Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Bunge kuchunguza madhara ya Operesheni
Tokomeza, James Lembeli, amekosoa ‘mchezo mchafu’ wa serikali
kuwasafisha baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.
Amehoji
kama suala ni kusafishana, kwanini juhudi kama hizo zisitumike
kuwasafisha wengine pia kama Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.
Lowassa alijiuzulu wadhifa wake kutokana na sakata la mtambo wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond, mwaka 2007.
Wengine
waliojiuzulu kufuatia sakata hilo ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir
Karamagi ambao wote walikuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati
tofauti wakati sakata hilo lilipoibuka bungeni mwaka 2008.
Akichangia
hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya
matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2015/16 bungeni
jana, Lembeli alisema, tabia hiyo italeta giza. Alisisitiza tabia ya
kuwasafisha viongozi wachache na kuwaacha wengine ni mbaya.
“Kama kusafishana basi tusafishane wote na siyo watu wachache tu.
“Nchi
hii sasa inaenda kubaya, watu wanawekwa kwenye makundi…kama kusafishana
tusafishane wote na kama siyo hivyo huko tunakoenda kuna giza. Tabia
iliyozuka sasa ya kusafishana na kuwaacha wengine ni mbaya,” alisema Lembeli ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Alisema
licha ya kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge
iliyochunguza sakata la Richmond lililomlazimisha Lowasa ajiuzulu, kwa
sasa haoni sababu za kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Monduli naye
kutosafishwa.
Tokomeza
Alisema
ripoti ya kamati yake ya Tokomeza, haikuwatia hatiani waliokuwa
mawaziri watatu, Dk. Emmanuel Nchimbi-Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi
Hamis Kagasheki-Maliasili na Utalii na Shamsi Vuai Nahodha- Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, isipokuwa waziri mmoja, Dk. Mathayo David
Mathayo-Mifugo na Uvuvi.
“Nimeshtuka
kusikia ripoti ya Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi kuhusu sakata la
Operesheni Tokomeza imesema mawaziri hao hawana makosa…kamati yangu
iliweka bayana kwamba hao hawakuwa na makosa, kuna siri gani hapo,” alihoji na kuongeza:
“Lakini
ripoti hiyo haizungumzii namna ya kuwalipa fidia ndugu wa watu
waliokufa, waliojeruhiwa na kupata ulemavu au kuharibiwa mali zao.”
Alimtaja pia Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kwamba naye pia anahangaika na anastahili kusafishwa.
Tegeta Escrow
Kuhusu
sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema, matokeo ya uchunguzi
uliofanywa na serikali umewasafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi na
kuwaacha wengine.
Alisema
tatizo kubwa la sakata la Akaunti ya Escrow ni wale walioidhinisha
fedha hizo kutolewa na siyo waliwekewa fedha kwenye akaunti zao. Kiasi
cha Sh. bilioni 301 zilichotwa katika akaunti hiyo.
Alisema
wakati akina Prof. Muhongo na Maswi wanasafishwa, akina Prof. Anna
Tibaijuka wanahangaika kwa kutiwa hatiani na sakata hilo.
Alisema
wakati Prof. Tibaijuka anahangaika kutokana na kuwekewa fedha kwenye
akaunti yake, waliohusika kuidhinisha fedha hizo kutoka hawajachukuliwa
hatua yo yote.
Alidai
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, naye anahangaika kwa
kuwekewa fedha hizo, lakini kwa mujibu wa maelezo yake fedha hizo ni
malipo ya kazi aliyokuwa ameifanya ya kutoa ushauri ambayo ni haki yake.
Ezekiel Wenje
Kwa
upande wake, Mbunge wa Nyamagana, Ezakia Wenje, (Chadema), alirusha
kijembe kwa watuhumiwa wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, akisema
haiwezekani kwa mtu ambaye yumo kwenye ‘dili’ la kashfa za fedha
asafishwe.
“Kosa
la escrow ni wale walioidhinisha fedha hizo zitoke. Nikisikia mbunge
yumo katika kila dili halafu anajisifia nje kuwa yeye ni ‘nyoka wa
makengeza’ huyo huwezi kumsafisha,” alisema.
Sugu
Mbunge
wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, amehoji sababu za serikali
kununua magari 700 ya deraya na ya maji ya kuwasha badala ya kuipa fedha
Tume ya Uchaguzi (NEC) isajili wapiga kura.
NEC iko taabani kifedha na imeshindwa kusajili wapiga kura na kununua vifaa vya kusajili kielektroniki (BVR).
Akiongea
kwa mbwembwe na vibwagizo wakati wa kuchangia hotuba hiyo, Mbilinyi
alisema inashangaza kuona kuwa hakuna kipaumbele. Alisema kati ya deraya
(magari yasiyopenya risasi) 700 yanayonunuliwa anaomba 500 yapelekwe
Mbeya ili wayafanyie kazi.
Sugu alisema wapinzani hawana ugomvi na serikali lakini wanachozungumzia ni masuala ya kutetea umma.
Alitoa
mfano wa kura ya maoni wapinzani walisema haitafanyika, lakini serikali
ikang’ang’ania kuwa itapigwa Aprili 30 jambo ambalo halikufanyika.
Aliongeza
kuwa kuna msemo kuwa namba hazidanganyi, lakini watu huongopa hivyo
serikali ya CCM ikubali kuwa hakuna sababu ya kuwadanganya wananchi kwa
vile ukweli unaonekana.
“Wanawake au wanaume wanadanganya, lakini namba haziongopi 2+2 ni sawasawa na 4,” alisema Sugu na kutamba kuwa atashinda uchaguzi wa Oktoba.
Akizungumza kwa kuweka lugha za kimziki kama ‘yaah men’ ‘kamooni’
aliitaka CCM na serikali wasipate hofu (kupaniki) bali wawasikilize na
wapinzani kwa vile nia ni kupeleka mbele maslahi ya nchi.
Mbunge mmoja alikifananisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ng’ombe anayesubiri kuchinjwa.
“CCM inaelekea kibla kama ng’ombe anayesubiri kisu, tumechoka tunataka kunufaika na rasilimali zetu. Ikifika Oktoba tunaichinja,” alisema Kuluthum Mchuchuri (CUF Viti Maalum).
Alisema Watanzania wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu na si sera, bajeti wala mipango ya CCM.
Akitaja baadhi ya mambo yanayoipeleka CCM kibla ni pamoja kujenga maabara wakati hakuna walimu wa sayansi.
Alisema shule kama Mwara, Mwaseni na Umwe mkoani humo hazina walimu lakini maabara zinashinikizwa kujengwa.
Lakini pia vijembe viliendelea pale Zarina Madabida (Viti Maalum CCM), alipowafananisha wapinzani na wake wenza wa CCM, akisema hawawezi kuisifia CCM kwani kufanya hivyo ni sawa na mke mwenza kumsifia mwenzake.
Mbunge
wa NCCR-Mageuzi Kasulu Mjini, Mosses Machali, alipinga kuwa serikali ya
CCM haiwezi kujenga maabara bali ni wananchi ambao wanachangishwa fedha
na wanashiriki kujenga majengo hayo.
Mbunge
wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, aliulipua ujenzi wa barabara ziendazo
haraka jijini Dar es Salaam (Dart) kuwa ni chanzo cha mafuriko.
Alisema
barabara hizo zimegeuza Jangwani kuwa uwanja wa mafuriko na kusababisha
maji kujaa juu ya barabara kutokana na ujenzi na vifusi vilivyomwagwa.
Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, alisema siasa zinazotumia
propaganda za udini na ukabila zinatumika kuichafua Chadema.
Aliyasema
hayo kufuatia maelezo ya Mohamed Amour Chombo (CCM) Magomeni, aliyesema
Ukawa wanashangaza kudai wataondoa ubaguzi wakati ndiyo vinara wa
kubagua.
Chombo
alieleza kuwa Cuf ni wabaguzi kwa asilimia 100, akitaja kuwa huko Pemba
kiongozi akiomba uongozi hawezi kupewa kama anatokea Unguja.
Na hata Unguja ndicho wanachofanya ni wabaguzi na wanachaguana kwa misingi ya U-Cuf na Upemba.
Aliendelea
kusema kuwa, kwa Chadema mtiririko wa uongozi wao unaonyesha jinsi
walivyo watu wa eneo moja, baada ya kumaliza maelezo hayo ilifika fursa
ya Lema kuchangia na akasema Chombo anastahili kupigwa risasi.
Akimshambulia zaidi, alisema ingekuwa ni Korea Kaskazini mbunge kama huyo Waziri wa Ulinzi, angeamuru apigwe risasi.
Alionya kuwa kuendelea kuendesha nchi kwa utaratibu wa udini na ukabila kutasababisha taifa kuparaganyika.
Waziri
wa zamani wa elimu, Prof. Athumani Kapuya, ametahadharisha kuwa sera ya
elimu inayoelekeza Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia taasisi zote za
elimu itahatarisha amani ya taifa.
Alisema sera ya elimu itateketeza amani ya Tanzania na kwamba yanahitajika mapinduzi ya elimu.
No comments:
Post a Comment