MACHAFUKO YA BURUNDI YANATUGUSA; NKURUNZIZA AELEZWE UKWELI - LEKULE

Breaking

12 May 2015

MACHAFUKO YA BURUNDI YANATUGUSA; NKURUNZIZA AELEZWE UKWELI


NIANZE makala haya kwa kumsifu Mungu aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana, aliyeumba mbingu na nchi, hakika ahimidiwe daima.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliposema kuwa vita vya karne ya 21 havitakuwa tena baina ya mataifa bali wenyewe kwa wenyewe aliona mbali sana. Tangu kauli hiyo ya busara ilipotamkwa tumeshuhudia kuchinjana kwa wananchi wa Burundi, Congo, Rwanda na Somalia ambako sasa kumevuka mipaka na kuwa ugaidi.

Utabiri wa Mwalimu tumeuona Nigeria, Mali, Kenya na Uganda, lakini hata na Afrika Kusini tumeshuhudia wenyeji wakiwabagua wageni!Hawakumbiki kabisa kwamba ubaguzi wanaoufanya kuwapiga wageni ni ukaburu uleule tulioupinga zamani.Ndugu zangu, moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Burundi, hivi sasa ipo katika hatari ya kurejea katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Tanzania tunaumia kwani wakimbizi wanaingia kwetu. Hili viongozi wa Burundi wanajua.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa nchini Burundi maandamano mfululizo yameikumba nchi hiyo na tayari kumeripotiwa kuwapo kwa zaidi ya wakimbizi 10,000 wa Kirundi wapo nchini Rwanda na zaidi ya 1,000 wamekuwa wakiingia Tanzania, hususan Wilaya za Ngara na Kibondo.

Chanzo kikuu cha maandamano na machafuko hayo ni dhamira ya Rais Pierre Nkurunziza wa huko kuwa atawania tena nafasi ya urais nchini humo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu kwa kipindi kingine na kwa mara ya tatu.

Viongozi wa upinzani na asasi zisizo za kiserikali nchini Burundi wanaamini kuwa kwa Nkurunziza kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya Burundi inayoelekeza kuwa rais atadumu katika madaraka hayo kwa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano.

Lakini Nkurunziza anajitetea kwa kujenga hoja akisema kwamba kipindi chake cha kwanza cha uongozi, hakuchaguliwa na wananchi bali na wabunge ndiyo waliomchagua kuongoza nchi. Itakumbukwa kwamba mwaka 2005 Nkurunziza aliingia madarakani baada ya shinikizo kubwa la kimataifa na makubaliano ya Arusha kumaliza utawala wa Pierre Buyoya.

Kwa maana hiyo, kwa tafsiri yake na wapambe wake, uchaguzi wa mwaka 2010 uliofanywa na wananchi ndiyo uliomwingiza madarakani ‘kidemokrasia’ na sasa anataka Warundi na dunia nzima ikubaliane na hesabu zake kwamba kipindi cha 2005 hadi 2010 hakihesabiki; kwamba huo si muhula wa kwanza wa uongozi wake!
Anataka kuiaminisha dunia kuwa kipindi chake cha kwanza cha utawala ni kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. Hivyo kugombea muhula huu ni haki yake.

Binafsi sikubaliani na hesabu hizo za Nkurunziza hasa kwa sababu wapo Warundi pia wasiokubaliana nazo ndiyo maana tunatoa wito kwa viongozi wa EAC kuingilia kati, kumkemea na kumlaani rais mwenzao huyo kwa kusababisha ghasia, vifo na usumbufu mkubwa kwa raia wa Burundi na kutuletea wakimbizi nchini mwetu.

EAC inao uwezo na hata mamlaka ya kuingilia kati na kubadili mwelekeo nchini humo kwa masilahi ya wananchi wa Burundi na raia wote wa EAC. Naamini Mwenyekiti wa EAC, Rais Jakaya Kikwete, anaweza kuitisha mkutano wa dharura kuhusu amani ya Burundi na kumwambia ukweli Nkurunziza na asiporekebisha hali atengwe na EAC.

Namuomba Rais Kikwete asisubiri hadi damu zaidi imwagike ndipo achukue hatua kwani itakuwa ni aibu kwa EAC, Nkurunziza aelezwe kwamba machafuko nchini kwake yanatugusa. Tunatoa ardhi, huduma, ulinzi na rasilimali mbalimbali kwa wananchi ambao wana nchi yao. Tutafurahi kama Rais Kikwete ataondoka madarakani huku Afrika Mashariki yote ikiwa salama.

No comments: