa huenda kamati hiyo ya kanuni ndiyo ile ile inayoandaa ilani ya uchaguzi ya CCM 2015-2020 inayoongozwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, ambaye pia anatajwa kuwania urais.
Wakati wajumbe hao wakiendelea na vikao ndani ya ofisi hiyo ya makao makuu, magari ya viongozi wa Serikali ambao ni wajumbe yalionekana nje yakiwamo ya mawaziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika (Wasira), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu Hassan.
Wakati vikao hivyo vikiendelea wajumbe, wengine wa Halmashauri Kuu, Kamati Kuu na maofisa wa chama walitarajiwa kuanza kuingia mjini hapa jana jioni kutoka maeneo mbalimbali, huku wapambe wa wagombea urais wakiwa wameshaanza kuingia.
Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati Kuu ya CCM, kinatarajiwa kufanyika kesho, kikifuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokaa kwa siku mbili.
Nje ya jengo la White House, wajasiriamali wanaouza mavazi ya CCM na vitu vingine walikuwa wamepanga bidhaa zao pembeni ya ukuta wa jengo hilo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema vikao vinavyoendelea mjini hapa ni vya maandalizi na hawezi kuvitaja, lakini akasisitiza kuwa ratiba ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu iko pale pale.
Wiki iliyopita CCM ilieleza kuwa mchakato wa kuwachunguza makada sita waliofungiwa haujakamilika na kwamba adhabu yao inaweza kuendelea hata baada ya vikao hivyo vya juu.
Nape alikaririwa na gazeti hili wiki iliyopita akisema: “Mchakato unaweza kuchukua miezi mitano, wiki mbili, mwaka au miaka na kama mchakato haujaisha, wataendelea na adhabu yao.”
Alisema hata kikao cha Kamati Kuu cha kesho kinaweza kujadili au kutojadili, akifafanua kuwa madhumuni ya mkutano huo siyo kufunga wala kumfungua kada yeyote kutoka katika kifungo chake, bali ni kwa ajili ya mambo ya chama na Uchaguzi Mkuu.
Nape alisema chama kinafuata kanuni ambazo zinasema mtu akiwa kwenye kifungo, haruhusiwi kugombea nafasi yoyote akisema hiyo ilitungwa hata kabla yeye hajazaliwa.
“Nasisitiza ni kanuni na wala si mimi, nasisitiza pia kuwa sijazuia watu kuchukua fomu bali chama kinafuata kanuni,” alisema.
Alisema kada yeyote wa CCM akiamua kufanya kampeni kabla ya muda ataadhibiwa, lakini akisubiri hana hatia kwani kinachogomba ni kanuni.
Maelezo hayo ya Nape yalikuwa yanalenga uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kuwafungia kwa miezi 12 vigogo wa chama hicho uliotolewa Februari mwaka jana kwa kubainika kuanza kampeni kabla ya wakati na kukiuka maadili ya chama. Waliokumbwa na adhabu hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na William Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema.
Ukiacha makada hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye ni naibu waziri wa fedha, alilimwa barua kwa kuendesha mikutano ya kibinafsi katika maeneo mbalimbali, hali iliyotafsiriwa kama kuanza kampeni za urais.
Kati yao, Wasira na Makamba wameshatangaza nia ya kugombea urais wakati Lowassa amepanga kutangaza kuanza ‘safari ya matumaini’ Jumanne ijayo mjini Arusha.
Kuhusu uamuzi wa kutangaza nia, Nape alisema: “Chama hakiwezi kuacha watu watangaze kiholela… wengine kuzimu, wengine mbinguni. Namna hii tutakiharibu chama,” alisema. Alifafanua kuwa kutangaza kama unagombea si vibaya, lakini matendo yanayoambatana na kauli yako ndiyo ambayo chama hakiyataki.
Alisema mchakato wa makada hao sita upo chini ya kamati ya nidhamu lakini hata hivyo, huenda kikao cha Kamati Kuu ya CCM kikayazungumza mambo ya vigogo hao.
Vikao vitatoa ratiba ya mchakato wa uchaguzi wa urais na wagombea wengine, vitapanga tarehe ya kuchukua fomu, kuzunguka kutafuta wadhamini, kutengeneza kanuni za kuwapata wagombea na mambo mengine yanayohusu wagombea.

No comments: