Dar es Salaam. Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni
limelazimika kupiga kura ili kupitisha mapendekezo ya kuyagawa majimbo
ya uchaguzi kutoka matatu ya awali ili yawe matano kama ilivyopendekezwa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Dalili za
kutofautiana kwa wajumbe hao zilianza kuonekana tangu mwanzo wa kikao
baada ya diwani kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kupendekeza ipigwe kura
ya maoni kama wasingekubaliana.
Majimbo yanayotakiwa kugawanywa ni Ubungo, Kawe na Kinondoni.
Kauli
hiyo ilipingwa na wajumbe kutoka vyama vya upinzani wakiwamo Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye aliamua kutoka
nje ya ukumbi kwa kile alichoeleza kuwa madiwani wa CCM walishafikia
uamuzi kabla ya kuingia ukumbini.
Akizungumza katika
kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Injinia Mussa Natty
aliyataja majimbo mapya kuwa ni Kibamba na Mambwepande na kwamba, uamuzi
huo umefikiwa kwa kuangalia kigezo cha idadi ya watu.
“Ukuaji
wa miji unawafanya wakazi wengi kuhamia katika maeneo ya pembezoni kwa
kasi katika kata za Kibamba, Goba, Bunju, Makubuli, Kimara, Mbweni,
Kunduchi na Mbezi ambayo mwaka 2012 yalichukuliwa kuwa ni ya vijijini,”
alisema Injinia Natty.
Pia, alisema mapendekezo ya
kugawa majimbo hayo yamezingatia mgawanyo wa huduma za kijamii na
kiuchumi kama shule, masoko, huduma za afya na miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake Mdee alisema NEC imekiuka utaratibu wa kugawa
majimbo kwa kuwa Katiba inaitaka tume hiyo kufanya uchunguzi kwanza na
kueleza sababu za kugawa majimbo jambo ambalo halijafanyika.
“Siogopi
kugawanywa kwa majimbo kwa sababu tunapunguziwa mzigo, lakini nahoji
kwanini katika kugawa majimbo baadhi ya kata zimechanganywa? mfano Kata
ya Mwananyamala imewekwa Kawe halafu Kata ya Makumbusho ipo Kinondoni?”
alihoji Mdee.
Mstahiki Meya wa Kinondoni, Yusuph Mwenda
alisema Manispaa ya Kinondoni ina watu milioni 1.8 kwa hiyo kila jimbo
sasa litakuwa na takriban watu laki nne.
Baada ya
kushindwa kufikia muafaka, Mwenda aliwataka wajumbe kupiga kura, ndipo
10 walinyoosha mikono kupinga uamuzi huo huku 20 wakipendekeza majimbo
kugawanywa.
“Walio wengi wameshinda hivyo majimbo
yatagawanywa,” alisema Mwenda. Kwa upande wake Mnyika alisema
hakubaliani na uamuzi wa kugawanywa kwa majimbo yaliyopo na kuongezwa
mengine mawili kwa sababu kufanya hivyo ni kufuja fedha za wananchi.
Akizungumza
baada ya kutoka ukumbini, Mnyika alihoji iweje Serikali iliyopinga kuwa
na serikali tatu kwenye Katiba Inayopendekezwa ije na mawazo ya
kuongeza majimbo mapya 42 nchini nzima.
“Kwenda kama
vipofu ni bora kutokwenda kabisa, naiona hatari kwa tume kuja na maamuzi
tofauti, mwaka 2010 Kinondoni iliomba kuongezwa majimbo mawili
haikupata hata moja, kujadili majimbo matano ni kujilisha upepo,”
alisema Mnyika.
No comments:
Post a Comment