Songea/Dar. Wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma jana
walikumbwa na taharuki baada ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) kuvamia mitaa, ofisi za Serikali na binafsi, benki, nyumba za
ibada na katika maeneo ya biashara wakiwa na silaha huku magari yao
yakiranda kila kona na kuanza kuwapekea watu wote waliyekutana naye huku
wakidai kuonyeshwa vitambulisho.
Hata hivyo, hiyo ni
mara ya kwanza kwa wanajeshi hao kuchukua hatua hiyo ambayo ilielezwa
kuwa ni sehemu ya mazoezi na mafunzo kwa vitendo.
Wananchi
waliohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofuti kufuatia kizaazaa hicho
akiwamo Anastazia Mhale alisema alikutana na wanajeshi hao alipokuwa
akielekea benki, walimsimamisha na kumuuliza maswali kisha wakamfanyia
upekuzi.
“Nilishangaa kusimamishwa na wanajeshi na
kutuhoji maswali huku wakitutaka tuwaonyeshe vitambulisho, hali hii
iliwakuta hata watu waliokwenda wanakwenda sokoni,” alisema Mhale.
Alisema
mbali ya kuwakagua raia, pia walisimamisha kila gari barabarani na
kulifanyia upekuzi sambamba na abiria waliokuwa ndani ya magari hayo.
Erasto Haule alisema: “Hata kama hakuna madhara yoyote wangetutangazia kama wanafanya mazoezi, wametutia hofu kubwa,” alisema.
Alisema baadhi ya watu jana walishindwa kutoka kwenda kuendelea na shughuli zao wakihofi kukamatwa na wanajeshi hao.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alipoulizwa alisema zoezi
hilo ni la kawaida na aliwataka wakazi mjini humo kuwa na amani na
waendelee kufanya shughuli zao kama kawaida.
Gazeti
hili pia liliwashuhudia askari hao wa jeshi wakiwa wametanda eneo lote
la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, lilipotaka kwenda kuonana na mkuu wa
mkoa ili atolee maelezo zoezi hilo.
Alipoulizwa Brigedia Jenerali wa Kamandi ya Kusini, John Chacha alisema hiyo ni sehemu ya mafunzo kwa wanajeshi hao.
Alisema JWTZ hufanya mafunzo mbalimbali ya kujiimarisha ikiwamo ya kulinda miji, maporini na mengineyo.
“Mazoezi
haya yameanza leo (jana) na tutamaliza usiku. Mafunzo hayo ni muhimu
kwetu, yanatoa mbinu za kujihami na uvamizi wa adui yeyote anayeweza
kuingia ndani ya mipaka yetu na kuteka viwanja vya ndege, ofisi nyeti za
Serikali, benki au hospitali kubwa, ndiyo maana tunayafanya mahali
popote,” alisema.
Hata hivyo, Brigedia Chacha alisema
kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, walitoa taarifa katika ofisi zote
kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kwa lengo la kuondoa hofu ambayo
ingeweza kutoa kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment