CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ratiba ya vikao vya chama hicho
kuanza mwezi huu ikionyesha mchakato wa kuchukua fomu za kuwania
kugombea urais utafanyika wakati makada wake sita waliofungiwa
wakiendelea kuwa kifungoni.
Akizungumza na gazeti la Mtanzania jana, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baada ya ratiba ya uchaguzi kutangazwa ndani ya chama hicho, wana CCM watatakiwa kuendelea kuheshimu taratibu na sheria za chama chao.
Akizungumza na gazeti la Mtanzania jana, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baada ya ratiba ya uchaguzi kutangazwa ndani ya chama hicho, wana CCM watatakiwa kuendelea kuheshimu taratibu na sheria za chama chao.
Februari 18, mwaka jana CCM iliwawapa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja
makada wake sita wa chama hicho ambao walidaiwa kuanza kampeni mapema za
urais nao ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushiriano wa Kimataifa Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu
Frederick Sumaye, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Stephen Wasira pamoja na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba.
Katika mazungumzo ya Nape Nnauye na gazeti la Mtanzania, mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Swali: Baada ya kutolewa ratiba utaratibu utakuwaje?
Jibu: Wana CCM watafuata ratiba itakayotolewa kwa sababu haiwapi watu
uhuru wa kufanya wanavyotaka na hii ni sawa na mpira. Kwa mfano, leo TFF
(Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) likisema ligi kuu itaanza Juni,
hamuwezi mkaanza Mei.
“Sisi tutakachotoa ni ratiba itakayosema tarehe fulani mpaka tarehe
fulani ni siku ya kuchukua fomu za udiwani na tarehe fulani mpaka tarehe
fulani ni siku za kuchukua fomu za ubunge.
“Ratiba itaonyesha tarehe fulani ni siku za kuchukua fomu za
wawakilishi, tarehe fulani ni Rais wa Zanzibar na tarehe fulani ni
kuchukua fomu kwa ajili ya mgombea nafasi ya urais wa Jamuhuri ya
Muungano.
“Mkishachukua fomu, mnazirudisha, mkizirudisha, mchakato wa kuchuja majina utaendelea mpaka tutakapompata mgombea wetu.
“Hiyo ndiyo ratiba yetu, hiyo ratiba haifuti mambo mengine, kama yapo
yaliyokuwa yakiendelea, likiwapo la maadili, mambo ya adhabu, mambo ya
nini, taratibu zake ni tofauti.
“Sisi tunashughulika na ratiba, kama hayo mambo ya adhabu yatashughulikiwa lini, basi hiyo ni ajenda nyingine.
Swali: Mnafikia hatua ya kutoa ratiba ya kuanza mchakato wa kugombea
wakati makada wenu sita mliowafungia hamjawafungulia, nini hatima yao?
Jibu: Hatima yao kama hawatafunguliwa, wataendelea kubaki kifungoni,
wale walio huru wataendelea kushiriki mchakato.
"Kama kifungo kitaendelea
maana yake ni kwamba hawatashiriki mchakato, lakini wakifunguliwa,
wataruhusiwa kushiriki. Hii hesabu ni rahisi sana, mimi sijui kwa nini
hamuielewi.
Swali: Adhabu yao ilikuwa miezi 12 na ilishakwisha kwa nini wanaendelea kubaki kifungoni?
Jibu: "Adhabu haijaisha, kanuni iko wazi, inasema watatumikia adhabu kwa
kipindi kisichopungua miezi 12 siyo kisichozidi miezi 12 ni
kisichopungua miezi 12.
“Kwa hiyo, inaweza kuwa miezi 12, 13, 14, 15, 20, 25, 30, nenda kasome
vizuri kanuni na imeeleza vizuri, kipindi kisichopungua miezi 12.
“Umeuliza kama ratiba ikitoka wanakuwa huru, nasema hapana. Kama
wasipofunguliwa maana yake wanaendelea kubaki kifungoni, wakibaki
kifungoni maana yake hawaruhusiwi kushirki mchakato, mfungwa hapigi
kura, hiyo ndiyo CCM ni zaidi ya ujuavyo."
Jana, Nape alikaririwa na vyombo vya habari akisema CCM itaanza vikao vyake Mei 18 hadi 22 mwaka huu mjini Dodoma.
Alisema vikao hivyo vitajadili ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea
udiwani, uwakilishi, ubunge, urais wa Zanzibar na urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kazi nyingine itakayofanyika ni kupitia rasimu ya kwanza ya maboresho ya
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kujadili mapendekezo ya
uboreshaji wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Pia vikao hivyo vitajadili jinsi CCM itakavyofanikisha ushiriki na
ushindi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao hivyo vitaanza rasmi Mei 18 hadi 19,
kitafanyika kikao cha Sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahman Kinana
Mei 20, kikao cha Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa Rais Jakaya
Kikwete na Mei 21 mpaka 22 kutakuwa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC).
Vikao hivyo vitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Makao Makuu Dodoma maarufu kama ‘Whitehouse’.
No comments:
Post a Comment