KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida, mamia ya wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma
katika shule za msingi nchini Kenya, wameripotiwa kufukuzwa nchini humo.
Tayari
50 kati yao, wamerejeshwa nchini huku wengine kadhaa wakiwa bado
wamekwama katika eneo la Narok Magharibi. Baadhi ya walioathirika ni
wale ambao wako katika hatua za mwisho za kuhitimisha elimu yao ya
msingi katika darasa la nane.
Vijana
hao wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza shule Oktoba mwaka
huu ; na kufukuzwa kwao kunawaweka katika wakati mgumu zaidi kimasomo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa alikiri kuwepo na tatizo hilo na aliueleza mtandao huu jana kuwa: “Ni
kweli wanafunzi wetu waliokuwa wanasoma Kenya wamefukuzwa nchini humo
na 44 kati yao wamesharudi nchini, ila tuna wasiwasi kwamba mamia
wengine watakuwa bado wamekwama huko na tuko mbioni kuwafuatilia zaidi.”
Meneja
wa Baraza la Wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro, Peter Metele naye
alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa yeye ndiye anayefanya
kazi ya kwenda kuwachukua wanafunzi waliotimuliwa Kenya.
Imeelezwa
kuwa chanzo cha kutimuliwa kwa watoto hao ni msuguano, ulioibuka baada
ya kufanyika kwa operesheni maalumu ya kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka
nchi jirani ya Kenya, wanaodaiwa kuvamia maeneo ya Loliondo na Sale.
Hadi
sasa watoto 27 wamehifadhiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Cobra
katika eneo la Wasso, Loliondo. Wengine takribani 10 wamepelekwa kwenye
kata ya Arash na waliobakia wako majumbani mwao.
“Tumewahifadhi
kwenye nyumba za kulala wageni kwa sababu kuna wale wanaotoka vijiji
vya mbali sana na tunataka tujitahidi kufanya mazungumzo na viongozi wa
upande wa Kenya ili waruhusiwe kurejea mashuleni, iwapo tutafanikiwa
basi iwe rahisi kuwarudisha Kenya,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Metili.
Imedaiwa
kuwa wanafunzi waliofanikiwa kurejeshwa ni wale wanaodhaminiwa na
Baraza la Wafugaji na wale waliopelekwa na taasisi mbalimbali, ambao
ilikuwa rahisi kutumiwa usafiri, ila kwa waliopelekwa na wazazi wao,
bado wamekwama Kenya.
“Tulishafanya
mazungumzo ya awali na viongozi wa upande wa Kenya siku ya tarehe 12
Mei mwaka huu, lakini ingawa tulikubaliana mengi, ikiwemo
wafanyabiashara wetu kuruhusiwa kupeleka bidhaa Kenya inaonekana kuwa
wananchi wa Narok wao wana maamuzi yao tofauti na serikali yao hivyo
wanasisitiza kuendeleza mzozo, na sasa wameamua kuongeza tatizo kwa
kuwatimua watoto,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa
upande wake, Katibu wa Baraza la Wafugaji, Ngorongoro, James ole
Moringe alisema baraza hilo pia linafanya jitihada za kukutana na
viongozi wa Narok na walimu wa huko ili kupata mwafaka wa suala hilo.
Akisimulia,
mmoja wa wanafunzi hao, Lilian Peter (14) anayesoma darasa la Nane
katika Shule ya Ilkerin-Loita, alisema Chifu wa eneo hilo alifika
shuleni kwao na kuwaita walimu ofisini, kisha baadaye Mwalimu Mkuu, Abel
Githinji alianza kuingia madarasani na kuwatoa wanafunzi wote wa
Kitanzania huku akiwaagiza wafungashe virago.
Wengi
wa wanafunzi hao ni wale wanaotoka kwenye tarafa mbalimbali za wilaya
ya Ngorongoro, ambayo imepakana moja kwa moja na Kaunti au Jimbo la
Narok, Kenya.
Mwanafunzi
mwingine, Naini Petey ambaye anasema wenzao wanaosoma shule nyingine ya
Naikara, pia walifukuzwa na wengi wao bado wamekwama nchini Kenya,
wakisubiri wazazi au wafadhili waende kuwachukua.
Juhudi
za kuwapata mawaziri wenye dhamana ya mahusiano ya kimataifa, Bernard
Membe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Dk
Harrison Mwakyembe wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
hawakupatikana katika ofisi zao, kwa njia za simu na hata bungeni Dodoma
kuweza kuzungumzia suala hilo.
No comments:
Post a Comment