Moshi. Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa
Wilaya ya Rombo, Lemrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
ya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa
kusimamia sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli
hiyo jana alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai
kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi,
gazeti hili liliripoti habari iliyomkariri Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi
ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya
kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na
ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa
pombe haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa
lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo
ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani la
Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa kama eneo linalohitaji kutazamwa
kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi
wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao
kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo,”
alisema Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya
wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya
kukamata pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili
zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa siyo
sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi huo au wanawake
wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni
wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao
wana shida hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” alisema.
Alisema,
“Haiwezekani mtu mmoja aliyehojiwa akawakilisha wanaume au wanawake
wenye matatizo hayo. Kauli hiyo imewadhalilisha wanaume na wanawake
ambao hawahusiki na tatizo hilo.”
“DC ndiye mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama aliyepaswa kusimamia sheria. Mwenyekiti
wa halmashauri, naye anawajibika. Kama wameshindwa kazi waachie ngazi.
“Siungi
mkono unywaji holela wa pombe ambazo hazina viwango vya TBS. Kama kuna
mtu ana tatizo la tendo la ndoa ajitokeza tumjue. Hili jambo limenifanya
nipokea simu nyingi sana,” alilalamika Selasini.
Selasini
alisema inawezekana hakuna mwananchi wake mwenye tatizo hilo kwa vile
hakuna utafiti wala majina ya waathirika na alimtaka Kipuyo kuomba radhi
kwa kauli yake hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama naye aliwahi kutoa kauli inayofanana na ya
Kipuyo aliposema wapo baadhi ya wanandoa wilayani humo wanalala “mzungu
wa nne”.
No comments:
Post a Comment