Dodoma. Ni wabunge 68 tu, wakiwamo mawaziri 10, waliokuwa ndani
ya ukumbi wa Bunge wakati chombo hicho cha kutunga sheria kikipitisha
bajeti ya Wizara ya Kilimo na Chakula, lakini uongozi umesema “hakuna
tatizo”.
Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa liwe na wabunge 357 iwapo kumetokea muujiza wakahudhuria wote.
Idadi
hiyo ndogo ya wabunge kwenye kikao muhimu cha kupitisha bajeti imetia
fora kwenye kikao cha 11 cha Bunge la 10 ambalo limetawaliwa na utoro
katika mikutano yake ya mwisho kutokana na akili za watunga sheria hao
kuwa majimboni.
Licha ya idadi hiyo ndogo, bajeti hiyo
ilipitishwa kwa kutumia utaratibu wa “guillotine”, ambao wabunge
hutakiwa na kiti cha Spika kutohoji jambo lolote katika vifungu
mbalimbali vya bajeti husika anapoona havunji sheria.
Utaratibu
huo hutumika wakati muda wa kawaida wa kikao husika au wa nyongeza
unapomaliza huku utaratibu wa kupitisha vifungu ukiwa bado
haujakamilika.
Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa
Bunge, Mussa Azzan Zungu ambaye aliongoza kikao cha jana asubuhi,
alisema: “Bajeti za wizara zinaweza kupitishwa hata kama idadi ya
wabunge ikiwa ndogo. Katika bajeti kuu (wa wizara ya fedha) hapo ni
lazima wabunge wote wawepo, akidi lazima izingatiwe.”
Kanuni
ya 77 ya Bunge inayozungumzia akidi ya wabunge inayohitajika katika
kikao cha Bunge kwa ajili ya kupitisha maamuzi, inaeleza kuwa lazima
wawe zaidi ya nusu ya wabunge wote.
Hata hivyo, iwapo
mbunge atasimama na kuomba muongozo wa Spika kama ataona ikidi ni ndogo,
kiti cha spika kinaweza kutoa uamuzi wa wabunge wote kuhesabiwa na
kisha kuwahoji wabunge kama wataridhia bajeti kupitishwa na idadi hiyo
ama la. Jambo hilo halikutokea jana kwa sababu hakuna mbunge aliyehoji.
Pia,
kanuni ya 146 ya bunge inaeleza kuwa mbunge atakwama kuwa mbunge iwapo
hatahudhuria vikao vitatu mfululizo bila kutoa taarifa rasmi kwa Spika
wa Bunge.
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John
Shibuda alisema kuwa jambo hilo si sawa na kinachofanyika ni “kufunika
kombe mwanaharamu apite”.
“Ninachokiona ni mambo ya
kuburuzwa tu. Yaani ili mradi tu bajeti imepita. Idadi inatakiwa kuwa
nusu au kuzidi,” alisema mbunge huyo wa zamani wa CCM.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja alisema kuwa kanuni za bunge zinaruhusu jambo hilo.
“Bajeti
hizi za wizara siyo mwisho. Kinachozingatiwa zaidi ni bajeti kuu ya
Serikali. Wakati wa kupitisha bajeti hiyo ni lazima akidi izingatiwe,”
alisema Ngeleja ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Jana
wakati Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, kulikuwa na wabunge 39 tu ndani ya
ukumbi wa Bunge, baadaye wakaongezeka hadi 47.
Wakati
Wasira na Naibu wake, Godfrey Zambi wakianza kujibu hoja za wabunge,
ukumbi ulikuwa na wabunge 51 na baadaye waliongezeka wanane.
Mpaka Bunge linakaa kama kamati saa 7:05 mchana kupitisha bajeti hiyo, wabunge walikuwa wamefika 68.
Mawaziri
waliokuwepo bungeni wakati huo ni Wasira, Zambi, George Mkuchika (Ofisi
ya Rais- Utawala Bora), Samuel Sitta (Afrika Mashariki) na Hawa Ghasia
(Ofisi ya Rais-Tamisemi).
Wengine ni Gaudencia Kabaka
(Kazi na Ajira), Mary Nagu (Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu), Profesa
Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi maalum), Adam Malima (Naibu Waziri-
Fedha) na Charles Mwijage (Naibu Waziri-Nishati na Madini).
Kati ya wabunge 68, wa upinzani walikuwa 15 na wa CCM walikuwa 53.
Kutokana
na kufika saa 7:48 mchana huku Bunge likiwa halijamaliza kupitisha
bajeti hiyo, Zungu alilazimika kutumia utaratibu wa ‘guillotine’ wakati
wabunge wakihoji baadhi ya mambo kwenye bajeti hiyo.
No comments:
Post a Comment