Mafuriko Dar: Rais Kikwete Awataka Wakazi Waishio Mabondeni Wahame - LEKULE

Breaking

15 May 2015

Mafuriko Dar: Rais Kikwete Awataka Wakazi Waishio Mabondeni Wahame

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wananchi wanaoishi mabondeni, wakubali kuhama, kwani Serikali itawapatia maeneo yaliyo salama ili kuepukana na adha ya mafuriko kila inapofika msimu wa mvua.
 
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo yaliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, Rais Kikwete aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni, kuacha tabia ya kujenga makazi katika maeneo ya mabonde na mikondo ya maji.
 
“Acheni tabia ya kujenga nyumba katika maeneo yenye mikondo ya maji au mabondeni, maana kila msimu mnakuwa wahanga wa mafuriko ambayo yanawarudisha nyuma kimaendeleo. Mkubali kuhama, serikali itawapatia maeneo ya kuishi yaliyo salama,” alisema Kikwete.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alimweleza Rais Kikwete kuwa eneo la Mkwajuni katika wilaya hiyo, lina jumla ya kaya 680 zenye familia 976 ambazo zipo kwenye mkondo wa maji na ndio zimefurika maji na kutatiza maisha ya wananchi hao.
 
Alisema serikali iliwaamuru wananchi hao, kuondoka mahali hapo na kuwapatia maeneo huko Mabwepande, ambapo jumla ya kaya 102 zilipatiwa viwanja huku nusu ya wananchi wakikaidi na kurudi katika makazi hayo duni yaliyoko mabondeni.
 
“Hawa waliopo ni sehemu ya wananchi waliokaidi kuondoka walipopatiwa viwanja kule Mabwepande, wengine wamesalia kule na wengine wakarudi huku. Hivyo zinahitajika juhudi za pamoja na mkakati wa kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa huru bila ya kuwa na makazi ya watu,” alisema Makonda.
 
Katika eneo la Boko Basihaya, ujenzi holela wa nyumba umesababisha kuziba kwa mkondo wa maji na kusababisha maji kutapakaa na kujaa kwenye makazi ya watu.
 
Akizungumzia tatizo la kujaa maji katika eneo hilo, Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) Kituo cha Boko, Maro Wambura alimwambia Rais Kikwete kuwa ili kuondokana na tatizo hilo, kunahitajika mifereji mikubwa na kuwazuia wananchi kujenga na kuziba mkondo wa maji.
 
“Maji haya yanasababishwa na ujenzi holela wa makazi ya watu. Manispaa inatakiwa iwajibike katika kuhakikisha hakuna ujenzi holela unaoziba njia ya maji,” alisema Wambura.
 
Hata hivyo, Rais Kikwete aliagiza nyumba zote zilizojengwa kwenye mkondo wa maji katika eneo hilo la Boko Basihaya, zibomolewe na kujengwe mfereji mkubwa utakaowezesha maji kwenda baharini moja kwa moja.
 
Akijibu kuhusu hatua za dharura zilizochukuliwa na Manispaa katika kukabiliana na tatizo la kujaa maji katika makazi ya watu, Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alisema walijaribu kuyatoa maji hayo kwa kutumia mashine, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda kutokana na mvua kunyesha mfululizo.
 

Katika eneo la Boko Nyaishozi, Kikwete alimwagiza Mhandisi huyo Kinondoni, kuhakikisha wanajenga mifereji mikubwa ya kupitisha maji na kubomoa nyumba zote zilizopo kwenye mkondo wa maji.

No comments: