MWANAMKE mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Remi Luchoma (30), mkazi
wa kijiji cha Mwamachoma kata ya Mamba wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi,
amekatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana, kisha wakatokomea na
kiganja cha mkono huo kusikojulikana.
Kwa sasa, mtu huyo amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa
alithibitisha kumpokea mama huyo na kwamba anapatiwa matibabu na hali
yake inaendelea vizuri.
Alieleza kuwa tukio la kukatwa mkono wa albino huyo, lilitokea hapo
jana majira ya saa 6 usiku nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji hicho.
Alisema baada ya kukatwa kiganja chake cha mkono wa kulia, albino
huyo alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Mamba, ambapo alipewa rufaa na
kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya matibabu
zaidi.
Alipokewa katika hospitali hiyo ya wilaya saa 10 alfajiri na amelazwa wadi namba mbili .Hali yake inaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Masuma Luchuma ambaye ni kaka wa albino huyo,
alisema tukio hilo la dada yake kukatwa kiganja cha mkono ni la kinyama
na limemsikitisha. Alisema tukio hilo lilitokea kwenye chumba alichokuwa
akiishi albino huyo, mwenye watoto wanne.
Kaka huyo alisema siku ya tukio majira ya saa 6 usiku, alisikia watu
wakivunja mlango wa chumba alichokuwa amelala Remi na baada ya muda
mfupi, alisikia dada yake huyo akipiga mayowe ya kuomba msaada.
Alidai alijaribu kutoka nje ili kumwokoa dada yake huyo, lakini
alishindwa kutoka nje kwa kuwa watu hao walifunga mlango wake kwa nje.
Alisema hali ya kufungiwa ndani, ilimfanya apige kengele ya jembe, kama
ishara ya kuomba msada kwa majirani .
Hali hiyo iliwafanya watu hao, wakimbie na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na msako mkali kuwasaka
waliohusika na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment